Sunday, January 9, 2011

Barua ya wazi kwa WanaCHADEMA

Padri Privatus Karugendo




NDUGU zetu Wanachadema, poleni sana kwa tukio la Arusha, la viongozi na wanachama wenu kupigwa, kuumizwa, kudhalilishwa na kuwekwa ndani wakati wakipigania haki za msingi za Mtanzania.

Tumepata habari kwamba hata mama mjamzito alipigwa na kuumizwa, watu watatu wamekufa na damu imemwagika. Haya si matukio ya kawaida; yanachukiza, yanasikitisha na yanaamsha hamasa na hasira ndani ya jamii yetu.

Kwamba meya wa Arusha, alichaguliwa kinyume cha sheria na taratibu, ni kitu kilichokuwa wazi; kwamba serikali inayoongozwa na CCM iliutambua uchaguzi wa meya wa Arusha ulioendeshwa kinyume cha sheria, liko wazi pia.

Hivyo nyinyi kusimama na kupinga kwa nguvu zote ni haki yenu ya msingi. Msingefanya hivyo tungewashangaa na kuwaita wasaliti.

Kwa vile nimeshindwa kabisa kuwapata kwenye simu kuwapa pole, naomba mpokee barua hii kama neno la pole! Mapambano yanaendelea!

Hivyo basi, tunaamini kwamba mlifanya maandamano kwa lengo la kutetea haki za msingi na si kutafuta sifa. Tunajua kabisa kwamba mlifanya hivyo si kwa vile chama chenu kilishindwa kuikamata dola.

Pia tunaamini mlifanya hivyo si kwa lengo la kuleta vurugu na kuvuruga amani ya Tanzania na kuifanya nchi yetu isitawalike.

Yamesemwa mengi kutaka kupotosha ukweli. Serikali inataka kujikosha na kuwabebesha mzigo wa yote yaliyotokea.

CCM inasukuma lawama zote kwenu. Polisi inawalaumu nyinyi na watu wengine wasiokuwa na mapenzi na taifa letu;

wanawatetea CCM na kuwalaumu nyinyi. Pamoja na yote hayo ukweli unabaki pale pale kwamba diwani wa Tanga hawezi kupiga kura ya meya wa Arusha. Kulikataa hili, mkapigwa, mkaumizwa na wengine kuuawa ni jambo lisilokubalika.

Kitendo chenu cha kufunga vitambaa vyeupe kwenye mikono yenu kama ishara ya amani ni ushahidi wa kutosha kwa dunia nzima kwamba mlikuwa na lengo la kufanya maandamano ya amani.

Watu waliostaarabika, watu wenye roho ya utu na kuheshimu haki za binadamu, wangeheshimu vitambaa vyeupe maana hii imekuwa ishara ya amani duniani kote. Hivyo msikubali lawama yoyote juu ya watu waliouawa na polisi ya serikali inayoongozwa na CCM.

Hamkufanya kosa lolote, nyinyi mlifanya maandamano, kitu ambacho ni haki yetu kikatiba na kazi ya polisi ni kuangalia usalama wa raia. Mzigo na lawama za vifo vya vijana wa Arusha, uiangukie serikali kwa kubali kuchakachua uchaguzi wa Meya wa Arusha.

Lowassa, alisikika akisema Arusha isifanywe Ivory Coast. Sasa ajue wazi kwamba chama chake (CCM), kina mpango wa kuifanya Arusha kuwa uwanja wa mapambano na bila hekima ya kutosha, mapambano haya yataenea nchi nzima.

Watu wanataka mabadiliko na mwenye nguvu wa kuyazuia mabadiliko haya ni Mungu peke yake. Hakuna nguvu nyingi inayoweza kufanya kazi hiyo hata kama ni risasi na mizinga!

Naandika barua hii ya wazi kuwapa moyo. Ninajua kabisa kwamba nyinyi ni binadamu na vitisho hivi mnaweza kukata tamaa. Msife moyo maana Watanzania wengi tuko nyuma yenu; polisi waandae risasi za kutosha.

Nina imani hawana risasi milioni 40! Pia nina imani hawana polisi milioni 40. Wananchi ni wengi; wananchi wamechukia, hivyo hakuna kurudi nyuma. Niwakumbushe historia kidogo; kwamba hakuna mtu yeyote duniani aliyejaribu kupambana na wananchi akawashinda.

Maandamano ya kupinga kupanda kwa bei ya umeme yabaki palepale. Hili nalo ni dai lenu la msingi; umeme unagusa maisha ya Mtanzania, unagusa uchumi.

Kupandisha bei ya umeme kwa lengo la kutaka kulipa deni la Dowans ni kitu kisichokubalika kwa wengi. Hivyo ni bora wachache wafe wakitetea haki ya wengi; kawaida ni kwamba akifa mtu mwingine anazaliwa. Tufe sisi tukitetea haki, ili watakaozaliwa waishi kwenye amani na utulivu.

Maandamano ya kudai Katiba mpya nayo yabaki pale pale. Na hili nalo ni dai la msingi sana. Tunahitaji Katiba mpya na si viraka. Tunahitaji Baraza la Katiba na wala si tume. Wananchi wanaburuzwa, hivyo ni lazima wajitokeze watu wa kuwasemea.

CHADEMA, mmejitokeza kuwasemea wananchi; ni vyema kazi hii mkaiendeleza kwa nguvu zote bila kurudi nyuma. Tukikubali kuundwa kwa tume ya katiba, tutakuwa tumejiuza wenyewe, maana tume hiyo itakuwa imeteuliwa na rais na itakuwa inawajibika kwa rais.

Nina uhakika rais hawezi kuwateua watu anaofikiri watatunga Katiba ya kukididimiza chama chake.

Ninajua jinsi CHADEMA, ilivyogawanyika na hasa wakati na baada ya mchakato wa uchaguzi. Mgawanyiko huu unasukwa na kusukumwa na maadui kutoka nje ya CHADEMA.

Hekima na busara ziwaongoze kutambua mbinu hizo chafu na kujitahidi kuijenga CHADEMA moja, yenye mshikamano wa nguvu.

Damu hii ya watu wasiokuwa na hatia iliyomwagika, iwe chachu ya kuwasaidia kumaliza tofauti ndani ya chama chenu ili kwa nguvu isiyogawanyika msimame pamoja kuwatetea Watanzania.

Naandika barua hii nikiwa Lushoto. Mji huu mdogo usomaji wa magazeti uko chini. Lakini siku ambayo matukio ya Arusha yaliandikwa magazetini, watu wengi walikimbia kuyanunua na kuyasoma.

Walichukia sana kusikia watu wamekufa; walisononeshwa na picha ya Mchumba wa Dk. Slaa, Josephine Mushumbusi, aliyepigwa na kuumizwa.

Walilaani vikali polisi kumpiga mama mjamzito. Walibeza msimamo wa CCM kumsimamisha mwanamke kugombea uspika, wakati bado haki za wanawake zinakandamizwa.

Nchi zilizoendelea hata kichaa hawezi kumpiga mwanamke, achilia mbali aliye mja mzito. Kitendo hiki cha kinyama kililaaniwa na wananchi wa Lushoto mjini na wa kule vijijini. Nami niliungana nao kulaani kitendo hicho.

Nafikiri baada ya maandamano ya kupinga bei ya umeme, maandamano ya kudai Katiba mpya, yafuate maandamano makubwa ya nchi nzima ya kulaani polisi kuwaua watu kule Arusha na kitendo kibaya cha kumpiga mja mzito.

Maandamano haya yawe na lengo moja la kuwataka wote walioshiriki katika zoezi hili la aibu kubwa kuachia ngazi mara moja.

Mwalimu Nyerere, aliunda vyombo vya usalama wa wananchi na wala si vyombo vya kuwaua wananchi. Utamaduni huu wa mauaji si wa Watanzania.

No comments: