Saturday, December 18, 2010

Nakusikitikia mheshimiwa Sitta

Samson Mwigamba
NILITAMANI sana kukupigia simu siku ile ‘ulipochakachuliwa’ kwenye nafasi ya uspika. Ni kwa bahati mbaya kwamba nilipoongoza majeshi kwenye ofisi za manispaa ya Arusha kudai matokeo ya kura za ubunge yatangazwe kama yalivyo simu yangu ilichukuliwa na namba zako nikazipoteza.
Waliichukua vijana ambao wameteseka kwa muda mrefu ndani ya manispaa ya Arusha ambao maisha yao ya kesho hayajulikani.

Ni wale vijana ambao hutembea barabarani kutwa nzima wakiuza seti mbili za vikombe vya chai. Ni vijana hao ndio hawaoni mwanga wa kwenye maisha yao huko waendako. Ndio hao walioamua kufanya mabadiliko ya uongozi. Ndio waliosimama nje ya geti la jengo la manispaa ya Arusha wakidai matokeo.

Waliwasili hapo tokea saa 12 asubuhi na hawakutoka bali waliongezeka mpaka saa 11 jioni matokeo yalipotangazwa rasmi. Walipoamua kuchukua simu nilikubali na kuwaachia.

Mheshimiwa Sitta, nasikitika kushindwa kuwasiliana nawe kwa sababu nimekuwa rafiki yako wa karibu siku hizi na bila shaka kama ningewasiliana nawe ungenisikiliza na usingefanya maamuzi uliyoyafanya hivi sasa ambayo kimsingi ndiyo yanayonifanya nikusikitikie.

Tatizo kubwa ni kwamba ulipata nafasi ya kuwa shujaa zaidi ya mara mbili lakini hukuitumia. Sasa nakusikitikia kwa sababu njia uliyoiendea naona inakupeleka kusiko. Umenifanya nikumbuke maneno yangu niliyokuandikia kwenye makala ya Kalamu ya Mwigamba ya Agosti 26, mwaka jana iliyokuwa na kichwa kilichosema, “Mheshimiwa Sitta, Waweza kuwa Shujaa Ukiamua”. Najua ulishasahau japo baada ya kusoma makala ile tuliongea kwenye simu. Naomba niweke hapa sehemu tu ya makala ile kwa ajili ya kukukumbusha nilishosema kabla sijafunga makala yangu ya leo:
“MHESHIMIWA naomba uniazime muda kidogo na uyapitie kwa makini sana yale yote kalamu hii iliyonuia kukueleza kwa kuwa kwa kiwango cha uelewa wa kalamu hii yatakuwa yanabainisha hatma ya maisha yako ya kisiasa. Hata hivyo, kalamu hii siku zote imeweka mbele uungwana na kutoa uhuru.

Kwa hiyo waweza kuchagua kuisikiliza ili uishi kisiasa na vile vile waweza kuchagua kutupilia mbali maneno yake kwa hatari ya kufa kisiasa ama kubaki kama ‘boya’ katika siasa ambalo kama ujuavyo hufuata upepo. Lakini nakufahamu vizuri Mzee wa Viwango na Kasi a.k.a Standard and Speed (SS). Naamini hutatupilia mbali maneno ya kalamu hii bali utayatafakari vema si tu kwa faida yako ya kisiasa bali pia kwa manufaa ya taifa hili.

“Mheshimiwa Sitta, Spika wa Bunge la viwango Afrika Mashariki na Kati, kwanza kabisa niruhusu nikupe pole kwa yaliyokukuta ndani ya mji mkongwe wa Idodomya. Lakini napenda nikupongeze kwa stahili yako ya kuruka vihunzi.

Najua wengi wameponda habari za kwamba uliomba radhi na umeandikwa sana. Rafiki yangu mmoja alikuita ‘jemedari aliyesalimu amri’. Lakini mimi nina sababu mbili za kukupongeza kwa yaliyotokea ndani ya NEC. Kwanza kabisa kwa sasa wengi tumekosa uhakika ikiwa ni kweli uliomba radhi au hukuomba. Gazeti moja ninalolipenda sana na kuliamini wiki iliyopita liliandika kwamba wewe hukuomba radhi ila ulitamka kwamba “kutenda kosa si kosa, bali kurudia kosa”. Maneno haya kama ni kweli ndiyo uliyoyatamka ndani ya kikao cha NEC basi sisi hatuwezi kujua ulichomaanisha mpaka wewe mwenyewe utakaposema.

“Sababu yangu ya pili ni kwamba kuna wakati ambapo jeshi hulazimika kunyanyua mikono ili kujipa muda wa kutafuta namna ya kujinasua. Huko nyuma niliwahi kueleza kwamba hata chama chako cha CCM imekuwa ni mbinu yake kwa muda mrefu. Si unakumbuka wakati wana CCM wengi mmekubali kwamba Waziri Mkuu ajiuzulu na kufanya Bunge lisiendelee kwa siku mbili kwa kuwa hakukuwa na serikali?

Ile ilikuwa ni mbinu ya kunyanyua mikono halafu umwangalie adui kakaaje halafu umshambulie. Kwa ujumla kile ambacho Watanzania wengi wamekuwa wakikiita kutoana kafara ndani ya serikali ya CCM ni kunyanyua mikono ili kutafuta njia ya kutoka na wewe unalijua zaidi hilo maana uko jikoni kwa CCM.

“Yaani wanafika mahali kwa sababu wamebananishwa wanakubali kwamba wamekosa na kufanya mambo machache ya kuudanganya umma kwamba wamekiri na wameamua kubadilika kumbe wanageuka ghafla na kurejea kule kule. Nachukulia mfano mwingine wa kukubali kwamba kumekuwa na ufisadi wa kutisha ndani ya serikali na Benki Kuu na kumfukuza kazi gavana wa Benki Kuu na kuagiza kwamba waliohusika warudishe pesa ama wapelekwe mahakamani na hatimaye ‘vifisadi’ vichache vidogo vidogo vinafikishwa mahakamani kwa kesi za kizushi halafu serikali inatangaza kwamba inapiga vita ufisadi ili kuwafumba macho wadanganyika na wao waendeleze ufisadi tena kwa Ari mpya, Nguvu mpya na Kasi mpya.

“Kwa hiyo sitashangaa kama kauli yako iliyotafsiriwa na baadhi ya watu kwamba ni kuomba radhi, itakuwa ni kurudisha majeshi nyuma ili ujipange upya. Kama ndivyo nakuunga mkono kwa sababu moja. Kwamba kama ungeamua kuwa ngangari pale pale na kukataa kutoa kauli yenye ‘radha’ ya kuomba radhi, wangekuvua uanachama pale pale na ungetoka ukiwa si mwana CCM na hivyo si mbunge na si Spika wa Bunge la Jamhuri. Najua kuna watakaosema kwamba kuna protokali kwamba ni lazima waiandikie ofisi ya bunge barua ya kuonyesha kwamba huna uanachama wa chama chao tena, na hivyo nafasi zako za ubunge na uspika ziko wazi. Lakini bado katika muda huo wa kufanya hivyo wewe usingekuwa na la kufanya tena. Usingekuwa tena na nguvu ya kuwaita majemadari wako na kupanga nao mikakati ya namna ya kutoka na yumkini wengi wangekataa hata kukusapoti wakihofia mustakabali wao. Ni muhimu kukumbuka kwamba wakati huo ungewaita ukiwa raia wa kawaida kwa hiyo wangeweza hata kutotilia maanani ushauri ambao ungekuwa unawapatia.

“Baada ya kusema hayo sasa nikueleze yajayo na kukupatia ushauri wangu. Mheshimiwa, kwa sasa unasimama njia panda. Mbele yako kuna njia mbili za kufuata, nazo ni kufyata mkia mbele ya mafisadi na ‘ukafa’ kisiasa au kutunisha misuri mbele ya mafisadi ‘ukafa’ kimaslahi ya muda lakini ukainuka juu ya ardhi ya Tanzania na kuwa shujaa wa aina yake ambaye kwa hakika tuzo yako itakuwa inakaribia ile ya Nyerere katika nchi hii na duniani. Ukichagua njia ya kwanza yafuatayo yanakusubiri: Kwanza unajua vizuri kwamba wakubwa wengi wa CCM wameshakuweka alama kwamba wewe ni mpinzani wao.

Kalamu hii inapenda ikuhakikishie kwamba hata kama utaamua kufyata mkia bado hutakuwa mwenzao. Wataendelea kukupiga vita maana hawatakuwa na uhakika kwamba hutawageuka tena. Ubunge wa Urambo Magharibi utaupata kwa shida kwa kuwa utakuwa na wapinzani watatu ambao wote utalazimika kuruka vihunzi vyao.

“Mpinzani wako namba moja watakuwa ni mafisadi ambao walitaka kukuvua uanachama. Watafanya kila liwalo usirudi bungeni na unajua maana ulishasema kwamba tayari wako jimboni wakitaka kukung’oa. …Wataendelea na juhudi zao za kukung’oa kwa sababu niliyoieleza hapo juu kwamba hawatakuwa na imani kwamba umefyata mkia kweli na kwamba hutawasulubu tena bungeni. Mpinzani wako wa pili watakuwa ni wananchi wenyewe wa Urambo ambao hata juzi umewahakikishia kwamba uko ‘ngangari’ na kwamba utaendelea na kasi ile ile ya utendaji na baadaye ukawaambia waandishi wa habari kwamba utapigana na mafisadi mpaka kufa. Wana Urambo kwa kusaidiwa na watanzania kwa ujumla wataona kwamba umewasaliti wataazimia kukunyima kura zao. Na mwisho utakuwa unapambana na kijana mmoja machachari kutoka CHADEMA ambaye tayari umesikia habari zake kwamba ametangaza kukuvaa. Utaponea wapi rafiki yangu. Na bado hata ukipenya kwenye tundu la sindano watahakikisha unabaki mbunge wa kawaida hata uenyekiti wa bunge usipate.

“Mheshimiwa Sitta, njia ya kwanza ni hatari kwako. Ni sumu itakayokuua pole pole lakini kwa uhakika. Utaendelea kutesa na uspika kwa mwaka mmoja uliobaki kabla rais hajalivunja Bunge hapo Agosti mwakani, lakini kwa taabu kubwa. Sisi Watanzania kwa ujumla tutakuzomea na hatutasita kukuweka kundi moja na mafisadi.

Maneno ya wachangiaji wengi waliochangia hoja ya kukuvua uanachama ndani ya NEC walisema unaichachafya serikali kwa maslahi binafsi ukitumia mgongo wa vita dhidi ya ufisadi. Napenda nikuhakikishie kwamba ukifyata mkia utakuwa umewawezesha Watanzania kupigia mstari kwamba madai hayo yalikuwa ya kweli. Hebu fikiria! Fikiria jinsi utakavyoporomoka na kushusha hadhi yako mbele ya jamii.

Fikiria watakavyokuona kumbe na wewe fisadi na kwamba vita yako ilikuwa kwa sababu ya kunyimwa fursa za ufisadi na uamue kukataa njia hii ambayo kila mwana CCM aliye upande wa pili anatamani uichukue halafu wakumalize.

“Njia ya pili ni hii. Kwamba utaamua kusimama imara. Na kwamba utaonyesha uimara wako hapo Novemba utakapoongoza bunge kuikataa taarifa ya serikali juu ya utekelezaji wa maazimio ya bunge kuhusu mkataba tata wa Richmond. Na utaongoza bunge kuwa kali kabisa na kwa kuanzia, Bunge litamlamzimisha waziri mkuu kujiuzulu na asipofanya hivyo utaliongoza Bunge kupokea na kupiga kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu.

Akina Slaa wako tayari kuleta hoja ndani ya bunge na unao wabunge wengi ndani ya CCM ambao watakuunga mkono kukubali hoja hiyo. Na hata hivyo, sheria itakuwa ikikulinda kwamba serikali imelidharau bunge.

“Mheshimiwa, maamuzi haya hayatapita hivi hivi. Watakaa kwenye kikao chao na kukuita ujieleze kwa nini umekaidi maelekezo yao. Natoa ushauri kwamba usihudhurie kikao hicho maana dhamiri inanituma kuamini kwamba ‘wataku-kolimba’ kwa kukuwekea vile ‘vitu’ vyao kwenye microphone. Usiende kabisa pale utakapoambiwa kwamba unaenda kuhojiwa.

Na kama hutajua agenda za kikao halafu ghafla kufika huko ukasikia unaambiwa ujieleze, basi utasimama kana kwamba unataka kujieleza halafu unatoka nje ya kikao na kupanda shangingi lako na kutokomea nyumbani Urambo. Utawaacha wakujadili wenyewe, waulize maswali wenyewe, wajibu wenyewe na kuamua kukuvua uanachama wenyewe.

“Wakati huo, utakuwa umeshaweka mikakati na makamanda wako. Na nakushauri mikakati hiyo uiweke sasa, usisubiri wakati huo. Waulize kwanza mmoja mmoja upate wale wanaokuhakikishia kwamba watapigana mpaka mauti itakapowakuta. Hao ni lazima ukubaliane nao kwamba mbele yenu kuna kuvuliwa uanachama na ubunge wenu kwa pamoja. Hao mkubali na muwe tayari kwa hilo. Na kwa sababu hiyo mtakuwa tayari kuhamia chama cha upinzani chenye sera na mikakati inayofanana na hiyo ya kwenu. Kalamu hii inakupa uhakika mmoja tu, kwamba wewe mheshimiwa Sitta ukipata wabunge wenzako watano tu ambao watakuwa tayari kuvuliwa uanachama na wakajiunga na upinzani.

Halafu tukakodi helikopta mkazunguka nchi nzima mkawaeleza wananchi kile kinachoendelea ndani ya lile dude kubwa liitwalo CCM, ndiyo utakuwa mwisho wa CCM, mwanzo mpya, mwanzo wa fikra mpya, mabadiliko halisi, uhuru wa pili wa mtanzania na maendeleo yenye ‘viwango na kasi’. Kama vile Nyerere anavyotukuzwa kwa kujitoa mhanga kuwafukuza wakoloni, ndivyo na wewe na wenzako mtakavyotuzwa pamoja na mashujaa wenzenu akina Mbowe, Slaa na wengineo kwa kuwafukuza wakoloni weusi.

Mwisho wa siku utamshuhudia yule rafiki yako mnayepambana naye akiwa kwenye viti vya upinzani bungeni …. na wewe ukiwa umekalia kiti cha Waziri Mkuu ndani ya ukumbi huo huo.

“Huenda haya ninayoyazungumza yakaonekana kama hadithi za Alinacha lakini ukitafakari kidogo na kuirejea historia ya dunia ukitilia maanani historia za watu kama Nelson Mandela, utanielewa na utachukua hatua ninazokueleza leo na mwisho wa siku utaishukuru kalamu hii kwa kukusaidia kuwa Shujaa wa Mwaka na shujaa wa mwongo”.

Tafakari maneno yangu ya Agosti, mwaka jana uone ni uamuzi upi uliouchukua. Kwanza kuhusu Richmond na Dowans dada yake, ulifyata mkia ukafunga hiyo hoja bila hitimisho na leo taifa linakabiliwa na kulipa bilioni 185 kama faini kwa Dowans. Na kama nilivyokueleza kwamba kuufyata mkia kusingekusaidia, ni kweli umepenya ubunge wa Urambo kwa taabu na hatimaye uspika wakakuchinjia baharini.

Sasa umefanya kosa lingine la kukubali kuwa kwenye baraza la mawaziri tena uwaziri wenyewe wa Afrika Mashariki ! Halafu bado unatamba kwamba utaendeleza vita dhidi ya ufisadi !? Mheshimiwa umekosea sana. Hujui kinachokusubiri mbeleni na nataka nikutahadharishe kwamba mwanzo wa mwisho wako kisiasa umeshaanza. Muda si mrefu tutakusahau. Endelea kufuatilia vyombo vya habari.

Watanzania hawakuamini kwamba ni wewe uliyejinasibu kwa kupigana vita dhidi ya ufisadi leo unakubali kuwa kwenye baraza la mawaziri la rais yule yule, waziri mkuu yule yule, na mbaya zaidi la chama kile kile ambacho juzi tu kilikutosa kwenye uspika kwa sababu kwamba kwa kupigana kwako na ufisadi ulihatarisha maslahi ya chama.

Leo kwa kukubali kuwa kwenye baraza lile lile ambalo kama unavyojua leo likiamua kuingiza Richmond namba mbili utakuwa umehusika kwa kanuni ile ya uwajibikaji wa pamoja, unawezaje kuuzuia umma kukubaliana na maelezo ya wajumbe wa NEC ya chama chako waliosema : unaichachafya serikali kwa maslahi binafsi ukitumia mgongo wa vita dhidi ya ufisadi ?

Sasa ngoja jamaa walete hoja binafsi bungeni kwamba wewe na kundi lako mmeliingizia hasara taifa kwa kusababisha taifa lilipe bilioni 185 kumbe mlikuwa na ajenda binafsi ya kutaka kumng’oa waziri mkuu na hatimaye na nyinyi muingie serikalini kwenye uwaziri. Sijui mtaponea wapi ? Na kuna kauli ile ya Kardinali Polycarp Pengo kwamba waliokuwa wakipiga kelele wakati ule ndani ya CCM za vita dhidi ya ufisadi ni kwa sababu walikuwa wamekosa nafasi za ‘kufisidi’.

Mara baada ya kukamilisha ‘mission’ mliyokuwa nayo mkafunga mjadala na kutulia. Na sasa mmeingizwa serikalini ndo mtatulia kabisa. Maneno ya Kardinali hayatakuwa yametimia ? Tafakari na uchukue hatua ! vinginevyo mimi rafiki yako nasubiri kuona.


Tuwasiliane : smwigamba@yahoo.com; 0713 953761 au 0767 953761.

No comments: