Wednesday, December 8, 2010

Moto wafuka Ivory Coast

• Wagombea kila mmoja atangaza baraza lake

na Mwandishi wetu, ABDIJAN, Ivory Coast



MGOGORO uliotokana na matokeo ya uchaguzi nchini Ivory Coast umezidi kupamba moto licha ya jumuiya za kimataifa kukataa kutambua ushindi wa Rais Laurent Gbagbo.

Laurent Gbagbo na kiongozi wa upinzani Alassane Ouattara, kila mmoja anadai kuwa ni rais wa Ivory Coast na wote wamekula kiapo cha kuongoza nchi hiyo.

Moto wa mgogoro huo umezidi kupamba moto jana, baada wote wawili kila mmoja kuendelea na zoezi la kuteua baraza lake la mawaziri.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi, imemtangaza mshidi wa uchaguzi huo uliofanyika Novemba 28 mwaka huu kuwa ni Ouattara. Lakini mahakama ya kikatiba ilipindua matokeo hayo ikidai kuwa ni batili na hivyo kumuidhinisha Gbagbo kuwa rais wa nchi hiyo.

Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS), Marekani, Ufaransa, Uingereza, na nchi nyingine, zimekataa kumtambua Gbagbo kama rais wa nchi hiyo.

Jana Rais wa Marekani, Barack Obama, alimtaka Gbagbo kukubali kuwa alishindwa katika uchaguzi wa hivi karibuni na kumkabidhi madaraka mpinzani wake, Ouattara.

Katika taarifa yake Obama alisema anamtambua Ouattara ndiye mshindi halali katika uchaguzi huo.

Tayari Umoja wa Nchi za Ulaya umetishia kumuwekea vikwazo Gbagbo endapo ataendelea kung’ang’ania madarakani.

Wakati hayo yakiendelea, Jeshi la Umoja wa Mataifa liliendelea kuimarisha ulinzi kwa Ouattara.

Naye Gbagbo amezitahadharisha nchi za kigeni zisiingilie kile alichodai ni masuala ya ndani ya Ivory Coast.

Wachunguzi wa mambo walitarajia kuwa uchaguzi wa Ivory Coast ungelimaliza mgogoro wa miaka mingi nchini humo, lakini inaonekana kwamba uchu wa madaraka umelibadilisha zoezi hilo la kidemokrasia na kuwa chachu ya machafuko na mgogoro.

Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, ambaye alitumwa na Umoja wa Afrika (AU) kwenda nchini humo kwa ajili ya kusuluhisha mgogoro huo anatarajia kutoa ripoti yake baada ya kukutana na pande zote mbili.

Duru ya pili ya uchaguzi wa Ivory Coast ilifanyika Novemba ikiwashirikisha mahasimu hao wawili, Laurent Gbagbo na Alassane Ouattara, baada ya uchaguzi wa kwanza kutotoa mshindi.

Nchi ya Ivory Coast imekumbwa na mgogoro wa ndani tangu mwaka 2002, ambapo machafuko yaliyotokea kwenye mgogoro huo yameigawa nchi hiyo kwenye sehemu mbili.

Sehemu ya kwanza ni ya kaskazini yenye wafuasi wengi wa upinzani na nyingine ni ya kusini inayodhibitiwa na wanamgambo wanaoongozwa na Laurent Gbagbo.

Mgogoro huo umevuruga sana uchumi wa nchi hiyo iliyokuwa ikiongoza kwa kuwa na uchumi mzuri magharibi mwa Afrika.

Kwa upande wao wachambuzi wa mambo wanasema kuwa hivi sasa ni mapema mno kujua mgogoro uliozuka nchini humo utamalizikia vipi na kwa namna gani

No comments: