Wednesday, January 12, 2011

Wahadhiri UDOM waendeleza mgomo

na Danson Kaijage, Dodoma




WAHADHIRI wa Chuo Kikuu cha Dodoma wameendeleza msimamo wao wa kutoingia madarasani hadi watakapopata maelezo ya kutosha kutoka kwa Rais ama Hazina juu ya marekebisho ya mishahara yao mipya.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanataaluma chuoni hapo (UDOMASA), Paul Loisulie, akizungumza na Tanzania Daima jana nje ya ukumbi wa mikutano katika jengo la utawala la zamani, alisema mkutano wa wanataaluma utaendelea hadi hapo atakapokuja Rais Jakaya Kikwete ama maelezo ya kutosha kutoka Hazina.

Alisema mpaka sasa bado hawajafikia mwafaka, kwani bado hawajaweza kupata maelezo ya kutosha juu ya kutopata mishahara yao kwa wakati lakini pia mishahara hiyo imekuwa na utofauti mkubwa tofauti na kazi yao.

Msimamo huo unatokana na tukio la juzi la wahadhiri kuanzisha mgomo wa kutoingia darasani na kufanya kile walichokiita mkutano endelevu, ili kujadili hatma ya maslahi yao ikiwa ni pamoja na mshahara mpya na fedha za kujikimu.

Alisema uongozi wao tayari umeshaandika barua kwa Rais Kikwete na kupeleka malalamiko yao ambapo nakala wamezituma Ofisi ya Wizara ya Elimu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Makamu wa Rais na Ofisi ya UDOM.

Alisema wahadhiri hawana mpango wa kugoma lakini hawataingia madarasani mpaka hapo watakapopata ufumbuzi wa suala lao kutoka kwa rais.

Loissulie alisema tangu mshahara mpya uanze kulipwa wao kama wafanyakazi wa UDOM hawajawahi kupata fedha hizo ikiwa ni pamoja na zile za kujikimu ambazo ni haki ya kila mwajiriwa.

Loisulie alisema licha ya Hazina kutoa fedha hizo na kuufikia uongozi wa UDOM bado wao kama waajiriwa hawajawahi kulipwa mshahara huo mpya.

Alisema wamelazimika kusimamia msimamo wao baada ya kugundua kuwa wafanyakazi wa UDOM hupewa 'Pay Slip' badala ya kupewa 'Salary Slip' inayotoka Hazina.

Hata hivyo, Makamu Mkuu wa UDOM, Profesa Idris Kikula, alisema madai ya wahadhiri si ya msingi bali ni kutokana na kutokuwa na uelewa.

Alisema madai yao ya kukosa mishahara na fedha za kujikimu ni suala ambalo liko katika hatua ambazo zinaweza kutatuliwa badala ya kuendeleza migomo na kususa kuingia madarasani.

No comments: