Sunday, January 9, 2011

Slaa amkaanga Kikwete

• Ataka iundwe tume ya kuchunguza mauaji Arusha


na Waandishi wetu
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema Rais Jakaya Kikwete, anawahadaa Watanzania kwa kauli za kisanii na utani kwenye masuala nyeti yahusuyo taifa.

Slaa alitoa kauli hiyo siku moja baada ya Rais Kikwete kuwaambia mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini kuwa vurugu zilizotokea mkoani Arusha na kusababisha vifo na majeruhi kwa wafuasi wa CHADEMA ni tukio la bahati mbaya na anaamini litakuwa la kwanza na la mwisho kutokea.

Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili jana, Dk. Slaa alisema Rais Kikwete hakupaswa kutoa kauli kama hiyo wakati huu na badala yake anatakiwa aunde tume huru itakayochunguza undani wa tukio hilo.

Dk. Slaa alisema tume ambayo Rais Kikwete anatakiwa kuunda, iwajumuishe majaji bila kuwahusisha polisi kwa kuwa hawawezi kutenda haki kutokana na kuhusika moja kwa moja katika tukio hilo.

“Kusema kwamba tukio hilo ni bahati mbaya, ni jambo la utani kwa Watanzania na ni usanii, anachotakiwa ni kuunda tume huru itakayochunguza tukio hilo, ambayo itaundwa na majaji bila kuwashirikisha polisi. Najua hawawezi kutenda haki,” alisema.

Alibainisha kuwa vitendo vya polisi kutumia nguvu kupita kiasi vimekuwa vikifanywa mara kwa mara kwa lengo la kuwadhibiti wapinzani, hivyo ni vema wanaohusika wakawajibishwa ili hali hiyo isijitokeze.

Aliongeza kuwa Rais Kikwete, hawezi kuonekana shujaa kama hatafanya jitihada za dhati za kuruhusu vyama vya upinzani kufanya shughuli zake kwa uhuru na uwazi.

“Kila mtu ni shahidi, nguvu zinazotumiwa na ndugu zetu polisi kuwazima wapinzani, hasa maeneo tunayotoa upinzani mkali kwa CCM, Kikwete awawajibishe, si kutoa kauli zisizotekelezeka,” alisema.

Alisema anashangazwa na kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha ya kutaka vyama vya CHADEMA na CCM kuketi mezani ili kumaliza tatizo hili ambalo ameliita ni la kisiasa.

Dk. Slaa alimtaka Rais Kikwete kumfuta kazi Waziri Nahodha, kwa sababu ameshindwa kumudu majukumu yake ya kikatiba.

“Nimeshangazwa sana na kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha, yaani serikali mpaka watu wapigwe na kuuawa ndipo itambue tatizo, nilitegemea Rais Kikwete angemfuta kazi mara moja kwa vile ameshindwa kutimiza kazi yake kikatiba,” aliongeza.

Dk. Slaa na mchumba wake, Josephine, jana walikwenda katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako walifanyiwa uchunguzi wa kina na kurejea nyumbani, kutokana na kujeruhiwa vibaya kwa kupigwa na polisi wakati wa vurugu zilizojitokeza jijini Arusha Jumatano iliyopita.

Mkoani Arusha, Naibu Meya wa jiji hilo, Michael Kivuyo, amejiuzulu wadhifa huo kwa madai hawezi kushikilia nafasi hiyo huku akishuhudia damu ya wananchi waliompa nafasi ya kuingia madarakani ikimwagika kwa sababu ya uroho wa madaraka wa viongozi wa chama tawala (CCM).

Msimamo huo aliutangaza jana, ambapo alisema lengo la kuwania nafasi hiyo ni kuwaletea maendeleo wananchi lakini hawezi kutimiza majukumu yake ikiwa wale anaowatumikia wanauawa au kunyanyaswa pasipo sababu za msingi.

“Mimi nilikuwa na malengo ya kutaka kuleta maendeleo katika Jiji la Arusha wakati nawania nafasi hiyo lakini kwa hali ilivyo sasa nitakuwa msaliti kwa wananchi wa Arusha kama sitajiuzulu, walionichagua wanauawa, sasa kwanini niendelee kung’ang’ania madaraka?” alihoji.

Alibainisha kuwa mara baada ya uchaguzi wa meya na naibu wake kufanyika, alibaini makosa yaliyofanyika katika uchaguzi huo na kuamua kumfuata Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Isidori Shirima, ambapo alimshauri kuzikutanisha pande zote (CCM na CHADEMA) ili kusuluhisha tatizo hilo.

Alisema pamoja na jitihada zake hizo ambazo kwa kiwango kikubwa zililenga kutaka mji wa Arusha uendelee kuwa kitovu cha amani na kivutio cha utalii lakini ushauri wake ulipuuzwa.

Kujiuzulu huko kwa Kivuyo pamoja na matamko yaliyotolewa na viongozi wa dini kutomtambua Meya wa Jiji la Arusha kunakiweka katika wakati mgumu Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kinadaiwa kufanya hila katika uchaguzi wa meya kwa kumjumuisha diwani wa Mkoa wa Tanga kupiga kura za kumchagua Meya wa Arusha.

Hata hivyo Meya wa Jiji la Arusha Gaudence Lyimo (CCM) juzi alinukuliwa na baadhi ya magazeti kuwa hafikirii kujiuzulu licha ya kukabiliwa na shinikizo kutoka kwa watu mbalimbali wa ndani na nje ya Mkoa wa Arusha.

Katika hatua nyingine, Chama cha TLP Mkoa wa Arusha, kimeilaani serikali na Jeshi la Polisi kwa kuhusika na mauaji yaliyotokea wakati walipoamua kuingilia kati na kuvunja maandamano yaliyokuwa yakifanywa na viongozi na wanachama wa CHADEMA Novemba 5, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa chama hicho mkoa na mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho taifa, Leonald Makanzo, alisema wanawataka Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Said Mwema, wajiuzulu nyadhifa zao.

Makanzo alisema kuwa viongozi hao wanapaswa kuchukua uamuzi huo kwa kuwa wao ndio walihusika na kutoa amri ya kuvunja maandamano kwani awali Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha liliyaruhusu.

Alibainisha kuwa ili kuonyesha kuwa TLP, imekerwa na kitendo hicho kilichosababisha damu ya watu isiyo na hatia kumwagika na wengine kufariki dunia, walimuagiza Diwani wa Kata ya Sokoni One, Michael Kivuyo, ambaye alichaguliwa kuwa Naibu Meya kujiuzulu wadhifa wake.

Makanzo alisema uamuzi huo umeamuliwa na sekretarieti ya chama hicho mkoa, umefanywa kwa kuamini kuwa CHADEMA walikuwa wakifanya harakati za kisiasa kupigania ukombozi wa demokrasia hapa nchini.

Alisema kuwa TLP ni wana mageuzi na wanaunga mkono jitihada zilizokuwa zikifanywa na CHADEMA, ambayo ilikumbana na nguvu ovu za polisi, ambao waliamua kutumia mabomu ya machozi na risasi za moto kukabiliana na waandamanaji.

No comments: