Wednesday, November 10, 2010

Zengwe laibuka nafasi ya Naibu Spika

na Mwandishi wetu, Dodoma




KATIKA hali isiyo ya kawaida na ambayo inayoonyesha kuwapo kwa mizengwe ya kutaka kuchakachuana ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika nafasi ya kugombea Naibu Spika, jina la Mbunge mteule wa Jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma (CCM) Jenister Mhagama, linaandaliwa mazingira ya kuenguliwa.

Habari za uhakika zilizopatikana mjini hapa zinasema kuwa tayari wengi wa wabunge kutoka ndani ya CCM wameunga mkono kupitishwa kwa jina la mbunge huyo ambaye awali kabla ya kuvunjwa kwa Bunge alikuwa Mwenyekiti wa Bunge.

Hata hivyo, alipoulizwa na mwandishi wa habari hizi kuhusu suala lililojitokeza kuwania nafasi hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Uchaguzi ndani ya CCM Mattson Chizi, alisema hana taarifa kama kuna mazingira ya kuliengua jina la muombaji yeyote na kusisitiza kwamba demokrasia itafuata mkondo wake.

Kulingana na Chizi, hakuna mgombea atakayepewa nafasi ambayo kulingana na taratibu za uchaguzi ndani ya CCM hakuiomba, kwa nia ya kufanya upendeleo, badala yake watafanya kazi kwa uadilifu mkubwa ili kukabiliana na malalamiko na kuwapo kwa dalili za hila za kubebana.

Chizi alisema hadi pazia la uchukuaji fomu za kuwania uspika likifungwa jana Novemba 08, 2010 jioni, nafasi ya Spika walijitokeza Job Ndugai, Samuel Sitta, Anna Abdallah, Anne Makinda, Andrew Chenge, Kate Kamba na wanachama wengine nje ya Bunge.

Aidha, alisema nafasi ya Naibu Spika alijitokeza Jenister Mhagama pekee na kwamba hakuna jina la Mwana CCM mwingine, na kwamba hata baada ya kuulizia katika vituo maalumu vilivyofunguliwa katika Ofisi ndogo ya Bunge jijini Dar es Salaam na bungeni Dodoma, kwa maagizo ya Makamba mwenyewe, hakuna aliyejitokeza zaidi ya Mhagama.

Hata hivyo, Makamba alikanusha kutoa taarifa ya kusitishwa ama kuanza upya kwa zoezi la kuchukua fomu za kuwania unaibu spika, na kusema kwamba tangazo la awali lililotolewa na CCM kuhusu namna naibu spika anavyoweza kupatikana limebaki kama lilivyo.

Alisema kuwa kulingana na kanuni za uchaguzi katika nafasi hiyo, mgombea anachukua fomu kupitia ofisi ya Katibu wa Wabunge wa CCM, ambapo atajaza na kuzirejesha kwa wakati ulioagizwa.

Makamba pia aliongeza kwamba hana taarifa za idadi kamili ya watu waliojitokeza kuwania nafasi hiyo, na kwamba ofisi ya wabunge wa CCM imemtaarifu kuwa kuna mgombea mmoja tu, na kwamba yeye hawezi kubatilisha maamuzi hayo.

Hata hivyo, habari za uhakika zilizopatikana mjini hapa zinasema kuwa kuna kila aina ya hila zinazofanywa na kundi moja la Wana CCM wenye nguvu kushinikiza jina la Mbunge mteule wa Jimbo la Kongwa Job Ndugai, kupewa nafasi ya kugombea unaibu spika badala ya Mhagama.

Habari zinasema kuwa waliokuwa mawaziri wa serikali ya Rais Kikwete, Sofia Simba na Hawa Ghasia, walidaiwa kumshinikiza Katibu Mkuu Yusuf Makamba, kutangaza kwamba zoezi hilo bado halijaanza.

Kwa mazingira hayo, kulingana na baadhi ya wabunge hao wa CCM, hatua hiyo ni makosa kulingana na kanuni za CCM, na kusema kinachofanyika hivi sasa ni kutaka kuharibu mchakato huo ama kwa namna nyingine kuchakachuana.

Mbunge mmoja alisisitiza kwamba dhamira ya Makamba katika suala hilo ni kutaka kuharibu utaratibu, na kuomba Mungu amsamehe, kwani kila kinachofanyika hivi sasa, jamii inatambua kuwa ni hila za kunyimana nafasi ambazo mtu anastahili kuipata.

Hali hiyo, hata hivyo inaonyesha kutokuungwa mkono na kundi la wabunge wa zamani wa CCM pamoja na wale wapya, wakidai kuwa kazi kubwa iliyofanywa na Mhagama ndani ya Bunge lililopita inamfanya mwana mama huyo kukubalika kwa ajili ya nafasi aliyoiomba.

“Hakuna sababu ya kumbeba mtu, kwani Mheshimiwa Job Ndugai aliomba nafasi ya spika na alifanya hivyo baada ya kujipima kwamba anao uwezo wa kuvaa viatu vya Samuel Sitta, sasa mambo yameonekana kwake ni magumu, wameanza kumshawishi kuachana na nafasi hiyo na kushuka chini kidogo,” alisema mmoja wa wabunge wa CCM ambaye hata hivyo aliomba kutotajwa jina.

Mbunge huyo mteule alisema Wana CCM, ndani ya Bunge wapo tayari kuhakikisha Mhagama ambaye ni muombaji pekee wa nafasi hiyo ya naibu spika kupitishwa na kuchaguliwa na wabunge wote kwa kura za ndiyo.

Wakati hayo yakiendelea, baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) wameanza kuwasili mjini hapa huku wakiwa na siri moyoni kuhusu nafasi ya spika mpya wa Bunge.

Hata hivyo, baadhi yao waliozungumza na mwandishi wa habari hizi, wameonyesha msimamo na kumuunga mkono spika aliyemaliza muda wake ambaye pia ni Mbunge wa Urambo Mashariki, Samuel Sitta, wakidai amelifanyia mambo makubwa Bunge na nchi.

Wajumbe hao pia walisema uongozi wa Sitta katika Bunge uliifanya nchi ya Tanzania kupata sifa kimataifa kwa kuwa na Bunge huru na linalotoa fursa za wazi kwa vyama kujenga hoja na kuzichambua kwa nia ya kuhakikisha serikali inafanya mambo kulingana na matakwa ya umma.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge wanaeleza kwamba vita baina ya Chenge na Sitta inaweza kuwa mwisho wa spika huyo wa viwango, ambaye anaweza kuenguliwa na Kamati Kuu ya CCM.

No comments: