Wednesday, November 17, 2010

Hamad Rashid alia na Hoseah

na Salehe Mohamed, Dodoma
MKURUGENZI wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dk. Edward Hosea, ametakiwa kujiuzulu wadhifa wake kabla ya kuwajibishwa na Rais Jakaya Kikwete.

Kauli hiyo imetolewa jana mkoani hapa na Mbunge wa Wawi, aliyekuwa Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohamed, (CUF), alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tamko lililotolewa na Ubalozi wa Uingereza juzi kuhusu kashfa ya ununuzi wa rada.

Alisema ni aibu kwa Dk. Hosea na watendaji wake kugeuka wasafishaji wa tuhuma za rushwa zilizofanywa na baadhi ya vigogo wa serikali wakati ukweli hauko hivyo.

Alisema TAKUKURU imegeuka chombo cha kuwatetea wala rushwa, badala ya chombo cha kuwashughulikia, hivyo hakuna sababu kwa Mkurugenzi wa chombo hicho Dk. Hosea na timu yake kuendelea kutumia fedha za walipa kodi kwa masilahi ya watu wachache.

“Dk. Hosea ajiuzulu wadhifa wake la sivyo Rais Kikwete, amfukuze kazi, haiwezekani kila kukicha taasisi hiyo iwe na kazi ya kuwasafisha watuhumiwa wa rushwa, hii ni aibu kwa taifa na serikali,” alisema Hamad.

Alisema TAKUKURU iliwahi kuwasafisha baadhi ya watendaji wa serikali kuwa hawahusiki na kashfa ya utoaji zabuni kwa kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura ya Richmond, lakini baadaye ilikuja kubainika kwamba kulikuwa na mazingira ya rushwa.

Alibainisha kuwa kamati teule iliyoundwa na Bunge kuchunguza zabuni iliyoipa ushindi Richmond, ilibaini kuwepo mazingira ya rushwa katika mkataba huo, jambo lililomfanya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kujiuzulu wadhifa wake na baraza la waziri kuvunjwa.

Alisema inasikitisha kuona TAKUKURU inaendelea na tabia ya kuwasafisha watendaji waliohusishwa na ufisadi ambapo hivi karibuni walitoa taarifa kuwa Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, hana ushahidi unaonyesha alihusika na rushwa katika ununuzi wa rada, ambayo iliigharimu Serikali ya Tanzania zaidi ya sh bilioni 40.

Katika taarifa ya TAKUKURU ilibainisha kuwa Taasisi ya kuchunguza makosa makubwa ya Uingereza (SFO), ambayo ilikuwa ikichunguza ununuzi wa rada hiyo imefunga jalada la uchunguzi na imeshindwa kumhusisha Chenge na rushwa.

Hata hivyo, taarifa iliyotolewa juzi na Ubalozi wa Uingereza ilisema ni mapema mno kuzungumzia kufungwa kwa suala hilo, wakati kesi ikitarajia kufikishwa mahakamani hivi karibuni.

Alisema taarifa ya Ubalozi wa Uingereza, imeiadhiri TAKUKURU na taifa, hivyo hakuna sababu kwa Dk. Hosea kuendelea kushikilia wadhifa wake.

Aliongeza kuwa alishangazwa pia na ujasiri wa Chenge, kutaka kuwania kiti cha uspika wakati akikabiliwa na tuhuma lukuki za ufisadi, ikiwamo hiyo ya rada, ambayo Serikali ya Uingereza imeweka bayana kuwa TAKUKURU hawakusema ukweli.

Aliongeza kuwa TAKUKURU ilionekana kuwa na makali pale ilipoanzisha sheria ya uchaguzi ambapo iliwakamata wagombea kadhaa wa vyama vya siasa, lakini kwa hali ilivyo hivi sasa watendaji wa taasisi hiyo hawapaswi kuendelea na nyadhifa zao.

“Hatuhitaji kuifuta TAKUKURU, bali tunahitaji kuwaachisha kazi watendaji wake ili kuifanya taasisi hii iwe na maana kwa Watanzania kuliko ilivyo hivi sasa, ambapo imekuwa genge la kuwasafisha mafisadi” alisema.

Baadhi ya makada wa CCM waliozungumza na Tanzania Daima kwa masharti ya kutotajwa majina yao, walisema wanashangazwa na hatua ya Rais Kikwete kuendelea kumbeba Dk. Hosea, wakati jamii inafahamu fika kuwa taasisi yake inafanya kazi kwa misingi ya kusafisha kundi la watu fulani.

No comments: