Wednesday, November 10, 2010

Chenge si lazima umchafue Sitta

Josephat Isango
HIVI hakuna vigezo vingine au sifa zingine zinazoweza kumtofautisha Chenge na Sitta ili wabunge wajue nani anafaa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?

Hii ndiyo kauli ya Chenge kuwa: “Ni hatari kuendelea kuliacha Bunge liendelee kuongozwa na mtu ambaye ubora wake unapimwa kwa umahiri wake wa kuwapaka matope wengine.”

Kama anajua kuwa Sitta alikuwa anawapaka wenzake matope, yeye angejitofautisha na Samuel Sitta kwa kutojiingiza katika tabia ya kupaka matope ili ajijengee heshima na kuonyesha tofauti? Cha kushangaza, yeye ndiyo kwanza ameanza kwa kumpaka matope mwenzake.

Aliongeza kusema kuwa “wabunge wa chama tawala hawatakiwi kuungana na wale wa upinzani kuikosoa serikali kwa lengo la kutaka kuiangusha au kuonyesha udhaifu kama ilivyokuwa katika Bunge lililopita.” Hapa Chenge anataka kusema kuwa yupo moja kwa moja kwenye mfumo wa kutetea Chama kwanza kuliko maslahi ya taifa!

Kwamba kama serikali iliyopo madarakani ikifanya makosa, basi wabunge wake wasiikosoe, au waikosoe kwa staha, sasa kazi ya wananchi tuliowachagua wawakilishi hawa ilikuwa ni kulinda Chama?

Chenge mwenyewe ana uhakika kuwa si kila wanachama wa CCM ndio waliomchagua ili awe mbunge, iweje aingie bungeni na wazo la kibaguzi kiasi hiki, na sisi tumvulie? Mbona analeta ubaguzi ndani ya Bunge?

Tena anasema “kuwa kinachopaswa kufanywa ni wabunge wa chama tawala kukosoana katika kamati ya wabunge wote wa chama husika na pindi waingiapo bungeni waikosoe serikali kwa staha. wabunge wa chama tawala wanapaswa kuikosoa serikali ya chama chao kulingana na taratibu za kichama, badala ya kuungana na wapinzani.”

Niwaulize wasomaji wangu, kila mtu akiingia na dhana ya kutetea chama chake bungeni, nani atazungumzia masuala ya kitaifa? Chenge ameeleza ukweli kuwa wabunge wa CCM hulinda heshima ya chama badala ya masilahi ya Watanzania.

Nasikitika kwa kuwa ameeleza msimamo huo baada ya uchaguzi, lakini pia sijui kama wabunge nao watakuwa wazembe kufikiri hadi watuchagulie mtu mbaguzi, anayetaka kuingia kwenye uongozi kwa kutukana wenzake.

Chenge anasema, Sitta ni hatari kwa taifa, mbona asiainishe uhatari wake? Atuambie Sitta amewakosea nini watanzania, au yeye si Mtanzania? Na kama ni hatari kwa Tanzania afukuzwe nchini?

Kama Sitta ni hatari kwa CCM imekuwaje yeye Chenge asiwashauri viongozi wa chama hicho tangu mwanzo wakamwondolea uanachama? Na uhatari wa Sitta katika CCM na taifa ulianza lini? Na kwanini ulianza? Na tutapimaje kuwa ni hatari ni kwa maneno ya Chenge tu, ndio tujue kuwa Sitta ni hatari?

Chenge ni mmoja wa vigogo katika Chama Cha Mapinduzi (CCM), kauli anayoitoa kuwa Sitta ni hatari kwa chama je ni msimamo wa chama au msimamo wake ambao pia unaweza kutafsiriwa kuwa ni msimamo wa kukurupuka?

Tukiondoka leo tukamwendea John Chiligati au Makamba na Kikwete mwenyewe, watatoa kauli kuwa Sitta ni hatari kwa taifa au hatari kwa chama kama Chenge alivyosema? Je, wakitoa msimamo tofauti tutachukuliaje kauli ya Chenge? Na kama Sitta ni hatari kwa taifa, mbona kuna maofisa wa Usalama wa Taifa, Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi.

Mbona vyombo hivyo vya usalama havijatoa tamko hili kuwa Samuel Sitta ni hatari kwa taifa letu?

Je, Chenge ametumwa na nani kusema haya? Na ametumwa kwa faida ipi? Na kwanini wakati huu anapotaka kugombea nafasi ya uspika katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?

Chenge kusema Sitta ni hatari kwa Chama Cha Mapinduzi, anadhani Sitta anafaa kuwa chama gani ambacho yeye anaona kuwa kinafaa Sitta ajiunge nacho?

Na je, Chenge tangu lini akawa msemaji wa Chama cha Mapinduzi? Anayo mamlaka yapi yanayomruhusu kuzungumzia maadili ya wanachama mmoja mmoja ndani ya CCM?.

Chenge ametumia utafiti upi? Ametumia vigezo vipi kujua wanachama ambao ni hatari kwa chama na wale ambao sio hatari kwa chama. Je, vigezo alivyotumia kutofautisha wanachama hatari na wale ambao si hatari kama yeye, vinafahamika pia kwa wananchama wengine wa CCM?

Kwamba Sitta ni wa kuogopwa kama Ukimwi, yeye ni wa kuogopwa kama nini mbona hajataja? Kwanini Sitta ameanza kuwa hatari kama ukimwi wakati Chenge anataka kugombea, siku zote wakati Sitta akiwa Spika yeye kama mbunge alimwona Sitta wa kuogopwa? Kama kweli yeye Chenge ni mwenye busara, alitumia nafasi zipi na kauli zipi za wazi kumshauri Sitta kwa “makosa” ambayo Chenge anayaona yanahatarisha taifa na CCM?

Hivi karibuni kulikuwa na kamati iliyoundwa ambayo iliongezewa muda wa mwezi mmoja kusuluhisha migogoro ndani ya CCM na ilikuwa ikiundwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM taifa, Pius Msekwa na mjumbe wa Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho, Abdulrahman Kinana.

Muda haujawa mrefu, mwanachama wa CCM anaibuka na kumwambia mwenzake kuwa ni hatari kwa chama, basi Mwinyi, Msekwa na Kinana hamjafanya chochote, mmezunguka tu, mkatafuna mafao ya chama, mkatoa ripoti kwa Mwenyekiti wenu Kikwete, kumbe mmeacha ufa mkubwa katika chama.

Kama kamati imeacha wanachama wema na wanachama hatari ndani ya zizi moja, walikuwa wanafanya nini? Au hawakujua haya? Na kama walijua walisuluhisha nini?

Hawaoni kuwa ilikuwa ni wajibu wao kutuambia wanachama hatari kwa CCM walikuwa ni fulani na fulani? Wala si kumwachia Chenge kuja kusema? Na walisuluhisha nini? Kama baada ya muda mfupi tu, ndiyo watu wanaanza kuchafuana hadharani kiasi hiki kwa kutafuta madaraka ndani ya chama?

Chenge anajenga hoja kuwa yeye si mtu wa visasi, na yeye si hatari. Kama anavyosema ameamua kuwania uspika kwa kuwa anaamini kuwa ana uwezo wa kutibu majeraha makubwa yaliyoliumiza Bunge na taifa, ambayo yalisababishwa na Sitta, aliyejitafutia umaarufu kwa kuwahujumu, kuwaumiza wenzake na kuwachafua kwa kuanzisha kashfa mbalimbali.

Imekuwaje maneno hayo tuyasikie leo, kutukumbusha vitu ambavyo tulisahau kuwa alishawahi kutuhumiwa kumwaga unga unga ndani ya Bunge? Hii si kulipa kisasi? Kama anaanza kwa kukumbushia vidonda vya Bunge lililopita?

Kinachonishangaza zaidi, kama huu mkakati haukupangwa, imekuwaje na TAKUKURU watoe taarifa za kumsafisha Chenge, siku moja tu baada ya kumchafua Sitta, tena siku chache tu, tangu Chenge atangaze kugombea nafasi hiyo ya juu katika Bunge la jamhuri ya Muungano wa Tanzania?

Dalili nyingi zinaonyesha kuwa kuna kitu zaidi nyuma ya pazia la Chenge kugombea uspika wa Bunge, wananchi Salini ili wabunge wawe kweli wazalendo kutuokoa na janga hili linalotaka kulikumba taifa.

Suala la msingi tukubali kuna tatizo katika sakata hili, na tuwe wakweli katika tatizo hili kwa manufaa ya taifa letu. Vinginevyo, tutaendelea kujiangamiza wenyewe.

Niliwahi kuandika kuwa CCM wana pesa ila hawataweza kununua mwenye akili wa kuwashauri, suala hili ni nyeti sana, na ni mtego mbaya kwa CCM, tusubiri watakavyoweza kuingia mkenge, ili timu iliyoundwa ya Mwinyi, Msekwa na Kinana muone kuwa haikufanya kazi na kama ilifanya, basi walitumia kanuni ya funika kombe mwanaharamu apite. Subirini muone.

No comments: