Wednesday, January 12, 2011

Umeya Arusha wazidi kuitesa CCM

na Ramadhani Siwayombe, Arusha




UONGOZI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha, umeiomba Ofisi ya Waziri Mkuu kutoa tamko kuhusiana na uchaguzi wa Meya jiji la Arusha, ili kuondoa utata.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari jana Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Onesmo ole Nangole, alisema suluhisho la mgogoro wa uchaguzi wa umeya jiji la Arusha ni Ofisi ya Waziri Mkuu ama Waziri Mkuu mwenyewe kutoa tamko juu ya uchaguzi huo.

Alisema kila uchaguzi una taratibu zake na usimamizi wake na katika uchaguzi wa halmashauri zote uko katika kanuni zinazoandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), hivyo wao ndio wanaopaswa kutoa tamko juu ya hilo.

Alifafanua kimsingi hakuna ugomvi wowote baina ya vyama vya CCM na CHADEMA hadi kuwe na wazo la kusema vikutane kusuluhisha suala hilo ambalo ni la kikanuni na kisheria.

“Uchaguzi wa kumpata meya ulifanyika na kusimamiwa na mkurugenzi na matokeo kutangazwa na msimamizi ambaye alikuwa mkurugenzi; kutokana na hali iliyojitokeza naomba Waziri Mkuu atoe tamko ili kumaliza tatizo,’’ alisema Nangole.

Naye Katibu Mkuu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu, alisema anashangazwa na utata unaojitokeza kuhusiana na yeye kuwa mbunge Arusha wakati alipigiwa kura mkoani Tanga.

Alisema kila chama cha siasa kina utaratibu wake katika kupata wabunge wake wa viti maalumu na kuwapangia mahala pa kufanyia kazi, hivyo chama chake kimempangia kufanya kazi mkoa wa Arusha na ndivyo kilivyowasilisha ofisi ya Bunge.

Akitolea mfano CHADEMA alisema wao kama chama walikuwa na utaratibu wao kupata wabunge wa viti maalumu na kuwapangia mahala pa kufanyia kazi na ndio maana wabunge kama Lucy Owenya na Grace Kiwelu wa Moshi wamepangiwa wilaya ya Hai ambako ndiko walikopigia kura katika baraza la madiwani.

Aidha, akizungumzia tamko la Makamu Mwenyekiti wa chama hicho na Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela, kumtaka awaombe radhi maaskofu kwa tamko lake kuwataka wavue majoho ya uaskofu na waingie katika siasa, Chatanda alisema hayo ni mawazo ya Malecela.

“Nasema hivi hayo ni mawazo yake na mimi namheshimu mzee wetu huyo, hata hivyo siwezi kuomba radhi kutokana na mawazo binafsi ya mtu. Mimi naamini nilichokisema ni sahihi,’’ alisema Chatanda.

Baada ya maaskofu mkoa wa Arusha kutoa tamko la kutomtambua meya wa Arusha na kuwa hawatatoa ushirikiano kwake, Chatanda naye alitoa tamko kuwataka maaskofu hao kuvua majoho yao na kujiingiza katika siasa.

No comments: