Saturday, January 8, 2011

TUCTA yawakataa CUF, NCCR

na Asha Bani
WAKATI Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR -Mageuzi wakithibitisha kushiriki maandamano yaliyoandaliwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) ya kupinga ongezeko la bei ya umeme Katibu Mkuu wa shirikisho hilo Nicholas Mgaya amewakana.

Akizungumza katika kipindi cha asubuhi kinachorushwa na televisheni ya Chanel Ten alisema shirikisho hilo halina haja na kufanya maandamano na chama chochote cha siasa na kwamba TUCTA wenyewe wanajuana.

Alisema hii hoja inawaumiza Watanzania wote lengo ni kuitaka serikali kusikiliza kilio cha watanzania kupitia wafanyakazi lakini halitakiwi kuwa la kisiasa zaidi kama vyama vinataka kuandamana basi viandae maandamano yao.

“Sisi hatuhitaji maandamano yetu kushirikisha vyama vya siasa si CUF, CHADEMA, NCCR, TLP wala chama chochote hatukihitaji bali tunahitaji wanachama wa shirikisho hilo tu na kwamba wenyewe tunajuana,” alisema Mgaya.

Mgaya alisema wao wanataka kufanya maandamano ya amani lengo likiwa ni kupinga kupanda kwa bei ya umeme ambayo itasababisha ugumu wa maisha uliopo sasa kutokana na hata wafanyakazi wenyewe kupata mshahara usio kidhi mahitaji yao.

Alisema umeme unategemewa katika kukuza uchumi wa taifa na hata uchumi wa mtu binafsi hivyo ni lazima serikali ikafanya jitihada zozote za kutumia vyanzo mbalimbali vya maji ili kuweza kufanya upatikanaji wa umeme kuwa wa uraisi zaidi.

Akizungumzia kuhusiana na kusikilizwa mahitajio yao ambayo kwa mwaka 2010 walidaiwa kupamba vyombo vya habari kwa maandamano kila kukicha alisema bado hayajatatuliwa ila wanaahidiwa ahadi nyingine mpya na serikali.

Alisema kwa sasa ana imani kubwa na waziri aliyepo kwa kuwa ameonesha nia ya kuwasaidia kutokana na ziara zake mbalimbali alizozifanya na kukutana na viongozi kadhaa wa shirikisho hilo na kufanya mazungumzo nao.

“Sisi tunapenda kufanya kazi na viongozi wanaojali watu wanaowatumikia kwa sasa waziri ameanza vizuri na mwaka huu hatutarajii yatokee yaliyotokea mwaka jana kwa kuwa tayari tumekaa na waziri pamoja tumezungumza naye hivyo mwaka huu tunatarajia kuona mafanikio kwetu ya tuliyokuwa tunaahidiwa tangu malalamiko yetu yapelekwe serikalini,” alisema Magaya.

No comments: