Wednesday, November 17, 2010

Andrew Chenge hakuutaka uspika

Chacha Kisiri




TAIFA letu liliingia rasmi katika vita dhidi ya matumizi mabaya ya mali za umma mwaka 2007. Kwa mara ya kwanza Orodha ya mafisadi ilisomwa hadharani na mijadala mikali iliyopinga matumizi mabaya ya madaraka ilijadiliwa na kupata uungwaji mkono na baadhi ya wabunge wa CCM waliokuwa tayari kuweka maslahi ya taifa mbele.

Ni wakati huo ambapo wananchi waliokuwa wamechoka na jinsi Bunge lilivyokuwa linaendeshwa walianza kupata imani nalo na kujipa matumaini ya viongozi wetu kuanza kuwajibika kutokana na Bunge kuonyesha makali yake dhidi ya serikali.

Kashfa kubwa ya mkataba wa kinyonyaji wa Richmond ilijadiliwa na kupelekea kuvunjika kwa serikali. Hoja binafsi kuhusu mkataba baina ya serikali na kampuni ya RITES iliyopewa zabuni kuendesha shirika la reli nayo ilisomwa na Mbunge wa Mpanda Mjini, Said Amour Arfi.

Na katika kipindi hicho hicho kwa kupitia vyombo vya habari iliibuliwa kashfa dhidi ya Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge ya kuhifadhi dola za Marekani milioni moja katika akaunti yake binafsi kisiwani Jersey nchini Uingereza.

Ni kashfa hii iliyomwondoa katika baraza la mawaziri kama waziri wa Miundombinu. Baadaye akahusishwa na tuhuma ya kunyunyizia unga ndani ya ukumbi wa Bunge, tukio lililokuja kuhusishwa na ushirikina.

Mwaka huu alipojitokeza kugombea kiti cha uspika, sikusita kulihusisha tukio hili na mkakati maalumu wa kuundiwa zengwe kwa aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta. Chenge kwa kuhusishwa na tuhuma za ushirikina bungeni na kuhujumu uchumi wa nchi akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali alikuwa amepoteza sifa muhimu ya uadilifu kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge hili la sasa.

Baadhi ya watu walidhani Chenge hakuyajua haya na walidhani alisukumwa kwa nia ya dhati kuwa spika. Ukweli ni kwamba Chenge anayo akili timamu. Yote hayo aliyajua.

Kwa staili aliyoingia nayo kwenye kinyang’anyiro cha uspika kwa kurusha makombora dhidi Sitta kwa jinsi alivyoliendesha Bunge lililopita, lengo lilikuwa ni kuikumbusha CCM kwamba ule mpasuko wa wabunge wao uliotokana na kujiuzuru kwa Edward Lowassa bado upo na haujapatipwa ufumbuzi. Na sababu kuu ya mgawanyiko wa wabunge wa CCM kulingana na staili ya kampeni za Chenge ni kuendelea kwa Sitta kukikalia kiti cha uspika.

Tukizisoma vizuri siasa za makundi ndani ya CCM, utagundua kuwa Andrew Chenge, Edward Lowassa na Rostam Aziz ni baadhi ya wanasiasa majeruhi wa uongozi wa Samwel Sitta akiwa Spika wa Bunge.

Rostam na Lowassa walihusishwa na mkataba wa Richmond. Chenge naye akahusishwa na tuhuma za ushirikina ndani ya jengo la Bunge.

Hivyo basi, inawezekana kabisa kujitokeza kwa Kate Kamba, Anna Abdallah na Anne Makinda kulikuwa kwa bahati mbaya au mkakati maalum ulioratibiwa na genge la mafisadi kwa ajili ya kumwadabisha Sitta baada ya mkakati wa awali wa kumpokonya kadi ya uanachama katika moja ya vikao vya Halmashauri Kuu ya CCM mwaka jana kushindwa baada ya kutetewa na Rais Jakaya Kikwete.

Kwa hiyo, kutokana na hasira na chuki zilizokuwa bado vichwani mwa genge hilo, safari hii walidhamiria kufa na Sitta kwa staili ya kukumbushia mgawanyiko wao licha ya kudaiwa kupatiwa ufumbuzi na kamati maalumu ya mzee Mwinyi.

Na kwa kuwa kundi lao lina mtandao mrefu ndani ya vikao vikubwa vya chama, hoja ya jinsia ikaibuliwa lengo likiwa kumchinjia baharini Samwel Sitta. Katika kumbukumbu zangu za mabunge yaliyopita, sikuwahi kuona idadi kubwa ya wanawake wakijitokeza kuwania uspika kama bunge hili.

Ingawa wengine wanaweza kusema kujitokeza kwa wanawake safari hii kunatokana na kukua kwa elimu ya usawa. Nasisitiza bado tutaendelea kuwa na mashaka maana kati ya watatu waliopitishwa, wawili walikuwa wasindikizaji kwa kuangalia kura 29 walizopata wote wawili dhidi ya 211 za mshindi.

Ukweli wa mkakati huu kwamba ulikuwa kwa ajili ya kumng’oa Sitta ulijidhiirisha hadharani mara baada ya Anne Makinda kuchaguliwa rasmi na Bunge kuwa Spika mpya pale Andrew Chenge aliponukuliwa na gazeti la Dar Leo la tarehe 12 mwezi huu akisema ‘uspika sasa ni vipindi viwili’.

Kutokana na kauli hiyo, aiingii akilini ni vipi Chenge yule yule sasa atangaze sera ya vipindi viwili vya uspika wakati alikuwa anampinga spika aliyekaa kipindi kimoja tu. Hapa ndipo inaibuka ile hoja yangu kuwa Chenge si chizi. Ni mtu mwenye akili timamu na alichokuwa anakifanya si kugombea uspika bali kuling’oa jina la Sitta.

Ingawa Anne Makinda ameshakiri kwamba hakutumwa na mtu kugombea uspika, ukweli unabaki kuwa kung’oka kwa Sitta ni hatua nzuri kwa kundi la majeruhi wa vita dhidi ya ufisadi kujipanga vyema kwa kuandaa mtu wao wa kugombea urais mwaka 2015 kwa kumjengea mtandao wenye nguvu ndani na nje ya Bunge.

Na kwa kuwa Sitta alikataa kuurejesha upya mjadala wa Richmond ujadiliwe na Bunge lililopita kabla ya kuvujwa, tusishangae mjadala huo ukarejeshwa kwenye Bunge hili jipya kwa hoja ya kwamba Spika Sitta hakuwa huru na Edward Lowassa muathirika mkuu hakutendewa haki kwa kutopewa fursa ya kuhojiwa na kusikilizwa na kamati ya Mwakyembe.

Ikiwa hili litatokea na tukichukulia jinsi wabunge walivyopiga kura kumchagua Spika wa Bunge hili kwa kuweka itikadi zao za kisiasa mbele zaidi ya maslahi ya taifa tusishangae kuona Lowassa akisafishwa na Bunge hili hivyo kumpatia jeuri ya kugombea urais 2015. Endapo CCM itaona aibu kufanya hivi basi nguvu kubwa itawekezwa kumwandaa mtu mithili ya Andrew Chenge mwenye mahusiano mazuri na mafisadi.

Lakini fundisho kubwa tulilolipata baada ya Sitta kuenguliwa kwenye kinyang’anyiro cha uspika ni kwamba mafisadi bado wapo hai kisiasa na wana nguvu ndani ya CCM na serikali. Wakiamua kitu hakuna wa kuwazuia. Iwe ni kumfukuzisha mtu uanachama au kumvua uongozi kwao ni jambo dogo.

Ni jinsi gani mafisadi wameweza kuwa na nguvu hadi ndani ya serikali ni jambo ambalo linaendelea kutushangaza wengi. Lakini kitendo cha TAKUKURU kumsafisha Chenge dhidi ya mlungura wa rada na kwamba hakuna ushahidi wa kumtia hatiani wakati kitengo cha uchunguzi wa rushwa kubwa cha Uingereza (SFO) kiking’ang’ania kuwa Chenge ana kesi ya kujibu ni ushahidi mwingine wa jinsi mafisadi walivyo na mizizi mirefu hadi kwenye taasisi nyeti za serikali.



Source:Freemedia

No comments: