Wednesday, November 17, 2010

Mbowe awa Kiongozi wa Upinzani Bungeni

• CUF wasusia kambi ya upinzani


na Mwandishi wetu
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimemchagua Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, kuwa Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, huku nafasi ya Naibu Msemaji ikienda kwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe.

Uamuzi huo ulitangazwa jana kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma na Mkurugenzi wa Masuala ya Bunge na Halmashauri ya chama hicho, John Mrema, ambaye alisema nafasi ya Waziri Mkuu Kivuli imekwenda kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Alisema utaratibu uliotumika kuwachagua viongozi hao ni wa West Minister Model, ambao unasema kama kiongozi mkubwa wa chama atakuwa mbunge, basi nafasi ya usemaji itachukuliwa naye, huku anayemfuatia kimadaraka akichukua nafasi ya pili.

Mrema alisema CHADEMA imeamua kuunda kambi ya upinzani kutokana na Chama cha Wananchi (CUF) kukataa kujiunga nao na badala yake kuamua kuungana na vyama vya NCCR-Mageuzi na TLP.

Alisema walizungumza na aliyekuwa msemaji wa kambi ya upinzani katika Bunge la tisa, Hamad Rashid Mohamed, ambaye aliwaeleza kuwa CUF haiko tayari kushirikiana na CHADEMA kuunda kambi ya upinzani, ila ipo tayari kuwaunga mkono katika kumsimamisha mgombea wa kiti cha uspika ambaye ni Mabere Marando.

Alisema kulingana na kanuni ya 14 ya Bunge, chama kilichopata asilimia 12.5 ya wabunge ndicho chenye mamlaka ya kuunda kambi ya upinzani na CHADEMA imefikisha wabunge 45, watatu zaidi ya idadi inayotakiwa.

“Tulizunngumza na wenzetu wa CUF, juu ya kushirikiana kuunda kambi ya upinzani, lakini kwa bahati mbaya wametukatalia na kuamua kujiunga na NCCR-Mageuzi na TLP,” alisema Mrema.

Alisema kwa mujibu wa kanuni za Bunge, chama chochote kisichofikisha idadi hiyo, hakina uwezo wa kuunda kambi ya upinzani, hivyo ni vema CUF wakaangalia upya uamuzi wao.

Alisema CHADEMA mpaka sasa haitateua mawaziri kivuli, kwa sababu Rais Jakaya Kikwete hajatangaza baraza la mawaziri.

Alisema pamoja na CHADEMA kuunda kambi ya upinzani, bado haijafunga milango kwa CUF au chama kingine kuungana nao katika kuunda baraza la mawaziri kivuli
“Milango yetu iko wazi kwa CUF na vyama vingine katika kuunda kambi ya upinzani bungeni, nia yetu ni kuifanya kambi hii kuwa imara zaidi na si vinginevyo,” alisema.

Katika hatua nyingine, aliyekuwa msemaji wa kambi ya upinzani katika Bunge lililomaliza muda wake, Hamad Rashid Mohamed (CUF), alisema wameamua kutoshirikiana na CHADEMA kuunda kambi ya upinzani kwa kuwa CHADEMA inajinasibu kuwa inao uwezo wa kuanzisha kambi hiyo bila kuvishirikisha vyama vingine.

Alisema kutokana na msimamo huo wa CHADEMA, CUF imeamua kujiweka pembeni kuangalia upepo wa kisiasa unavyoendelea.

No comments: