Wednesday, November 10, 2010

Dk. Shein amteua Maalim Seif kuwa Makaumu

na Hassan Shaaban, Zanzibar




RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, amemteua Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu Zanzibar, uteuzi huo umeanza jana Novemba tisa, mwaka 2010.

Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Abdulhamid Yahya Mzee, katika taarifa hiyo, alisema uteuzi huo ni kwa mujibu wa kifungu cha 39 (1) (2) (3) cha Katiba ya Zanzibar.

Maalim Seif amewahi kushika nyadhifa mbali mbali kabla ya kuanzishwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na ndani ya Chama Cha Mapinduzi.

Miongoni mwa nyadhifa hizo ni Waziri Kiongozi na Waziri wa Elimu, ambapo pia aliwahi kuwa Katibu wa Idara ya Mipango na Uchumi ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM.

Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, amemteua Balozi Seif Ali Idd kuwa Makamu wa Pili wa Rais ambaye kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, atakuwa mtendaji mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa.

Taarifa hiyo ya Ikulu imesema uteuzi huo ulioanza jana ni kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar kifungu cha 39 (1) (2) (6).

Balozi Seif Ali Idd ambaye pia ni Mbunge mteule wa Jimbo la Kitope, alikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika serikali iliyopita ya Rais Kikwete.

Aidha, kabla ya kuingia katika mbio za ubunge, Balozi Idd aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar.

Huo ni uteuzi wa tatu wa Rais Dk. Shein tangu kuingia Ikulu ya Zanzibar, ambapo awali alimteua, Jaji Omar Makungu, kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na kuteua watu wanane kuwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakiwamo viongozi wawili wa CUF.

Katika hatua nyingine, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi jana walifanya kikao chao cha kwanza mjini Zanzibar na kumteua, Pandu Ameir Kificho, kuwa Spika wa Baraza hilo.

Spika Kificho alitangazwa mshindi baada ya kupata kura 45 dhidi ya 32 alizopata mgombea wa CUF, Abbas Juma Muhunzi kati ya kura 78 zilizopigwa ambapo moja iliharibika.

Kificho amekuwa akishikilia wadhifa huo tangu mwaka 1995, ambapo mara baada ya kula kiapo aliwaapisha wajumbe wa Baraza hilo.

Baadaye Spika Kificho aliwapa taarifa wajumbe hao kuwa Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein atalihutubia Baraza hilo kesho.

No comments: