Saturday, December 18, 2010

Magufuli, Mwakyembe hatarini

• Mipango ya kuwakwamisha yaandaliwa


na Mwandishi wetu




MIKAKATI ya kuwakwamisha kiutendaji Waziri wa Ujenzi, John Magufuli na Naibu wake, Dk. Harrison Mwekyembe, inadaiwa kuanza kuandaliwa na vigogo wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kushirikiana na baadhi ya makandarasi, Tanzania Daima Jumapili imedokezwa.

Mawaziri hao wameanza kuonekana tishio kwa baadhi ya vigogo wa TANROADS ambao inadaiwa walikuwa wakijinufaisha kupitia zabuni mbalimbali zilizokuwa zikitangazwa na serikali.

Vigogo hao wa TANROADS inadaiwa walikuwa wakivuna fedha kutoka kwa wamiliki wa kampuni za ujenzi ambao walikuwa wakitoa fedha ili kujenga ushawishi wa kampuni zao kupewa ushindi wa zabuni husika.

Tanzania Daima Jumapili imedokezwa kuwa hivi sasa baadhi ya vigogo hao wamekuwa na wasiwasi wa kuendelea na mchezo huo wa kuvuna fedha hasa baada ya Rais Jakaya Kikwete kumteua Magufuli kuwa Waziri na Dk. Mwakyembe kuwa Naibu Waziri.

Magufuli alipoanza kazi katika wizara hiyo alibatilisha tangazo la ajira lililotolewa na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TANROADS, Ephraim Mrema, ambaye kwa muda mrefu amekuwa akishtumiwa kwa kuiendesha ofisi hiyo kwa masilahi ya kundi fulani la watu.

Kinachochangia wasiwasi wa watendaji hao ni hatua ya wizara hiyo kutoa taarifa kuwa imempa barua ya kuondoka kazini Mkurugenzi wa TANROADS, Ephraim Mrema, ambaye kwa muda mrefu amekuwa akituhumiwa kuitumia ofisi hiyo kwa masilahi binafsi.

Mrema, pia alikuwa akidaiwa kufanya marekebisho kwa baadhi ya watendaji mikoani na makao makuu kwa lengo kuweka safu mpya itakayokuwa na utii kwa yale atakayokuwa anawaagiza.

Marekebisho hayo yalizusha mzozo mkubwa ambao ulitikisa TANROADS na Wizara ya Miundombinu iliyokuwa ikiongozwa na Dk. Shukuru Kawambwa ambaye kila mabadiliko yanayofanywa na Rais Jakaya Kikwete katika baraza la mawaziri humkumba.

Tanzania Daima Jumapili imedokezwa kuwa baadhi ya makandarasi ambao walikuwa wakinufaika na kuwapo kwa Mrema hivi sasa wanafanya mikakati ya chini kwa chini ikiwamo kuhujumu baadhi ya miradi ili uongozi wa Mafuguli uonekane haufai, hasa katika sekta ya ujenzi wa barabara.

Habari hizo zilidokeza pia kuwa Mrema, alikuwa akiungwa mkono na baadhi ya vigogo waliopo serikalini ambao wana kampuni za ujenzi lakini wamekuwa wakiwatumia ndugu au jamaa zao kuziendesha.

Tanzania Daima Jumapili, ilidokezwa pia kuwa Mrema alikuwa na uhusiano na baadhi ya vigogo wa ikulu au familia zao jambo lililokuwa likichangia kwa kiasi kikubwa kuzorota kwa ushirikiano na wafanyakazi wenzake.

Taarifa hizo zilidai Waziri Magufuli, anaonekana kuwa tishio kwa makandarasi wa barabara ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakinufaika na fedha za ujenzi wa barabara, ambapo walikuwa wakizidisha gharama zake.

Wakati wa utawala wa Magufuli katika wizara hiyo, ujenzi wa kilometa moja ya lami ilikuwa sh milioni 300-400 lakini hivi sasa kilometa moja ni sh bilioni moja.

Wataalamu wa masuala ya ujenzi wanabainisha kuwa pamoja na kupanda kwa gharama za vifaa, lakini gharama za ujenzi wa kilometa moja ya lami kwa sh bilioni moja ni mkubwa na kuna uwezekano baadhi ya watendaji na makandarasi wananufaika na ongezeko hilo.

Wataalamu hao wanadokeza kuwa Magufuli atakabiliwa na wakati mgumu wa kurekebisha jambo hilo ambalo kwa kiasi kikubwa linawanufaisha makandarasi na wale wanaofanikisha mipango ya kuwapatia zabuni.

Ufuatiliaji wa karibu wa Magufuli pamoja na uwezo wake wa kuhifadhi takwimu ndio unaowatia hofu wale wote waliokuwa wakinufaika na fedha za serikali kwa kutumia njia za mkato.

Historia ya Magufuli kufuatilia ubora wa barabara au jengo linalojengwa ndio unaozidisha hofu kwa makandarasi ambao wamekuwa wakijenga chini ya viwango kwa lengo la kujinufaisha zaidi.

Mara kadhaa wakati akiwa Waziri wa Ujenzi, Magufuli alikuwa akiyakataa majengo, barabara au kuvunja mikataba pale anapoona havikujengwa kwa kiwango kinachotakiwa.

Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili kuhusu kuwapo kwa taarifa hizo za kuhujumiwa, Mwakyembe alisema ni mapema mno kulizungumzia jambo hilo, kwa sababu ndiyo kwanza ameingia ofisini na anahitaji muda zaidi kujua nini kinafanyika ndani na nje ya ofisi hiyo.

Alisema kuwa muda ndio utakaoamua kuhusu njama hizo, lakini katika mazingira ya kawaida hakuna mkandarasi au mtendaji wa serikali ambaye anaweza kufanikisha hujuma kubwa kama hiyo.

“Ndugu yangu, sina jibu la kukupa kuhusu njama hizo, lakini ni vema tukapeana muda ili tuweze kufanya kazi,” alisema Mwakyembe.

No comments: