Wednesday, December 8, 2010

Sitta afyatuka

• Adai Dowans ni genge la ulaji wa vigogo watatu

na Mwandishi wetu



WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amesema ametishwa na hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC), iliyoipa ushindi Kampuni ya Dowans dhidi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), lakini akasema haya ni matokeo ya genge la watu wachache wanaofahamika ambao wameamua kutafuna rasilimali za taifa bila huruma.

Sitta ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano katika miaka mitano iliyopita na ambaye aliruhusu Bunge kujadili masuala kashaa ya kifisadi, alisema hayo jana katika mazungumzo maalumu na Tanzania Daima kwa simu kutoka Kampala Uganda.

Alisema vigogo hao waliileta Dowans makusudi baada ya kampuni ya awali iliyopewa zabuni ya kufua umeme wa dharura, Richmond Development LLC, kushindwa kutimiza malengo.

Dowans ndiyo ilirithi mkataba wa Richmond na kwa mujibu wa Sitta, njama za kuileta kampuni hiyo zilisukwa na vigogo watatu ambao ni wabunge wa muda mrefu na wamekuwa wanahusishwa na matukio mbalimbali ya ufisadi, na mmojawao ni mwanasheria maarufu aliyebobea katika masuala ya mikataba ya kimataifa. Kwa sababu za kitaaluma, gazeti hili litahifadhi majina yao kwa sasa.

Kwa mujibu wa Waziri Sitta, hili ni genge ambalo limeamua kutafuna rasilimali za taifa bila huruma, na bila kujali maslahi ya vizazi vijavyo.

“Nakwambia hakuna jambo ambalo linakera kama kuona genge la watu wachache limeamua kutafuna rasilimali za taifa hili bila huruma. Wameshindwa kufikiria kizazi kijacho kitanufaika vipi.

“Hii inaletea hisia kuwa kundi hili linaendesha hujuma nzito dhidi ya mali za taifa hili… haiwezekani hata kidogo kununua jenereta halafu unasema huu ni uwekezaji… huu si uwekezaji,” alisema Sitta.

Alisema hukumu iliyotolewa dhidi ya TANESCO ni mwendelezo wa hujuma kubwa dhidi ya taifa kwa vile inaonekana wazi kwamba kuna kundi la watu maarufu ambalo ndilo chanzo cha suala hilo, na ambalo kwa namna moja au nyingine lilishiriki kuhujumu mwenendo wa kesi ili serikali ishindwe, wao walipwe pesa.

Alisema Dowans ni mali ya wachache hao ambao wameamua kufumba macho ili kufanikisha malengo yao kibiashara, na kwamba umefika wakati serikali iamue kwa nguvu zote kuwashughulikia bila huruma kwa vile ni sawa na wahujumu uchumi.

“Sisi tulioko serikalini lazima tukomeshe hali hii… kwani mchezo huu umekuwa ukijirudiarudia mara kwa mara. Lazima tujipange vizuri ili kuhakikisha nchi haichezewi tena.

“Serikali iko kwa ajili ya watu. Sasa iweje tushindwe kujipanga vizuri, tunataka kuona wananchi wetu wananufaika na rasilimali zilizopo, na hiyo ndiyo sifa (yetu) kwa taifa,” alisema Sitta.

Alisema hata hukumu hiyo ni matokeo ya watu fulani ambao walitaka kesi hiyo isikilizwe nje ya nchi kisha wagawane fungu la fedha zitakazopatikana.

“Inashangaza mno kuona kuna watu fulani wamekuwa wakipendekeza kesi hizi zisikilizwe nje ya nchi… lazima tujiulize, wanavuna nini? Hata hii inawezekana wazi ulikuwa mpango wao wa kuhakikisha wanapokamilisha mambo yao wanagawana wanachovuna.

“Wamesababisha mahakama zetu zinyang’anywe uwezo wa kusikiliza kesi hizi... wanawapelekea Wazungu… hii haijakaa sawa hata kidogo,” alisititiza.

Kauli ya Sitta ni ushahidi mwingine wa vita ya makundi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na serikali ambayo imeibuliwa upya na sakata la Dowans.

Sitta anatoa kauli kali hii siku moja baada ya mwanasheria mkongwe anayeheshimika nchini, Jaji Mark Bomani, kuzungumza na gazeti hili juzi akisema ushindi kampuni ya Dowans dhidi ya TANESCO ni matokeo ya namna taifa lilivyoshindwa kushughulikia vema mikataba mikubwa ya kimataifa katika uwekezaji na nishati.

Alisema: “Sakata la TANESCO na Dowans linasikitisha. Nafikiri liliendeshwa kwa namna ambayo ingewafikisha wahusika pabaya kama ilivyotokea.

“Fundisho ni kwamba unaposhughulikia masuala yanayogusa mikataba ya kimataifa kama haya yanayohusu nishati, madini na mengineyo, umakini mkubwa unatakiwa,” alisema Bomani.

Mjadala wa mitambo ya Dowans, uliwahi kuligawa taifa kwa kipindi kirefu mwaka 2008 baada ya Kamati Teule ya Bunge chini ya Uenyekiti wa Dk. Harrison Mwakyembe baada ya kutoa taarifa ya kuchunguza uhalali wa kampuni ya Richmond na mtakaba kati yake na serikali.

Kutokana na taarifa iliyowasilishwa bungeni Februari mwaka 2008 aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alijiuzulu ikiwa ni ishara ya kuwajibika kama kiongozi mkuu wa ofisi yake iliyodaiwa kushiriki katika kuiwezesha Richmond kushinda zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura.

Hali ilipokuwa tete, aliyekuwa Mkurugenzi wa TANESCO, Dk. Idris Rashid, aliishauri serikali kuinunua mitambo hiyo, lakini baadhi ya wanasiasa walilisukuma Bunge kukataa kununua mitambo hiyo kwa maelezo kuwa Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004 inakataza serikali au taasisi zake kununua mitumba.

Wengine walikwenda mbali zaidi wakisema ununuzi wa mitambo hiyo utaifaidisha Dowans ambaye ni dada yake Richmond.

Katika uamuzi wa ICC uliotolewa na jopo la majaji watatu chini ya uenyekiti Gerald Aksen na wasuluhihi Swithin Munyantwali na Jonathan Parker, TANESCO imeamriwa kuilipa Dowans fidia ya zaidi ya sh bilioni 36 na riba ya asilimia 7.5 kwa mwaka inayofikia kiasi cha zaidi ya sh bilioni 26 tangu Juni 15 mwaka huu, hadi fidia hiyo itakapolipwa.

Kadhalika, jopo hilo liliamuru malipo ya sh bilioni 60 na riba ya asilimia 7.5 ambayo ni sawa na sh bilioni 55 kuanzia Juni 15, 2010 hadi wakati wa malipo.

Jopo hilo lilisisitiza kuwa ada na gharama za wasuluhishi wa ICC na utawala ni sh bilioni moja zinazotakiwa kulipwa na pande zote.

No comments: