Wednesday, January 12, 2011

Kila la kheri Mapinduzi ya Zanzibar

LEO Watanzania tunaadhimisha siku ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo ni sehemu moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Januari 12, 1964, siku kama ya leo, yalitokea Mapinduzi yaliyouondoa utawala wa Sultan kwenye kisiwa cha Zanzibar; Mapinduzi ambayo yalitekelezwa na Wazanzibari weusi tena kwa kutumia silaha za jadi kama mapanga, majambia na kadhalika.

Ulikuwa ni ujasiri wa hali ya juu kuamua kupambana na askari wa Sultan ambao walikuwa na silaha za moto na hatimaye wazalendo wakashinda vita ile na kuuondosha utwana wa wana Zanzibar.

Kwa miaka 48 sasa Zanzibar imekuwa huru, miezi zaidi kidogo ya mitatu, ikiwa nchi inayojitegemea; na miaka 47 na ushehe ikiwa ndani ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar unaoitwa Tanzania.

Tunachukua nafasi hii kuwapongeza Watanzania wote na hasa mashujaa waliojitoa mhanga kuundosha utawala wa Sultan visiwani humo.

Hata hivyo, tunavyosherehekea miaka hiyo 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar ni vema tukakumbushana kwamba maendeleo ya visiwa hivyo yakilinganishwa na umri wa kujitawala wa miaka 48 hayalingani kabisa.

Miaka 48 ni mingi na tungetarajia kuona maendeleo makubwa yakiwa yamefanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ); umaskini, ujinga na maradhi vimeendelea kuwa matatizo makuu visiwani humo.

Zanzibar ilipaswa kuwa na maendeleo makubwa hasa tukitilia maanani raslimali zilizopo kama ardhi yenye rutuba na hali ya hewa nzuri kwa kilimo (cha mazao ya biashara hasa karafuu), bandari, vivutio vya utalii ikiwemo pwani ya kuvutia ya Bahari ya Hindi inayofaa pia kwa shughuli za uvuvi na uwezekano wa kupatikana kwa mafuta.

Tunaamini kama raslimali zote zilizopo kisiwani humo zingetumika vizuri kuiingizia SMZ mapato na kisha mapato kugawanywa kwa usawa katika kufanikisha miradi ya maendeleo kwa wananchi wa maeneo yote ndani ya visiwa hivyo, basi Wazanzibari na Zanzibar yetu ingekuwa na maendeleo makubwa na ingestahili hadhi ya kuitwa Dubai ya Afrika.

Kwa maoni yetu, chanzo kikuu cha umaskini ulioko Zanzibar leo hii ni ukosefu wa uwajibikaji wa kutosha ndani ya serikali na mgawanyo mbaya wa raslimali za visiwa hivyo katika kushughulikia maendeleo ya wananchi, huku kero za Muungano nazo zikichangia kwa upande mwingine.

Aidha, matatizo ya kisiasa yaliyokikumba kisiwa hicho ndani ya uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995 kwa kiasi kikubwa yalichangia kukwamisha harakati za maendeleo kwani hakukuwa na amani ya kutosha wala umoja wa kitaifa ambao ni muhimu kwa maendeleo.

Kwa hiyo, Tanzania Daima tukiwa chombo huru cha habari kinachopigania haki, uhuru na maendeleo ya Watanzania wote, wa bara na visiwani, tunawasilisha salamu zetu za kheri katika maadhimisho haya ya Mapinduzi ya Zanzibar, tukipongeza kufikiwa kwa muafaka wa kisiasa visiwani humo lakini pia tunawahamasisha Watanzania wa Zanzibar kufuatilia na kusimamia uwajibikaji wa serikali iliyopo ili iwajibike kwao na kuwaletea maendeleo wanayoyastahili kulingana na utajiri wa visiwa hivyo.

Tunawahimiza viongozi wa serikali ya umoja wa kitaifa huko Zanzibar kuharakisha maendeleo ya visiwa hivyo kwa kupiga vita ubadhirifu na ufisadi, kusisitiza utawala bora na kubuni mipango ya maendeleo kwa faida ya watu wa Zanzibar.

No comments: