Wednesday, January 12, 2011

Mkurugenzi Manispaa ya Arusha anasubiri nini?

Ruhazi Ruhazi
KWA mara ya kwanza upuuzi wa watendaji wanaopewa mamlaka ya kusimamia uchaguzi yameacha kovu la aina yake na kuchafua demokrasia nchini, hususan Tanzania Bara baada ya watu watatu kuuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa na polisi wiki iliyopita jijini Arusha.Kumwagwa kwa damu hizo za wananchi wasio na hatia, kumetokana na dharau na kiburi kisichokuwa na sababu za msingi kilichofanywa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Arusha, kuendesha uchaguzi wa meya wa jiji hilo kihuni.

Mkurugenzi huyo, aliendesha uchaguzi kwa kile ambacho hajakisema lakini kinachoonyesha kwamba alipanga kukipa Chama Cha Mapinduzi (CCM), meya wa jiji hilo kwa kuendesha uchaguzi kinyemela baada ya kujua kuwa madiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hawapo ukumbini.

Hili liliwalazimisha madiwani kutoka chama hicho kilichoshinda kiti cha ubunge wa Arusha Mjini, kuja juu na kuhoji uamuzi wake na uhalali wa kikao hicho cha uchaguzi wa meya, aliousimamia.

Matokeo yake yalikuwa ni kudhalilishwa na kuvunjiwa heshima kwa madiwani hao wa CHADEMA pamoja na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema, aliyepigwa na polisi hadi kupoteza fahamu bila sababu za msingi.

Mbali ya kipigo hicho na udhalilishwaji wote uliofanywa na polisi, bado mkurugenzi huyo hakuona ulazima wa kukaa na madiwani wa CHADEMA na kuzungumza nao ili kuondoa msigano uliokuwepo na ikibidi uchaguzi urudiwe.

Badala yake aliweka msimamo akijibu kwa nyodo na jeuri kwamba uchaguzi umeshafanyika, anayepinga na apinge lakini yeye hawezi akapoteza muda kuitisha uchaguzi mwingine.

Kauli hizo za kiburi na dharau ziliwasukuma madiwani na wabunge wao kuamua kulifikisha suala hilo kwa uongozi wa juu wa chama ili kupata namna nzuri ya kulipatia ufumbuzi.

Ni hapo ulipoandaliwa mkutano wa hadhara, ambao ungetanguliwa na maandamano ya amani ya kulaani uamuzi wa mkurugenzi huyo wa kuitisha na kusimamia uchaguzi kihuni.

Ni bahati mbaya kwamba Inspekta wa Polisi nchini (IGP) Said Mwema, amesahau wajibu wake, utu umemtoka kwa sababu ya ama kutaka kuwalinda ama kuwatetea waliompa ulaji huo, ama kwa sababu za maslahi fulani akawaamru vijana wake wapige watu.

Kweli vijana wakatii agizo lake wakapiga, wakajeruhi na mwisho wakaua.

Sipati picha jinsi Mwema alivyojisikia baada ya mauaji hayo kwani hakuwa tayari kuomba msamaha, bali alipaza sauti na kusema mauaji na upigwaji huo ulikuwa halali kwa sababu watu hao walikiuka agizo halali la polisi la kutofanya maandamano hayo.

Ninaamini atatufanyia kiburi na mzaha hapa duniani, kwa sababu wanasheria wetu hawatampandisha kizimbani na hata ikitokea umma ukashinikiza hivyo, bado hakuna jaji atakayemtia hatiani kwa sababu iliyo wazi.

Lakini Mwema afahamu kuwa roho za watu hao watatu atakwenda kuzilipa haki zao kwa yule hakika asiyeonea, anayehukumu kwa haki, asiyekula rushwa ili kuchakachua matokeo, atambe na kusema kila neno atakalo kwa sasa lakini naamini siku hiyo atajuta na kusaga meno na atayakumbuka haya nimwambiayo leo.

Hao anaowafurahisha leo kwa kuua watamruka na kumkana, atabaki kusutana na roho za watu hawa aliowaua bila hatia kwa kisingizio cha kutekeleza habari zake alizoletewa na wanaintelijensia.

Chonde Mwema, huna cha kujitetea, kwa hili hutasema chochote jamii ikusamehe, cha msingi jiuzulu, uwasake ndugu wa wote waliouawa uwaombe msamaha, huku ukikesha kumuomba msamaha Mola wako.

Kwa kuwa chanzo cha yote haya ni ushabiki wa kisiasa, uliofanywa na Mkurugenzi huyu wa Jiji la Arusha, ninamuuliza anasubiri nini kujiuzulu hadi leo? Kwa nini asijiuzulu.

Siku zote tunasema chanzo cha mauaji ya haliki ni uonevu na dhuluma za aina hii, inafikia mahali mamia kwa maelfu ya watu wanaamua kujitoa mhanga kwa kuutoa uhai wao kwa kupigania haki.

Ninajiuliza, kwa nini Mwenyezi Mungu hakumsogeza jamaa yeyote wa Mwema au mmoja wa viongozi wetu wa juu ndugu au jamaa yake asiwe mmoja wa watu ambao risasi zingevisambaratisha vichwa ama vifua vyao ili tulie sote?

CCM, Mwema na polisi wenzake, wanasahau kuwa siku moja nao watakuwa wapinzani, je, hoja zao zizimwe kwa mabavu kama vinavyofanya vyombo vyao vya dola leo?

Kuna mambo ambayo yanapotokea lazima tukubali kukiri makosa bila kusubiri kukosolewa au kunyooshewa kidole na yeyote kwa namna na jinsi yoyote.

Mauaji ya watu wasio na hatia yataendelea kubaki kama moja ya doa baya katika historia ya utawala wa Kikwete.

Kutochukua hatua za kuwawajibisha wawili hawa na wengine wote waliohusika kwa mauaji hayo kwa namna moja ama nyingine ni sawa na kulichimbia bomu ardhini, ambalo hata likikaa karne moja, kuna siku litalipuka na haitaangalia litamlipukia nani.

Jambo jingine lililo la msingi hapa ni kwa serikali kuamuru uchaguzi wa meya na naibu wake ufanyike upya, ushirikishe madiwani wote wenye sifa za kushiriki na kusiwe na hila za aina yoyote kwa nia ya kuchakachua matokeo.

Aachwe mshindi apatikane kwa kura halali, kwa kuwa madiwani wana utashi na uamuzi wao na ikumbukwe kuwa yeyote atakayechaguliwa, atafanya kazi kwa nia ya kuleta maendeleo kwa wananchi wa Arusha na si chama cha siasa anachokiwakilisha.


Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu namba 0784 au 0713- 765757, barua pepe:wiruhinda@yahoo.com
juu

No comments: