Wednesday, January 12, 2011

Mauaji ya kisiasa Arusha: Intelijensia, Usalama wa CCM umehusika

Bakari M. Mohamed




TANGU kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, 3010 Arusha limekuwa jiji lenye harakati na vuguvugu kisiasa. Uchaguzi Mkuu uliopita umeifanya CCM kupoporomoka kisiasa na CHADEMA kuchukua uongozi wa kisiasa.

Kwa jinsi hiyo, kumekuwapo mbinu za kimkakati zinazofanywa na taasisi za ulinzi na usalama (hususan Intelijensia na Usalama wa CCM) katika kuweka hali-tete na au hali-joto ndani ya viunga vya kisiasa vya Jiji la Arusha.

Baada ya CHADEMA kulitwaa Jiji la Arusha kwemye kinyang’anyiro cha kiti cha ubunge kwa kumuangusha mwanasiasa aliyeandaliwa na kuenziwa na vigogo wa saisa za CCM akiwemo aliyekuwa Waziri Mkuu (aliyelazimishwa kujiuzulu) Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa kumekuwapo kwa hali iliyokuwa inaashiria kwamba hila na mizengwe ya kisiasa itatawala jiji hilo ili kuifanya serikali ya jiji (Halmashauri ya Jiji la Arusha) imezwe na CCM.

Pamoja na hali hiyo, tayari mizania ya uwiano wa kisiasa jijini humo ilishaipa CHADEMA umiliki wa siasa za jiji hilo lenye upinzani mkali unaohanikizwa na maeneo jirani ya Hai (kwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Aikaeli Mbowe) na Moshi Mjini (kwa Philemon Ndesamburo). Ukweli utabaki kuwa Arusha imeanza kuchemka kisiasa na inachukua mkondo wenye vuguvugu halisi la mabadiliko.

Kutokana na harakati za maisha ya kila siku ya kisiasa, kiuchumi, na kijamii ni rahisi sana kwa jiji hilo kuwa na taarifa nyingi zinazoibuka kila kukicha kutoka sehemu mbalimbali zinazozunguka jiji hilo.

Taarifa nyingi (ghafi) hupatikana kwenye sehemu mbalimbali muhimu zikiwemo sehemu za biashara (maduka, migahawa, hoteli, masoko, vilinge, na vijiwe vya kahawa), kwenye ofisi za umma na za mashirika mbalimbali ya ndani na ya kimataifa. Hali hii hulifanya Jiji la Arusha lichemke kama bahari!

Taarifa za kiuchunguzi zinaonyesha kwamba Arusha kwa sasa ina nguvu kubwa ya upinzani na inaweza kuwa ndiyo “ngome” ya upinzani kwa Ukanda wa Kaskazini.

Sababu kubwa ni kule kuangushwa kwa Dakta Batilda Burian aliyewahi kuwa Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais – (Mazingira).

Wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 31 Oktoba, 2010 Mheshimiwa (Dakta) Batilda Burian alipewa aina zote za msaada kutoka kwa vigogo wa siasa za CCM akiwamo Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete. Hata hivyo, aliangushwa na Mheshimiwa Godbless Lema wa CHADEMA.

Kuchukuliwa kwa kiti cha ubunge Arusha Mjini kulifanyika sanjari na CCM kupoteza sehemu muhimu ya uwakilishi kwenye Baraza la Jiji la Arusha, hali iliyoifanya CCM kutafuta hila na mizengwe ya kubakisha nguvu zake kwenye umiliki wa halmashauri (Baraza la Jiji). Songombingo na sintofahamu zilianzia kwenye uchaguzi wa Mstahiki Meya wa jiji ambapo hila zilitumika na hatimaye CCM kukitwaa kiti cha umeya kwa mizengwe.

Hali ya songombingo na au sintofahamu ya vuta-n-kuvute baina ya CCM na CHADEMA ikiambatana na vurugu la kimyakimya na au za chinichini ilianza kufukuta na kuweka fukuto la kisiasa kwa takriban muda wote wa matokeo ya uchaguzi wa kiti cha umeya.

Kwa kuwa CCM walipora kiti cha umeya; na kwa jinsi chama hicho (tawala) chenye nguvu za dola (Polisi, Usalama wa Taifa, JWTZ, Magereza, Askari wa Siri, na kadhalika) kilivyojipanga kuendesha siasa za kibabe; Jiji la Arusha lilishawekwa kwenye hali-joto (kwa alama nyekundu) ya kiusalama.

Pamoja na hali hiyo, bado CHADEMA walikuwa na wana kila sababu ya kudhani kwamba haki yao imeporwa na walikuwa na wapo tayari kutumia “nguvu ya umma” kuuonyesha umma wa Jiji la Arusha juu ya uporwaji wa nafasi ya Mstahiki Meya uliofanywa na CCM kwa njia ya maandamano ya amani na hatimaye kufanyika kwa mkutano wa hadhara.

Mwanzo na kutokana na hali-joto na hali-tete iliyokuwapo hapo kabla, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha hakuona busara kuruhusu maandamano na hatimaye mkutano wa hadhara ambao ungeamsha hisia za kudhulumiwa na hali hiyo ingeweza kuleta uvunjifu wa amani.

Kwa utumizi wa busara na hekima viongozi wa CHADEMA walikubaliana na maoni na au mawazo (yenye hekima na busara) ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Afande Thobias Andengenye na kusitisha maandamano na mkutano wa hadhara ambao ungefanyika kwenye eneo lililokusudiwa.

Baada ya joto na au gafugafu la kisiasa kupoa, CHADEMA waliiandikia Polisi Arusha kuomba kufanyika kwa maandamano na hatimaye mkutano wa hadhara, ombi ambalo kimsingi lilikubaliwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha.

Maandalizi ya maandamano na mkutano yalianza kufanyika na hatimaye viongozi wa kada na ngazi mbalimbali wa CHADEMA kuwasili Jiji la Arusha kwa shughuli ya kisiasa ya tarehe 05 Januari, 2011.

Kinyume na matarajio ya CHADEMA, siku moja kabla (na si zaidi ya saa 36) Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) Afande Said Mwema, akatangaza kupitia vyombo vya habari kwamba maandamano yaliyopangwa kufanywa na CHADEMA Arusha yamefutwa, isipokuwa wanaruhusiwa kufanya “mkutano wa hadhara.”

Taarifa ya zuio la kufanyika maandamano lilikuja baada ya kile kilichotajwa kuwa ni “taarifa za ki-intelijensia na ki-usalama.”

Ni ukweli usiyopingika kwamba Afande (IGP) Said Mwema ni mtaalamu wa masuala ya ulinzi na usalama na zaidi anaijua vema intelijensia ya usalama. Sidhani kama amezingatia weledi kwenye “amri” ya kuzuia maandamano ilhali ruhusa ilishatolewa na Kamanda wa Polisi, Afande Thobias Andengenye, ambaye kwa maarifa na ustadi (na hata maadili) ya kazi ya usalama wa raia ndiye anayejua hali halisi ya usalama wa Jiji la Arusha na siyo Afande (IGP) Said Mwema ambaye si mkaazi wa Arusha!

Taarifa za ki-intelijensia na ki-usalama nadhani kwanza zilianza kupatikana Arusha kwa: kukusanywa; kupembuliwa; kuchakatwa; kusanifiwa; na hatimaye kutolewa maamuzi kwamba maandamano na mkutano wa hadhara kwa CHADEMA ruhusa kufanyika! Sasa suala la kujiuliza hapa linaweza kuwa: Ni taarifa zipi za ki-intelijensia na ki-usalama zilizosababisha zuio la maandamano ya CHADEMA?

Hakuna shaka wala wasiwasi kwamba, vyombo vya ulinzi na usalama (pamoja na Askari wa Siri na Usalama wa Taifa – TISS) vinafanya kazi kwa falsafa ya amri baada ya amri (chain of command) na amri ya kijeshi mara zote hutoka juu kwenda chini na haipingwi.

Hapa pana jambo la kujifunza juu ya nani anayetoa “amri” na nani anayepokea!

Rais wa CCM ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya Ulinzi na Usalama – yeye (Rais) ndiye mwenye amri ya mwisho juu ya utendajikazi wa majeshi yote.

Na ndiyo maana hata ilipotolewa amri ya Afande (IGP) Said Mwema juu ya zuio la maandamano pamoja na ukweli kwamba Polisi Arusha walishayaruhusu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha hakuweza kupinga amri ya mkuu (boss) wake. Na suala la pili hapa linaweza kuwa: Ni wapi Afande (IGP) Saidi Mwema amepata amri ya kuruhusu matumizi ya nguvu kupita kiasi na hatimaye kufanyika mauaji ya raia wasio na ulinzi?

Ili kuielewa vema nukta hii ni vema tukirejea historia ya harakati za maandamano Tanzania. Haijalishi maandamano hayo ni ya nini na yaliongozwa na nani.

Kwanza, mifano ya karibuni ni mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi Tanzania katika Jiji la Dar es Salaam eneo la Msikiti wa Mwembechai ambapo watu watatu waliuawa na wengine kutiwa vilema vya maisha (akiwemo aliyekuwa kijana wa shule ya msingi wakati ule Chuki Athumani).

Kadhia ya Mwembechai ilikuwa kubwa na ilichukua sura ya udini na kidini zaidi kuliko kisiasa. Hata hivyo, tutosheke kwamba Polisi wa Tanzania waliwaua Watanzania wenzao kwa risasi za moto (tena kwa amri ya “piga yule” iliyotolewa na Kamanda wa Polisi).

Achilia mbali mauaji haya na yale ya kuuwawa kwa watu wasio na hatia waliosingiziwa ujambazi; tunawajibika kukubali kwamba Polisi wa Tanzania wamekuwa wakiwaua wananchi wenzao katika mazingira ya kutatanisha!

Mauaji yaliyotisha sana ni yale yaliyofanywa kisiwani Pemba baada ya maandamano ya chama cha wananchi (CUF) kuzimwa kwa nguvu za kijeshi. Mwaka 2000 CUF iliingia kwenye Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar baada ya Muafaka wa Kwanza wa 1998.

Hata hivyo, kinyume na matarajio ya CUF, CCM walifanya “mchezo mchafu” na rafu za kisiasa hali iliyoifanya CUF kuyakataa matokeo ya uchaguzi na vilevile kutomtambua Rais Amani Abeid Karume.

Januuari 26 na 27 2001 na siku zilizofuata baada ya hapo zilikuwa za kutisha pale makumi ya watu walipouwawa na polisi na vikosi vingine vya SMZ.

Inakadiriwa mauaji yale yaligharimu maisha ya watu zaidi ya thelathini na tatu (33). Pamoja na kusababisha umwagikaji wa damu na vifo vya wananchi wasio na ulinzi, machafuko yale yalishuhudia unajisi wa wanawake (kwa kubakwa) kulikofanywa na askari waliotumwa kuua, kubaka na kunajisi!

Mauaji ya Januari, 2001 yaliushtua ulimwengu na kulaaniwa na mashirika mbalimbali ya utetezi wa haki za binadamu yakiwamo Amnesty International na ACAS (Association of Concerned Africa Scholars).

Hali-joto ya kisaisa iliyotanda katika visiwa vya Unguja na Pemba ilipelekea kwa mara ya kwanza Tanzania kuzalisha wakimbizi waliokimbilia Shimoni, Mombasa (Kenya).

Mwenendo huu wa kuendesha mauaji ya watu wasiokuwa na ulinzi kunakofanywa na Jeshi la Polisi la Tanzania pamoja na taasisi nyeti za ulinzi na usalama wa nchi umekuwa ukichukua sura na mazingira tofauti kwa utashi wa kisiasa.

Taasisi za ulinzi na usalama badala ya kuaminiwa na raia kwamba ndio tegemeo la ulinzi wa hali na mali zao zimekuwa adui wa wananchi. Wakati wa harakati za kisiasa majeshi ya ulinzi na usalama yamekuwa yakiegemea upande wa CCM na kusahau dhima na wajibu wao katika kuwapatia ulinzi raia na mali zao bila kujali itikadi za kisiasa.

Viongozi wa majeshi ya ulinzi na usalama wamekuwa wakionekana kutoa usaidizi wa moja kwa moja kwa CCM ilhali wajibu wao kikatiba ni kutokufungamana na chama chochote cha siasa.

Ikumbukwe hapa kwamba mwaka 2005 aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Omar Idd Mahita, aliwahi kutoa kauli tata juu ya CUF kwamba ni “chama cha kigaidi na kimeingiza majambia nchini ili kuleta machafuko na umwagikaji wa damu”.

Vilevile, wananchi tusisahau kwamba mwaka 2010 wakati tukielekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, 2010 ilitolewa kauli tata na Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali Afande Abdul’Rahman Shimbo.

Imekuwa kawaida ya viongozi wa taasisi za ulinzi na usalama kujihusisha na siasa kwa kuwa ni utaratibu unaotumiwa na CCM katika kuwarasmisha viongozi wa kijeshi kwenye siasa na kuwapa nafasi na au vyeo vya kisiasa kwa mtaji wa kustaafu jeshi na kujiunga na siasa.

Kwa kuwa mauaji yaliyotokea Arusha yamekumbusha na yale yaliyosahaulika: Mauaji ya Bulyanhulu; Mauaji ya Mwembechai; Mauaji ya Mererani; Mauaji ya wafanyabiashara ya madini (waliouawa chini ya Kamanda Abdallah Zombe); na mauaji ya Pemba; ipo haja ya kudurusu na kufanya upitizi makini juu ya utendaji wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama.

Vyombo vya ulinzi na usalama vya Tanzania havina budi kupitiwa upya na kama kuna sheria za kikoloni zinazowapa “kichwa ngumu” askari na viongozi wao kufanya kama vikosi vya kikoloni (motorised companies) na kuua watu wasiye na ulinzi, lazima sheria mbovu kama hizo zibadilishwe ili kwenda na mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa.

Pamoja inafahamika kwamba CCM inazitegemea sana taasisi za ulinzi na usalama kwa masilahi ya kibinafsi (kwa baadhi ya vigogo wa chama) na kwa manufaa ya kundi la mafisadi wa siasa wanaoyatumia majeshi kwa faida zao, lazima juhudi za makusudi zichukuliwe ili kurekebisha hali hiyo kabla hayajatokea maafa makubwa yatakayochafua sura ya nchi inayoimbwa ya “utulivu na amani”.

Watu wachache wasitumie nafasi walizopewa na umma ndani ya majeshi kwa mafungamano yao ya kisiasa na au kirafiki na viongozi mafisadi wanaotaka kutawala kwa njia ya mabavu na utumizi wa nguvu za kipolisi na au kijeshi.

Mauwaji ya Arusha yawe kielezeo cha uhuru, haki, usawa, na uadilifu na yasichukuliwe kama yaliyotokea kisiwani Pemba kwa kuwa kama wananchi wataendelea kukosa imani na vyombo vyao vya ulinzi na usalama kuna hatari ya kumomonyoa uhuru na umoja kati ya wananchi na majeshi yao.

Kama kweli tunataka kujenga Tanzania yenye amani na utulivu wa kudumu basi tuna wajibu wa kuhakikisha kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vinatoa ulinzi kamili (na unaostahili) kwa raia na mali zao bila ubaguzi wala kuegemea upande wowote.

Na umefika wakati kwa CCM kuacha kuwatumia makada wa kijeshi katika kufanikisha mipango ya kutawala kwa nguvu ya amri baada ya amri. Hata kama CCM ni chama cha kijeshi isiwe sababu ya kupoteza mujtamaa wa demokrasia kwa wendawazimu wa udikteta. CCM iache demokrasia ishike mkondo wake; na ikumbukwe, “mauaji yakizoeleka, damu ya wahanga itaiathiri nchi na umwagikaji wake utaongezeka.”

No comments: