Sunday, January 9, 2011

Dowans mvurugano

• Sitta akerwa, akiri ’wajanja’ wamewabana kila kona


na Waandishi wetu
KUNA kila dalili zinazoonyesha kwamba hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Kusuluhisha Migogoro ya Uwekezaji (ICC) ambayo hatimaye imeridhiwa na serikali, imeleta ufa mkubwa miongoni mwa mawaziri na wanasiasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Daima Jumapili limebaini.

Moja ya matukio ya hivi karibuni yanayothibitisha kuendelea kuwapo kwa mizozo isiyokwisha na misiguano ndani ya serikali kuhusu jambo hilo ni hatua ya Rais Jakaya Kikwete ambaye siku zote amekuwa mwepesi kutoa kauli kila linapotokea jambo kubwa na zito kukaa kimya pasipo kusema lolote kuhusu hukumu hiyo ambayo inaitaka serikali kuilipa Dowans fidia ya shilingi bilioni 94.

Uamuzi wa Rais Kikwete kuamua kukaa kimya pasipo kulizungumzia wakati alipolihutubia taifa kwenye mkesha wa mwaka mpya na akaendelea kulifumbia macho hata alipozungumza na mabalozi wa mataifa ya nje juzi, ni kielelezo cha wazi kwamba uamuzi wa ICC ni shubiri kubwa serikalini.

Hatua ya Rais Kikwete kukaa kimya ilhali rekodi zikionyesha kuwa ama yeye mwenyewe au ofisi yake wamekuwa wepesi kutoa matamshi kila mara linapotokea jambo kubwa linalogusa sakata la Richmond au Dowans, kwa kiwango kikubwa imeibua maswali mengi vichwani mwa wadadisi mbalimbali wa mambo.

Ukimya huo wa Kikwete ndio ambao kwa nyakati mbili tofauti hivi karibuni umesababisha Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa kuibuka na kumhusisha rais moja kwa moja na sakata hilo la Dowans na Richmond.

Wakati Rais Kikwete akiendelea kukaa kimya kinyume cha desturi yake, viongozi wa juu watatu; Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, kwa nyakati tofauti wametoa kauli za kuridhia kulipa mabilioni hayo ya fedha kama ilivyotakiwa kufanywa na ICC.

Kiongozi wa mwisho kutoa kauli hiyo ni Ngeleja, ambaye juzi alizungumza na waandishi wa habari na kutangaza rasmi kwamba serikali ilikuwa imeridhia uamuzi huo wa ICC na kwamba kinachosubiriwa kwa sasa ni kusajiliwa kwa kesi hiyo katika Mahakama Kuu ya Tanzania kama sheria inavyotaka.

Kauli hiyo ya juzi ya Ngeleja, imemtoa ’mafichoni’ Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, ambaye jana alirejea tena msimamo wake wa kupinga hatua ya serikali kukubali kuilipa Dowans mabilioni hayo ya fedha kabla ya Baraza la Mawaziri kukutana na kujadili kwa kina suala hilo.

Sitta aliyekuwa akihutubia kwenye mahafali ya Shule ya Sekondari ya Maranatha mjini Arusha, alisema ni jambo lisiloingia akilini kusikia kwamba serikali inailipa Dowans kiasi hicho kikubwa cha fedha ambazo zinaweza kutumika kujenga shule 300 za sekondari.

Waziri Sitta ambaye kwa namna yoyote uamuzi wa serikali kulipa mabilioni hayo unamgusa moja kwa moja kutokana na ukweli kwamba ndiye aliyekuwa Spika wa Bunge aliyesimamia kijasiri uchunguzi wa sakata la Kampuni ya Richmond, ambayo mkataba wake ulirithiwa na Dowans, alieleza kusikitishwa na hatua ya Jaji Werema kukata tamaa ya kuendelea na kesi.

“Kitendo cha serikali kukubali kulipa mabilioni ya fedha kwa kampuni hewa ni hatari kwa jamii. Siku za usoni wananchi watatuhukumu kwa hilo,”' alisema Sitta katika kauli ambayo ilionekana kupingana na tamko la Waziri Ngeleja ambaye aliwataja kwa majina wamiliki wa Kampuni ya Dowans ambayo imesajiliwa kwa Wakala wa Makampuni nchini.

Huku akionyesha kumlenga mfanyabiashara mmoja maarufu ambaye pia ni mwanasiasa pasipo kumtaja kwa jina, Waziri Sitta alieleza kushangazwa na mfumo wa usajili wa makampuni hapa nchini ambao unamuwezesha mtu mmoja kumiliki kampuni 17 pasipo jina lake kuonekana popote.

“Tutafanya nini wakati wajanja wenzetu wameshatuwahi na kutubana kila kona, sasa tutalazimika kuwalipa mabilioni ambayo yangetusaidia kwenye shughuli za maendeleo,” alisema Sitta kwa masikitiko.

Kauli hiyo ya Sitta inafanana na ile iliyotolewa na mwanasheria mmoja maarufu aliyezungumza na Tanzania Daima Jumapili hivi karibuni ambaye alisema upo uwezekano wa watu wenye hisa katika kampuni kama ya Dowans kutojulikana.

Mwanasheria huyo ambaye aliomba jina lake lisitajwe kutokana na maadili ya kazi yake alisema, kumekuwa na mbinu nyingi zinazotumiwa na baadhi ya vigogo katika kuingia na kuwekeza ndani ya makampuni mbalimbali nchini.

Alisema moja ya mbinu za namna hiyo ni ile ya kuwatumia mawakala au mawakili kushikilia hisa zao wakiingia mikataba mahususi ya siri ambayo aghalabu haiwezi kujulikana kwa watu wengine wasiohusika.

Kwa mujibu wa mwanasheria huyo maarufu, sababu kubwa ya vigogo kutumia mbinu hiyo ni kukwepa tuhuma mbalimbali zikiwamo zile za kuonekana kuwa watu waliojilimbikizia mali kinyume cha maadili ya uongozi.

“Unajua viongozi wengi ni wajanja, wamekuwa wakitumia mbinu ya kuweka mawakala au mawakili kushika hisa zao ili kukwepa kuonekana wanajiingiza katika masuala ya biashara,” alisema.

Alieleza kuwa taratibu na sheria za kuwekeza nchini zinamtaka mwekezaji kuijua nchi vizuri pamoja na kuwa na hati ya makazi (A) (Residensial Permit).

“Kama mwekezaji haijua nchi atawekezaje? Ni lazima awe na hati ya ukaazi na tena awe na ofisi inayofanya kazi, siyo ofisi inayoishia kwa mwanasheria na hakuna sheria inayozuia mgeni kuwekeza binafsi….anaweza kuwekeza yeye na familia yake, mradi awe amefuata taratibu,” alisema.

No comments: