Wednesday, January 12, 2011

Tumetapakaa damu hadi nafsini mwetu

Paschally Mayega




RAIS wangu, kama tutaendelea kufikiri hivi tunavyofikiri na kutawala hivi tunavyotawala nina hakika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu yatatimia.

Yametokea mauaji ya kinyama Arusha na bado kuna wanafunzi waliojeruhiwa katika mapambano kati ya wanafunzi wa Chuo Kikuu Dodoma na Polisi wa Serikali.

Bado tena tunasubiri maandamano mengine. Kwa nini tunataka tufike huko? Wote walio makini wanajua kuwa kama wale watu wangeachwa waandamane na wahutubiane hakuna ghasia zozote ambazo zingetokea. Lakini kwa ujinga wa mtu mmoja mikono yetu imetapakaa damu.

Hatupendezi tena mbele ya macho ya mataifa. Tunaonekana wauaji. Tumepandikiza chuki nzito ndani ya mioyo ya watu wetu dhidi yetu. Kutawala kwetu kuna utamu gani tena? Lakini na hukumu ya Mwenyezi Mungu dhidi yetu kwa mauaji haya iko pale pale!

Rais wangu mtu mjinga hufikiri kijinga. Na kwa ujinga huo maisha ya Watanzania yamepotea. Wako wengi watakaobaki vilema siku zote za maisha yao. Mtu mjinga hajifunzi kutokana na yaliyotangulia.

Ni mpinzani gani atakuja kuwa maarufu kama alivyokuwa ndugu Augustino Lyatonga Mrema wa NCCR Mageuzi? Idadi ya mabomu aliyopigwa Mrema na wafuasi wake inapita kiasi. Watu walipigwa na Polisi wengine ni vilema mpaka leo. Mungu bariki, mwana mwema Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa hili alikuwa hai. Alikemea akasema, “Acheni kupiga watu. Huyo anayebebwa muacheni abebwe hata kama wanaombeba watakuwa wanapokezana kama jeneza!”

Julius ulale pema peponi! Mabomu kwa Mrema yalipokoma na umaarufu wa Mrema ukakoma. Leo mwana mwema Lyatonga ukitaka kumsoma kama yuko upinzani mpaka uvae miwani.

Rais wangu tunaambiwa kuwa Yesu Kristu alipoona saa yake imekwisha aliinua macho yake juu akamshukuru Mungu akisema, “Baba nakushukuru kwa kuwa wote ulionipa sijampoteza hata mmoja!” Baba utakapokuwa unaondoka utakabidhi wangapi? Utakuwa umepoteza wangapi? Wote wanaopayuka hivi sasa na kutoa amri za kipuuzi siku yako ya kukabidhi mahesabu mbele ya Mwenyezi Mungu hawatakuwapo.

Siku hiyo utasimama mbele ya haki peke yako! Msaada wako utatoka wapi? Tumeiacha njia ya kweli, tumwombe Mungu atufundishe kufanya ibada.

Mwana mwema aliniandikia akasema, “Mwalimu mkuu tusalie kwakuwa wewe Mungu wako huwa anakusikia!” Tumwombe Mwenyezi Mungu ashushe huruma yake juu ya watu wake, atuondolee viongozi wasio na busara.

Ukurasa wa nane kitabu cha Mwalimu mkuu wa watu tunasoma, “Maandamano yalijumuisha watoto, vijana, wazee, akinamama, na hata vilema na ulemavu wao.

Waliendelea mbele na kukata kushoto kuingia katika barabara iendayo moja kwa moja. Hapo ndipo…lahaula! Walikutana na askari wengi wa kutuliza ghasia waliojisheheneza silaha nzitonzito. Basi bila onyo wala hadhari yoyote, na kwa nguvu kubwa ajabu, askari wale wa kutuliza ghasia walianza kutuliza ghasia ambayo kwa kweli haikuwepo.

Walifyatua risasi za moto. Walifyatua risasi za mpira. Walifyatua mabomu ya machozi. walitumia virungu na silaha nyingine nyingi dhidi ya ule umati. Kwa kufanya hivyo, askari wa kutuliza ghasia wakawa wameanzisha ghasia kubwa.

Ilikuwa tafrani kubwa patashika nguo kuchanika. Traa tra….. traa…bunduki zilifyatuliwa ovyo. Mabomu ya machozi yalilipuliwa na virungu kutembezwa ovyo. Waliopoteza maisha yao waliyapoteza. Waliojeruhiwa walijeruhiwa. Watu walikimbia hovyo kusalimisha maisha yao. Umati ulitawanyika na kusambaa huku na huko. Moshi wa risasi na ule wa kiwandani ulizagaa hovyo hewani.

Patashika yake ilikuwa kubwa na matokeo yake yalimtoa machozi kila aliyekumbuka baadaye. Aliyesimuliwa alishindwa kuelewa ni kwa kiasi gani binadamu anaweza kuwa mkatili kwa binadamu mwenzake.

Askari wa kutuliza ghasia walianzisha ghasia ambazo mwisho wake ulikuwa ni vifo, majeruhi, mateso na vilio vingi vya wale waliokuwa wakizitoa roho zao. Huo ndio ukawa mwisho wa maandamano ya amani”. Hapo serikali ikawa imejichongea yenyewe kwa wananchi.Ndugu Edward Lowassa alishauri wana wema wa Arusha wakae pamoja kama ndugu walipatie ufumbuzi jambo lililowasibu. Mawazo ya mtu mwenye busara. Lakini mwana wa shetani akampuuza. Sasa wana wa nchi hii wanauawa kama nguruwe.

Busara imekosekana katika uongozi wetu. Huyu na mwenzake wa Arusha anayekashfu viongozi wa dini siyo viongozi wanaofaa. Ni watu wa hovyohovyo. Chuki wanayoipandikiza katika mioyo ya wananchi inaelekezwa kwa mkuu wa nchi maana ndiye mwenye dhamana ya kuwaadabisha. Mbele ya wananchi hawa hawana thamani yoyote!

Rais wangu tuambie askari wa serikali walipowafikia waandamanaji walikuta ghasia gani? Walianzaje kutuliza ghasia ambayo haikuwapo? Malaika wa Mungu watoto wadogo nao walifanya ghasia gani? Wasafiri pale stendi walileta ghasia gani? Wote waliadhibiwa. Kosa lao shetani peke yake anajua. Unatulizaje ghasia kwa kumvua mwanamke nguo?

Baba kuua watu hapana. Waache Watanzania katika neema uliyowakuta nayo na Mungu atakubariki. Wameanza kuwa sugu kwa shuluba za polisi. Watakapoyakumbuka maneno ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere risasi za kuua mlizonazo hazitawatosha Watanzania wote.

Mwana mwema Maturo akaandika, “Arusha imekuwa Kenya ndogo. Siyo tena raia bali polisi wanakimbia raia. Ningefurahi kama Kikwete na Makamba wangekuwa Arusha maana ndio waliosababisha hali hii. Kama kuongoza halmashauri wanatumia nguvu hivi, nchi itakuwaje?”

Mtaua wangapi? Wako watakaobaki kwa ajili ya kuwahukumu wahusika. Kweli kweli nawaambieni mwisho wao utakuwa mchungu kuliko shubiri. Nao hawatachagua baba, mama, wala mtoto. Ole! wao watu hawa, kwa maana ingelikuwa bora kwao kama wasingezaliwa!

Josephine Mushumbusi mama mjamzito mwili wake ulitapakaa damu zilizokuwa zinamvuja kutoka kichwani! Wanyama wale walimpiga mama huyu mpaka wakampasua kichwa. Akiwa katika maumivu makali mama yule alilia, “Nipigeni! Niueni! Nitakufa kwa ajili ya kutetea wananchi wengi walio maskini na wanyonge.

Kama nchi imefikia hivi, hali si nzuri…mnanipiga kiasi hiki wakati nimeisha waambia nina ujauzito….hakuna neno. Damu mlioimwaga haitaenda bure. Lazima matunda yake yatapatikana kwani wananchi watapata haki zao. Hata huyo dereva mnayemtoa sadaka damu yake haitaenda bure.”

Katika mateso makali kama haya bado mama huyu hakujililia yeye. Anawalilia wananchi maskini na wanyonge. Mungu atambariki. Kilio hiki alilia Mahlangu mpigania uhuru wa Afrika Kusini alipokuwa anawekwa katika kitanzi tayari kwa kunyongwa na utawala katili wa makaburu.

Alisema: “Damu yangu itakayomwagika itazirutubisha mbegu za mti utakaochipua na kuleta uhuru wa kweli.” Kristu Yesu akiwa katika magumu aliwaambia wale wanawake waliokuwa wanamlilia, “Msinililie mimi, jililieni wenyewe na watoto wenu.” Walio wema huwaza wengine kwanza. Watawala wetu wamepofuliwa na umimi kwanza.

Waliowatuma kutenda unyama huu walibaki katika makasri yao wakiangalia katika runinga vijana wao wakifanya kazi waliyowatuma. Mungu apishe mbali! Wasome ukurasa wa 60 katika Mwalimu Mkuu wa Watu imeandikwa, “Ala kumbe! Kila zama na watu wake.

“Walikuwapo wafalme waliokuwa na mamlaka na majeshi yenye nguvu kupindukia. Watawala walioitawala dunia kwa upanga wa moto. Leo wako wapi? Hawako tena. Wamekwishapita.

“Walikuwepo masultani waliofanya kila aina ya ufirauni, wao wakiuita starehe! Je, leo wako wapi? Hawako tena! Wamekwishapita.

“Walikuwepo majemedari Nduli walioua raia na askari kwa maelfu kwa utashi tu na ujivuni. Lakini je, leo wako wapi? Hawako tena! Wamekwishapita. Na sisi tunapita!” Wako wapi kina Mobutu Sese Seko, Iddi Amin na wenzake? Wote nyama ya udongo! Mpumbavu hudhani yeye ataishi milele!

“Atawalaye kwa upanga atakufa kwa upanga”.

No comments: