Wednesday, November 17, 2010

Wananchi wamlilia Sitta

na Mwandishi wetu




SAKATA la mchujo wa nafasi ya Spika kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), limewagawa wananchi, huku baadhi wasomi wakitamka wazi kwamba Spika wa Bunge aliyemaliza muda wake, Samuel Sitta, hakutendewa haki.

Wakizungumza na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam jana, baadhi ya wananchi hao walisema Sitta alipaswa kuachwa atetee kiti chake badala ya kuliengua lake katika hatua za awali tena bila sababu za msingi.

Wapo waliosema hatua ya kumuengua Sitta, imebomoa nguzo ya kutetea wanyonge na kumuingia mtu atakayelinda maslahi ya CCM bila kujali maslahi ya taifa kama alivyofanya Sitta.

Katika mahojiano yake, mkazi wa Ilala, Hamad Juma, alisema amebaini kuwa Chenge aliingizwa kwenye kinyang’anyiro hicho kwa ajili ya kuchafua hali ya hewa ili kuhakikisha Sitta hapati tena nafasi hiyo.

“CCM wameamua kumwondoa Sitta mtetezi wa wanyonge na kumleta mtu wao ambaye nina hakika, hataweza kulimudu Bunge lijalo kwani limesheni wasomi, watu makini na uzoefu wa kutosha katika masuala ya siasa,” alisema Hamad.

Naye Joseph Lubojo alisema Chenge aliingizwa kwenye mchezo huo ili kumchafulia Sitta asigombee kwa sababu za kisiasa hasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015.

Naye Dick Malugo, alisema kuwa vita ya Uspika ndani ya chama hicho tawala iliyosababisha Sitta aenguliwe ni mwendelezo wa makundi yaliyotokea mwaka 2005 na yataendelea hadi 2015.

Malugo ambaye ni mwanazuoni wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema mchakato wa uspika umeingia katika sura nyingine ambayo inaonekana baadhi ya wanachama wamelenga kujiimarisha kwa uchaguzi wa 2015.

ka upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake, Ananilia Nkya, alisema kuna haja ya kuhakikisha spika anafanya kazi katika mfumo wa vyama vingi hivyo kuna umuhimu wa kubadili katiba.

“Spika atakayepatikana, ahakikishe katiba inafanyiwa marekebisho ili kuhakikisha mihimili ya dola inafanya kazi katika mfumo wa vyama vingi, hivyo lazima awe refa atakayekuwa anawajibika vema bila kupendelea chama chake,” alisema.

Kwa upande wake, aliyekuwa Mbunge wa Ulanga Magharibi, Dk. Juma Ngasongwa (CCM), alisema uteuzi wa wanawake katika nafasi ya uspika ni wa kihistoria nchini na unapaswa kupongezwa.

Kada mwingine wa CCM, Abdallah Kibunda, alipinga uteuzi huo akisema haukufanywa vizuri kwani umekiuka misingi ya demokrasia.

Naye mtaalamu wa masuala ya Rasilimali watu, Alois Shayo, alipongeza uteuzi huo na kusema nguvu za wanawake kitaalamu haijatumika muda mrefu.

Aliishauri serikali katika uteuzi wake wa nafasi nyingine mbalimbali kutimiza malengo ya milenia ya mgawanyo wa madaraka wa asilimia 50 kwa 50.

No comments: