Wednesday, January 12, 2011

Malipo ya Dowans, usiri wa nini?

Mwinjilisti Kamara Kusupa




NIANZE na kukiri kwamba nimeandika mengi kuhusiana na suala la Richmond na Dowans, hata hivyo wakati naandika hayo sikuwa nimepata ukweli wa upande mwingine.

Hii ni kwasababu sikuwahi kuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na yeyote kati ya Dk. Mwakyembe, Spika Sitta, na Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Zuberi Kabwe, watu waliosema sana juu ya Dowans na Richmond.

Niliandika kutokana na hoja zao kama walivyonukuliwa na vyombo vya habari, na pia kwa kuisoma ripoti ya Dk. Mwakyembe kwenye kumbukumbu ya Bunge la 2005-2010 (Hansard).

Lakini mara baada ya kupata ukweli kutoka upande mwingine nimeanza kuona mantiki ya madai ya Spika wa zamani mheshimiwa Samwel Sitta kwamba Dowans na Richmond ni dili ya genge la watu walioamua kuchota fedha za walalahoi wa nchi hii.

Kusema kweli imani yangu kwa serikali imepungua, na kupitia safu hii napenda kuifikishia serikali yetu iliyoko madarakani ujumbe huu kwamba iachane kabisa na usiri kwenye suala hili la malipo kwa Kampuni ya Dowans.

Inabidi serikali iweke wazi kila kitu ili isitokee hali ya Watanzania wengi kukosa imani nayo, kwani kwa kadiri wananchi watakayokosa imani ndiyo serikali itakavyozidi kujipunguzia uhalali wa kutawala.

Suala la kupanda kwa gharama za umeme linawatia uchungu sana wananchi, na walio wengi wanalinasibisha na malipo kwa kampuni ya Dowans baada ya kushinda kesi ambapo sisi tumeamriwa kuwalipa mabilioni.

Mazingira yaliyopelekea Tanzania kushindwa katika shauri hilo, ama hali iliyoifikisha kampuni hiyo kwenye ushindi inatatanisha.

Maelezo ya Mheshimiwa Waziri William Ngeleja kwenye taarifa yake ya Januari 6, mwaka 2011 kwa vyombo vya habari kuhusiana na tozo/uamuzi wa mahakama ya kimataifa ya usuluhisho, yameongeza utatanishi unaofanya wananchi makini wazidi kuishuku nia ya serikali.

Kwanza, bado haijajulikana bayana hukumu ya mahakama hiyo ya kimataifa ilifanyika katika nchi gani ya dunia yetu, kwani wengine wanasema ilifanyika Paris nchini Ufaransa na wengine wanasema kikao cha Mahakama kilikuwa pale Kilimanjaro Hotel Kempsink. Je, ukweli ni upi?

Tafadhali serikali iliweke wazi neno hili na ikiwezekana mwenendo mzima wa kesi au “proceedings” zitolewe kwenye vyombo vya kuamriwa kulipwa kwa hayo mabilioni.

Kama kweli kesi ilifanyika kwa uficho wakati inaeleweka kwamba kesi hii inagusa maslahi ya jamii? Ni kwanini mashahidi muhimu kama akina Mwakyembe hawakuitwa?

Pili, uhalali wa kampuni hizi Richmond, Dowans ya Costa Rica na Dowans (T) Limited ya Tanzania uthibitishwe na kuwekwa wazi na msemaji mmoja wa serikali yetu ikiwezekana tamko litoke aidha kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ama kwa mwenyewe Rais Jakaya Kikwete.

Sababu ya kusema hivi ni moja kwamba sasa kauli za mawaziri wake haziaminiki. Ninaposema haziaminiki sikusudii kuwavunjia heshima yao mawaziri wetu kwa kuchora picha ya kwamba siyo waaminifu la hasha!

Bado nawachukulia wamezidi mno kutofautiana, karibu kila aliyejitokeza kusema, ametoa kauli yake tofauti na kauli za wenzake na hilo linatufanya sisi wananchi tuone kwamba wote wametoa hisia zao binafsi hakuna kauli inayotokana na kikao cha Baraza la Mawaziri.

Kwa mfano kulingana na Mheshimiwa Mwakyembe Kampuni za Richmond na Dowans ni kampuni hewa kwa maneno mengine ni kampuni za kitapeli.

Mwakyembe hajasema hivyo akiwa kama Naibu Waziri wa Miundombinu lakini taarifa yake bungeni akiwa kama Mwenyekiti wa kamati teule ya Bunge kwa ajili ya kuichunguza Richmond, ndivyo inavyosomeka.

Siamini kama kuna tofauti kati ya Mwakyembe Waziri, na Mwakyembe mwenyekiti wa kamati ya uchunguzi ya Bunge, na hata kama kuna tofauti bado ukweli unabaki pale pale haubadiliki wala hautofautiani kwa sababu tu ya nyakati tofauti.

Wananchi tunataka kujua kama kweli hizi ni kampuni “genuine” ama kampuni hewa.

Kama itakuwa kweli ni kampuni hewa, kuna swali zito kwamba hiyo Mahakama ya Kimataifa ingewezaje kusikiliza hoja kutoka kwa kampuni ambayo kisheria haipo?

Hivi ni kweli Mahakama ya Kimataifa iliyo makini inaweza kuamuru mamilioni ya fedha yalipwe kwa kampuni hewa na isiyotambulika kisheria kwamba iko?

Hapa kuna maswali mengi yanayoongeza mashaka dhidi ya serikali yetu kwamba hata hao hao wanaowasajili na kuwapokea wawekezaji katika nchi yetu hawako makini.

Mashaka yatakapoongezeka dhidi ya serikali, mwisho wake ni serikali kutoaminika na hao inaowatawala, na hatimaye kutoheshimika.

Ndiyo maana nasema inabidi sasa serikali iamke na kuondoa usiri wote uliogubika sakata la Dowans.

Kuna kauli ya Mheshimiwa Samweli Sitta Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, amekuwa na ujasiri wa kusema yale yale aliyokuwa akisimamia hapo alipokuwa Spika wa Bunge, kwa hili namwona Sitta kama mtu aliyebeba dhamira ya kweli ya kupambana na ufisadi.

Sitta amenukuliwa kusema kwamba Dowans ni genge la watu watatu, na kwamba mabilioni ambayo yameamriwa kulipwa kwa Dowans ni mpango wa genge hilo kujikusanyika fedha kwaajili ya kampeni za urais 2015.

Pamoja na kwamba hii ni kauli binafsi za urais tamko la serikali, bado wananchi tumeichukulia kwa umakini kwasababu Samuel Sitta siyo mtu wa kijiweni, ni Spika wa zamani Bunge la Muungano, na sasa ni memba wa Baraza la mawaziri, kauli yake haiwezi kupuuzwa na watanzania makini nahasa hapo inapojitokeza hali ya serikali yetu kuonekana inakubali kushindwa kirahisi.

Serikali yetu inaonesha kuridhia na kuharakisha malipo ya dola za Marekani 65, 812, 630.00 ili deni hilo lisizae riba kubwa.

Hapa ndipo shina la uchungu linapochipuka moyoni mwa mlalahoi iweje TANESCO inayowakamua maskini bila huruma izitose milioni zote hizo kiulani kwa kampuni inayoshukiwa kwamba ni ya kitapeli?

Ilipata mashaka juu ya utapeli wa Richmond LLC yafutwe kwanza ndipo tuje kwenye mjadala wa kwanini TANESCO (Tanzania) ilishindwa kirahisi kwenye kesi hii.

Mara ya kwanza nilipoandika kuwalaumu Mwakyembe, na Sitta kwa kuupotosha umma na pia kulishawishi Bunge kufanya maamuzi potofu nilikuwa na uelewa wa kwamba Richmond Development Company LLC (RDEVCO) ni kampuni halali na inayotambuliwa kisheria kwamba iko, kwani kwa uelewa wangu serikali makini isingeweza kuingia kwenye majadiliano na kampuni ambayo haiku (haina legal entity).

Niliamini pia wataalamu wa TANESCO wasingeweza kuingizwa mkenge na kuzidiwa ujanja na matapeli kwasababu wataalamu wetu wana elimu na uzoefu.

Pia niliamini kwamba kwa jinsi ninavyouelewa urasimu wa kibenki kuanzia Benki za hapa nchini hadi benki za kimataifa, siyo rahisi benki iifungulie akaunti kampuni hewa na kuendesha “transactions” kadhaa huku kampuni husika ikiwa haina uhalali wowote wa kisheria.

Mwisho niliamini kwamba haingekuwa rahisi kwa kampuni ya Dowans kurithishana mkataba na kazi na kampuni hewa iitwayo Richmond, na kwa maana hiyo serikali yetu baada ya kubaini dosari za Richmond iliyoleta mtikisiko hata kwa baraza letu la mawaziri isingeridhia wala kutambua kurithishana mikataba baina ya Dowans na Richmond kwani ingekuwa ni ubatili kwa Dowans kurithi mkataba na kampuni ya Richmond ambayo serikali yote imejua kwamba ni kampuni hewa.

Kutokana na uelewa wa jinsi hiyo ndiyo maana nikawa nawaona Dk. Mwakyembe na Spika Sitta kama watu wanaoendesha siasa nyepesi.

Lakini mara baada ya hukumu kutolewa, inayoonyesha kwamba Tanzania imeshindwa kesi, na mwanasheria mkuu wa serikali kuishauri TANESCO iyakubali matokeo, hapo ndipo nilipozinduka kuona kumbe huko serikalini tuna watu ambao hawaisadii nchi.

Hii itakuwa mara ya tatu Tanzania kujeruhiwa sawa na mwanakondoo anavyoweza kularuliwa na kutafunwa na mbwamwitu akiwa hai.

Mara ya kwanza ni kwenye ununuzi wa ndege ya Rais tukasikia serikali yetu ilimtumia wakala (Mhindi) badala ya serikali yenyewe kuwasiliana moja kwa moja na wauzaji.

Wakala huyo huyo akatumika pia kwenye ununuzi wa magari ya jeshi letu, mbaya zaidi ikatokea kwamba ndege hiyo iliyonunuliwa kwa bei mbaya ni mbovu na sasa haitumiki.

Mara ya pili ikawa kwenye ununuzi wa rada, pia serikali yetu ikamtumia wakala badala ya kuwasiliana moja kwa moja na wauzaji, mbaya zaidi ni kwamba bei ya rada hiyo ikawa juu kuliko thamani yake halisi.

Ajabu ni kwamba ni Waingereza ambao walionyesha kukerwa na rushwa hiyo kuliko sisi Tanzania walipaji wa fedha hizo.

Mpaka hapo kwanini mwananchi wa kawaida asiamini kwamba serikali yetu imeridhia rushwa kubwa na inaonea walaji rushwa wadogo?

Rais wetu Jakaya Mrisho Kikwete hata baada ya kujua pasipo shaka kwamba kuna watu walionufaishwa kutokana na ununuzi wa rada, hakuonyesha ukali wowote walau kuagiza wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.

Hali hiyo imesababisha wananchi tujiulize hivi ni kweli wapelelezi wa Uingereza wa kitendo cha SFO ni waongo au viongozi wetu wa kitaifa ndio wasiokuwa na uchungu na kodi zetu?

Na kama hawana uchungu inakuwaje wakose uchungu kwa rushwa kubwa na wawe na uchungu kwa rushwa ndogo?

Hapa ndipo yanapoibuka mashaka kwamba viongozi wetu wa serikali kuu wanahusika na rushwa kubwa na kama hawahusiki kwa njia moja au nyingine, basi walau wananufaika kutokana na rushwa hizo.

Hadi hapo tunafikia kwenye nukta ya kwamba serikali imefanywa kuwa mtuhumiwa na wananchi inaowatawala hivi kweli itaendelea kuwatawala wakati inatuhumiwa?

Ndiyo maana nasema umefika wakati kwa serikali kujisafisha na kujiweka mbali na tuhuma ili kudumisha uhalali wake wa kutawala kwani tuhuma za mara kwa mara zinaipunguzia serikali yetu uhalali wa kutawala.

Namna ya kujisafisha ni rahisi sana ianze na kuondoa usiri kwenye sakata hili la Dowans iweke wazi kila neno hata pale ilipoteleza ama ilipopungukiwa umaskini.

Wananchi wakiwa hata pale ilipokosea wataisamehe na kuendelea kuiheshimu.

Serikali iwatoe wote waliohusika na kuichafua iwaambie wazi wazi kwamba kila mmoja aubebe msalaba wake mwenyewe.

Rais Kikwete ajiweke mbali na kila anayetuhumiwa kukosa uadilifu vinginevyo kama ataendelea na utamaduni wake wa kutaka kuwa rafiki wa wote kwa wakati wote basi ajue kwamba kila mmoja kati ya hao walio karibu naye atakaponuka harufu ya rushwa, atamwambukiza na yeye ataanza kutoa harufu.

Asije kushangaa kujikuta akizomewa na wananchi kwenye ziara zake za kukagua maendeleo. Wengine wana hasira ya kupandishwa umeme na TANESCO, majibu ya mheshimiwa Ngeleja hayatoshi.


Mwandishi anapatikana kwa simu namba 0715 311422/ 0767 3111422/0786 311422. Au barua pepe kusupa@yahoo.com

No comments: