Wednesday, January 12, 2011

Uchaguzi kwa Watanzania haujaisha

M. M. Mwanakijiji
TUNAAMBIWA kuwa “uchaguzi umekwisha” hivyo tusiendelee na malumbano ya kisiasa. Tuaambiwa “uchaguzi umekwisha” na kuwa tuendelee na mambo mengine.

Na wengine wanasema “uchaguzi umekwisha” wakimaanisha kuwa wananchi wasifuatilie mambo yanayofanywa na viongozi wao na serikali yao kwani kwa kuyafuatilia kwa karibu ni sawasawa na kuendeleza kampeni za kisiasa.

Mawazo ya “uchaguzi umekwisha” yameanishwa vizuri na Rais Kikwete katika hotuba yake ya mwaka mpya ambapo alinukuliwa kusema kuwa “Naomba kurudia kukumbusha kuwa uchaguzi ulishaisha Oktoba 31, 2010 na malumbano ya kampeni za uchaguzi yalimalizika wakati ule. Sasa ni wakati wa kuendelea kufanya shughuli zetu za kawaida za kujiletea maendeleo yetu wenyewe na ya nchi yetu. Kuendeleza malumbano na kuendelea kuishi kama vile kampeni za uchaguzi bado zinaendelea si sahihi hata kidogo.”

Ina maana gani kusema kuwa “uchaguzi umeisha”? Wanapotuambia kuwa “uchaguzi umeisha” maana yake ni kuwa wananchi wasifuatilie siasa za watawala. Hii ina maana ya kwamba wananchi wanasababu ya kufuatilia siasa za nchi yao wakati wa mwaka wa uchaguzi au wakati wa kampeni. Hivyo wale wanaotaka wananchi wasiwafuatilie na kuwahoji, wanataka watu wakubali tu kuwa uchaguzi umeisha?

Wanaposema “uchaguzi umeisha” wanachotaka kusema ni kuwa tuwaache watawale wapendavyo. Kwamba, tukihoji maamuzi yao, tukiuliza kauli zao au tukiwapinga tutaonekana kuwa tunaendeleza “malumbano” ya kisiasa.

Hivyo, jambo jema kwao ( au kwetu kwa maoni yao) ni kuwa tuwaache wafanya kazi zao, waseme wanalosema, watende wanavyotaka; tusiwahoji au kuwapinga. Wanachotaka ni kuwa tuwape uwanja huru wa wao kutawala wanavyopenda kwani kwa vile wao ndio wako madarakani na wameshinda uchaguzi basi tuwaache wafanye tu wanavyotaka na tusubiri hadi mwaka mwingine wa uchaguzi.

Wanaposema “uchaguzi umekwisha” wanachotaka kutuambia ni kuwa wao waendelee na siasa sisi wengine tusiendelee nazo.

Yaani, wao watamke jina la chama chao wanavyopenda, wao watangaze sera zao bila kuhojiwa na kuwa wao wajiimarishe wakitumia mgongo wa serikali huku wengine wakikaa kimya kwa vile “uchaguzi umekwisha”.

Wanachotaka ni kuwa wao waimarike kama chama cha siasa baada ya kibano walichokipata katika uchaguzi uliopita ili hatimaye wajipange vizuri.

Hivyo, wanachotaka ni kuwa vyama vingine, wanasiasa na wanaharakati wengine wakae kimya huko wao watawala wakiendelea kujiimarisha na kujijenga kisiasa.

Ndiyo maana wanataka wengine waache malumbano ya siasa lakini wao wawendelee nayo. Wao wanataka kuendelea kupiga picha za ki - CCM, kutangazwa na vyombo vya habari n.k lakini wapinzani wakitangazwa itaonekana ni kuendeleza kampeni.

Hilo hata hivyo haliwezekani kwani katika demokrasia siasa ni maisha ya kila siku. Huwezi kufuta siasa kwa siku moja au kwa miezi hadi wakati wa kampeni. Siasa ni maisha ya watu, ni maamuzi ya kila siku na ni matokeo ya maamuzi hayo ya kila siku. Siasa ni sawasawa na pumzi ya kila siku ya taifa, hivyo haiwezi kutenganishwa na maisha ya taifa hilo. Hivyo, haiwezekani kuacha siasa.

Lakini ukweli pia ni kuwa mwisho wa uchaguzi mmoja ndio mwanzo wa uchaguzi mwingine.

Kitu ambacho kimefikia kikomo mwaka 2010 ilikuwa ni kupiga kura siyo uchaguzi wenyewe. Uchaguzi kwa Watanzania haujaisha bado kwani kila siku wanajikuta wanafanya uchaguzi mpya au wanaendelea na uchaguzi ule ule. Walimaliza kupiga kura siku ile lakini wengine baada ya matokeo ya uchaguzi wamejikuta wanajutia uchaguzi huo na sasa wanaanza kufikiria uchaguzi mpya.

Yote hiyo ni sehemu ya uchaguzi wa kudumu kwani ni katika kufuatilia siasa za nchi yao ndivyo wanavyozidi kujua mwelekeo wao wa kisiasa uwe vipi.

Ni katika kusikilia maneno na kuangalia matendo ya viongozi wao Watanzania wanajikuta wanazidi kuelewa kama kura yao ya Oktoba 31, 2010 ilikuwa ni sawa au la.

Na ni kutokana na ukweli huu ndio maana basi tunaweza kusema kwa uhakika mkubwa tu kuwa mwisho wa uchaguzi mmoja ndio mwanzo wa mwingine.

Hii ina maana ya kwamba, kipindi cha kutoka uchaguzi mmoja kwenda mwingine ni kipindi cha kufuatilia na kuangalia wale walioshinda wanatawala vipi.

Siyo kipindi cha kukaa pembeni na kukunja nne na kuwaangalia kutoka kwa mbali tu. La hasha kwani kufanya hivyo ni sawa na kuwaachia mbuzi bustanini ukitegemea watakula magugu tu ati kwa sababu hakuna mbuzi wengine karibu.

Watawala wote duniani wasipoangaliwa na watawaliwa wao kwa karibu wana mwelekeo mmoja wa kuelekea ufisadi, kujinufaisha, kufuja fedha na matumizi mabaya ya madaraka.

Itakuwa ni makosa makubwa sana kwa mpiga kura kukaa pembeni baada ya uchaguzi na kujisahau akitegemea kuwa watawala watafanya yote walioahidi bila ya kuwaangalia kwa karibu.

Ni kwa sababu hiyo basi vyama vya upinzani vina nafasi ya pekee katika kuhakikisha kuwa chama tawala hakilali madarakani au viongozi wake hawatumii nafasi ya wao kuwa madarakani kutawala bila ya kujali. Wapinzani wana jukumu la kuendeleza siasa hadi uchaguzi mwingine unapokuja hawawezi kukaa pembeni na kutokuwa wapinzani vinginevyo waitwe wapinzani wa msimu.

Upinzani wa kweli ni kufuatilia serikali iliyoingia madarakani kuanzia siku ile walipoapishwa kuingia madarakani. Upinzani wa kweli na imara ni ule ambao haufumbi macho hata sekunde moja ati kwa vile kupiga kura kulimalizika.

Kutokana na ukweli huu Chama cha Mapinduzi (CCM), hakina budi kutambua kuwa siasa hazijaisha kwa sababu siku ya kupiga kura imepita. Viongozi wake ni lazima watambue kuwa wanasiasa wa upinzani hawawezi na hawapaswi kuacha siasa ati kwa sababu wao (watawala) wanakereka.

Njia pekee ya kunyamazisha upinzani na siasa kuendelea wakati huu ni kwa CCM na Serikali yake kupiga marufuku vyama vyote vya siasa, kukataza waandishi kuandika mambo ya siasa na ikiwezekana kuwatia pingu wanasiasa na waandishi wote ambao wanaendeleza “malumbano ya kisiasa”.

Hiyo ndiyo njia pekee ya kuhakikisha kuwa uchaguzi umekwisha kweli. Nje ya hapo, libeneke la demokrasia linaendelea na litaendelea.

No comments: