Wednesday, November 17, 2010

MBIO ZA USPIKA: Vita Marando, Makinda

• Sitta atoweka viwanja vya Bunge


na Salehe Mohamed, Dodoma




VITA ya kuwania kiti cha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inatarajiwa kufikia tamati leo, wakati mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Anne Makinda, atakapopambana na mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mabere Marando.

Makinda ambaye ni Mbunge wa Njombe Kusini, alipitishwa na chama chake jana, baada kupata kura 211, akiwabwaga wapinzani wake Kate Kamba aliyepata kura 15 na Anna Abdallah aliyepata kura 14.

Wakati hali ikiwa hivyo, CHADEMA imeamua kumsimamisha Marando ambaye ni mmoja wa waasisi wa siasa za mageuzi nchini.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, alisema uamuzi wa kumsimamisha Marando unatokana na uzoefu mkubwa katika masuala ya Bunge na kuwa mmoja wa wanasheria waliobobea katika taaluma hiyo.

Alisema amewahi kuwa mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki na Jimbo la Rorya, ana uhakika wa kuibuka mshindi katika uchaguzi wa leo na kuandika historia mpya.

Naye Marando aliiambia Tanzania Daima jana kuwa ana uhakika wa kuibuka mshindi katika kinyang’anyiro cha leo na kuandika historia mpya.

Naye Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, John Chiligati, alisema mwaka huu CCM inataka kufanya mabadiliko makubwa katika Bunge, kwa kumchagua mwanamke kuwania nafasi hiyo ambayo tangu Tanzania ipate uhuru mwaka 1961, haijawahi kushikiliwa na mwanamke.

Alisema ushindi wa Makinda unaonyesha kukubalika kwa wabunge na ana imani leo ataibuka na ushindi wa kishindo kwa kuwabwaga wagombea wengine wa vyama vya upinzani akiwamo Marando.

“Tuna imani kubwa Makinda ataibuka na ushindi wa kishindo, uzoefu wake na utendaji wa kazi ndivyo vinavyotujengea imani kuwa atakuwa spika bora,” alisema Chiligati.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutoka kwenye ukumbi ya kupigia kura, Makinda alisema anafurahia ushindi huo na atafanya kazi kulingana na kanuni za Bunge ambazo hutungwa na wabunge wote.

Alisema Bunge la mwaka huu lina changamoto kubwa kwa kuwa litakuwa na idadi kubwa ya vijana na wabunge wa kambi ya upinzani lakini hilo halitamfanya atetereke au kupendelea chama fulani kwa sababu Bunge linaendeshwa kwa kanuni.

Alisema wapinzani wanafahamu utendaji wake wa kazi, hivyo wategemee Bunge imara na la kisasa zaidi ambapo hakutakuwa na uminyaji wa hoja za wabunge ili mradi zitolewe kwa kuzingatia kanuni zilizowekwa.

Alisema wabunge wapya wataelimishwa kanuni za Bunge na pindi watakapokosea wataadhibiwa kulingana na kanuni. Alisema kuwa anapenda kuwahakikishia wabunge wapinzani kwamba hatawaminya kutoa maoni yao.

“Nataka kuwa na kipindi cha kutoa elimu kuhusu Bunge, hasa kuzijua kanuni ili mbunge akikosea hata wananchi waweze kujua adhabu itakayomkabili kama ilivyo kwenye mpira, ambapo mtazamaji anaweza kusema ile ni penalti au adhabu ndogo,” alisema Makinda.

Aliongeza kuwa kama kuna upungufu katika maeneo fulani fulani ya kanuni za Bunge, wabunge wanaruhusiwa kufanya mabadiliko kulingana na matakwa yao.

Alibainisha kuwa ni lazima kuwepo kwa uvumilivu katika kutoa na kusikiliza hoja, kinyume na hapo, Bunge halitaweza kuwa na amani, hivyo kukosa imani kwa wananchi.

Wakati huo huo, Spika aliyemaliza muda wake, Samuel Sitta, jana kutwa nzima hakuonekana katika viwanja vya Bunge na wala hakuhudhuria mkutano wa kamati ya wabunge wa CCM, ambao ulikuwa na jukumu la kuchagua jina moja la spika ambalo lingepelekwa kwa Katibu wa Bunge.

Kutoonekana kwa Sitta, kuliwafanya baadhi ya makada wa CCM na wapinzani kudai kuwa huenda amekasirika kwa sababu ya jina lake kutopitishwa kuwania nafasi hiyo, iliyomjengea umaarufu mkubwa ndani na nje ya Bunge.

Sitta alikuwa akikabiliana na upinzani mkali wa maneno na vitendo kutoka kwa baadhi ya makada wa CCM ambao walidai kuwa katika utawala wake alikuwa akiruhusu mijadala mikali ambayo ilikuwa ikitishia uhai wa chama chake na serikali inayoongozwa na chama chake.

No comments: