Sunday, January 9, 2011

Tunamtenganisha vipi Kikwete na Dowans?

Salehe Mohamed




UKWELI kwa kawaida huuma, na tulio wengi hatupendi kuambiwa ukweli hasa kwenye maeneo ambayo hatujafanya vizuri.

Lakini ili tuendelee ni lazima tujenge utaratibu wa kuambiana ukweli na kukosoana kila tunapokwenda tofauti na inavyotakikana.

Kwa muda mrefu hivi sasa kumekuwa na mjadala wa malipo yanayopaswa kufanywa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) dhidi ya Kampuni Dowans ambayo ilikuwa ikizalisha na kuuza umeme wake kwa TANESCO.

Dowans waliamua kuwaburuza TANESCO katika mahakama ya kimataifa ya usuluhishi wa migogoro ya kibiashara ambako mwisho wa shauri iliamuliwa Dowans walipwe sh bilioni 185 (ingawa serikali imesema wanapaswa kulipa sh bilioni 94).

Sina haja ya kuanza kujikita kwenye uhalali wa malipo hayo lakini ninalotaka kulihoji hapa ni jitihada za viongozi kadhaa wa serikali, chama tawala na ikulu kupinga Rais Kikwete kuhusishwa na sakata hilo.

Binafsi sikubaliani nao hata kidogo kuwa Rais Kikwete hahusiki na sakata hilo, yapo mambo mengi ambayo yananifanya niwastaajabu wale wote wanaopinga kiongozi mkuu wa nchi kuhusishwa katika sakata hilo.

Uingiaji wa Kampuni ya Richmond ambayo baadaye ilizaa Dowans ulifanywa na Baraza la Mawaziri ambalo Mwenyekiti wake ni Rais Kikwete, hapa tunawezaje kusema Kikwete hauhusiki na Dowans?

Mbali na Rais kushiriki katika uamuzi huo lakini pia alikuwa akipelekewa barua kuhusu mwenendo wa kampuni hiyo na aliyekuwa Waziri Mkuu wa wakati huo, Edward Lowassa, je, alichukua hatua gani?

Hata baadhi ya magazeti hapa nchini yaliweza kuchapisha nakala za barua hizo zilizokuwa zikitoka kwa Lowassa kwenda kwa rais na kwa watendaji wengine.

Kibaya zaidi ni kwamba Rais Kikwete alishauhakikishia umma kuwa mgawo wa umeme utakuwa historia kwa kuwa serikali imeshapata Kampuni ya Richmond lakini matokeo yake kila mmoja ni mashahidi wa utimizwaji wa hiyo ahadi.

Kama Rais Kikwete aliweza kuutangazia umma uhakika wa umeme wa Richmond ambayo baadaye ilikuja kubainika ni ‘hewa’, kwa nini tusiamini alihusika kwa namna moja au nyingine?

Rais anatakiwa kuwa makini sana kwa kila kauli yake, taarifa anazopelekewa na wataalamu wake au kinachofanywa na walio chini yake, sasa kama anaweza kuitambulisha kampuni hewa kwa wananchi kwa nini asihusishwe na madhambi ya kampuni hiyo?

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Salva Rweymamu, kabla ya kupata cheo hicho alikuwa ni miongoni mwa watu waliokuwa mstari wa mbele wakati wa uingiaji wa mitambo ya Richmond, leo hii awezaje kuwa mtu sahihi kuzungumzia sakata hilo?

Salva ni miongoni mwa waliohojiwa na kamati teule ya Bunge kuhusu Richmond na anavyomfahamu mkurugenzi wa kampuni hiyo na alichokisema huko sitaki kukizungumzia hii leo, yatosha kusema hana udhu wa kulizungumzia sakata la Dowans.

Binafsi naamini kuwa Rais Kikwete, anaijua vizuri Dowans na Richmond ndiyo maana aliweza kujitokeza hadharani na kuwapongeza TANESCO pale walipofuta hoja yao ya kutaka kununua mitambo ya Dowans.

Lazima tuambiane ukweli kuwa Rais wetu huwa hapendi kuzungumzia mambo magumu na yenye kumharibia taswira yake bali hupenda yafanywe na watendaji wengine ili washambuliwe wao.

Nina hakika kama Rais Kikwete angekuwa jasiri na kulitangazia taifa kuwa tunainunua mitambo ya Dowans kwa wakati ule ilikuwa ikiuzwa sh bil. 86, tusingefikia hapa tulipo ambapo tunatakiwa kulipa sh bil. 94 na mitambo si mali yetu.

Angeamua hivyo asingepata upinzani mkali kwa kuwa yeye ni rais na muamuzi wa mwisho, hata wale waliokuwa mstari wa mbele kupinga jambo hilo wangenywea kwa kuwa kiongozi wao wa chama ameshaamua.

Kama Kikwete aliweza kuamuru mitambo ya IPTL ambayo ilikuwa ikitumia zaidi ya sh bilioni 20 kwa mwezi iwashwe, watendaji wakatimiza alishindwa vipi kuamuru ununuzi wa mitambo hiyo?

Kuna watu wanaojenga hoja kuwa sheria ya manunuzi ya umma ya mwaka 2004 ambayo inazuia kununua mitambo iliyotumika ingekuwa imevunjwa na kiongozi wa nchi, sasa kipi bora kuivunja sheria hiyo ili kuwa na umeme au kuilinda na kukosa umeme huku tukitakiwa kulipa bilioni 94.

Najiuliza wapo wapi wale waliokuwa mstari wa mbele kupinga ununuzi wa mitambo hiyo, je, wanafurahia giza na hasara wanayopata wananchi kwa sababu ya kukosa umeme?

Sioni mantiki ya kutohusika kwa Rais Kikwete katika sakata la Richmond na Dowans hata kama watendaji wenye lengo la kuganga njaa (kulinda ajira) wataendelea kumtetea kuwa hahusiki.

Nitakubaliana nao kuwa Rais Kikwete, hahusika katika sakata hilo kama wataniambia alikuwa hajui na haambiwi chochote, na kama hivyo ndivyo ana sababu gani ya kuendelea na wadhifa huo?

Rais Kikwete angeweza kutumia taarifa za kiintelijensia kama anazozipata Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema kuhusu wamiliki, uwezo wa Kampuni ya Richmond na baadaye Dowans kamwe tusingeweza kufikia hapa tulipo.

Je, taarifa za kiintelijensia ni kwa lengo la kuzuia maandamano ya vyama vya siasa pekee?

No comments: