Wednesday, November 17, 2010

Ujumbe wa Hija kwa Waislamu mwaka 1431 Hijria

Shabani Matutu
IKIWA Waislamu wanafanya ibada yao ya Hija ya mwaka huu wa 1431 Hijria ikiwa ni kukamilisha moja ya nguzo za Kiislamu kwa wale waliojaaliwa kipato.

Katika siku hizi za Hija ambazo zimekuwa na historia ya kipee katika dini ya kiislam kumetolewa ujumbe na kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei.

Ujumbe wake unaanza kwa kusema: Alkaaba ambayo ni nembo ya umoja na heshima ni nembo ya tawhidi na umaanawi, ni mwenyeji wa nyoyo zilizojaa mapenzi na matumaini kutoka kila kona ya dunia ambazo zimeitika mwito wa Mola mlezi katika eneo hilo tukufu ambalo ni chimbuko la Uislamu.

Hivi sasa umma wa Kiislamu unaweza kushuhudia taswira jumla ya ukubwa na upana wa umma huo pamoja na imani yao thabiti ya wafuasi wa dini hii tukufu kupitia wajumbe wa umma huo waliokusanyika Makkah kutoka pembe zote nne za dunia na sasa umeweza kuilewa vyema rasilimali yake hiyo adhimu na kubwa.

Kujitambua huko kupya kunatusaidia sisi Waislamu kuelewa nafasi yetu tunayostahiki kuwa nayo katika dunia ya leo na kesho Akhera na kujibidiisha vyema kuelekea huko.

Kuzidi kuwa kubwa wimbi la mwamko wa Kiislamu katika dunia ya leo ni uhakika ambao unatoa ishara njema ya mustakbali bora kwa umma wa Kiislamu.

Wimbi hilo kubwa la mwamko Kiislamu limeanza katika kipindi hiki cha miaka 30 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuundwa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran, hivi sasa umma wetu mkubwa umekuwa ukipiga hatua za kimaendeleo bila ya kusita, umekuwa ukiondoa vizuizi vyote vinavyojitokeza mbele yake na kufanikiwa kupata ushindi mkubwa. Mbinu za maadui mabeberu zimezidi kuwa tata hivi sasa na wametenga fedha nyingi sana kwa ajili ya kukabiliana na Uislamu.

Adui hufanya propaganda kubwa za kueneza chuki dhidi ya Uislamu, anafanya hila mbalimbali za kuzusha hitilafu na mizozo kati ya makundi ya Kiislamu sambamba na kupalilia taasubu na utesi wa kimadhehebu, kuzusha uadui bandia kati ya Waislamu wa Kishia na Kisuni, kuchochea kitali na ugomvi kati ya tawala za nchi za Waislamu, kujaribu kushadidisha hitilafu na kuzigeuza kuwa uadui usioweza kutatuka, kutumia mashirika ya kijasusi kwa ajili ya kueneza vitendo vya ufisadi na uasherati.

Leo hii, tofauti na miaka 30 iliyopita, utawala wa Kizayuni silo tena lile zimwi lisiloshindika; tofauti na miongo miwili iliyopita, Marekani na Magharibi sio wale wachukuaji wa maamuzi wasio na wapinzani katika Mashariki ya Kati; kinyume na miaka 10 iliyopita, teknolojia ya nyuklia na teknolojia nyinginezo nzito na tata, haziko tena mbali na mikono ya mataifa ya Kiislamu ya eneo hili na wala hazihesabiwi tena kuwa ni kioja.

Leo hii taifa la Palestina ni bingwa wa ‘muqawamah’, taifa la Lebanon peke yake limeweza kuzima haiba na utukufu bandia wa utawala wa Kizayuni kwa kushinda dola hilo katika vita vya siku 33; na taifa la Iran nalo ni mbeba bendera na muongoza njia ya kuelekea kwenye vilele vya mafanikio.

Leo dola la Marekani linalodai kuwa kiongozi wa eneo hili la Kiislamu licha ya kuunga mkono utawala wa Kizayuni, limekwama kutuliza labsha za Afghanistan na Iraq ambako linachukiwa mno.

Kambi iliyo dhidi ya Uislamu ambayo imeyakandamiza kidhulma mataifa na tawala za Kiislamu kwa karne mbili, na kupora utajiri wa mataifa hayo, hivi sasa inashuhudia yenyewe jinsi ushawishi wake unavyozidi kutoweka huku ikikabiliwa na ‘muqawamah’ wa kishujaa kutoka kwa mataifa ya Kiislamu.

Katika upande wa pili harakati ya mwamko wa Kiislamu inazidi kuimarika na kupata nguvu. Mambo hayo yenye kuleta matumaini na kutoa bishara njema, inabidi yatufanye sisi mataifa ya Kiislamu kwa upande mmoja: tuwe na matumaini makubwa zaidi kwamba, mustakabali wetu ni bora, na kwa upande mwingine tupate funzo kutokana na mambo hayo na tuzidi kuwa macho kuliko wakati mwingine wowote.

Mwito huu unaowahusu watu wote, inabidi uwafanye maulamaa wa kidini, viongozi wa kisiasa, wasomi na vijana, wapate nguvu zaidi za kutekeleza inavyopasa majukumu yao, kama ambavyo mwito huu unawataka pia watu wa namna hiyo waongeze jitihada zao na waweko mstari wa mbele wakati wote katika juhudi za kuuletea maendeleo umma wa Kiislamu.

Kitabu kitakatifu cha Qur'ani kilicho hai wakati wote kinabainisha wazi kwamba:
Nyinyi mmekuwa bora ya umma waliotolewa watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamuamini Mwenyezi Mungu. Aal Imran (3:110).

Aya hiyo inautaja umma wa Kiislamu kuwa ni umma wenye heshima bora kuwahi kutolewa kwa ajili ya wanadamu. Lengo la kuletwa umma huu ni kumwokoa mwanaadamu na ni kwa ajili ya kuwatakia kheri watu.

Jukumu kubwa la umma huo nalo, ni kuamrisha mema na kukataza maovu na kuwa na imani thabiti ya Mwenyezi Mungu.

Hakuna jambo bora kabisa kama kuyakomboa mataifa ya wanaadamu kutoka katika makucha ya kishetani ya madola ya kibeberu na hakuna jambo baya na la kuchukiza mno kuliko kuwa kibaraka wa kuwatumikia mabeberu.

Leo hii suala la kulisaidia taifa la Palestina na wakazi waliozingirwa wa Ghaza, kuyahurumia na kuyaunga mkono mataifa ya Afghanistan, Pakistan, Iraq na Kashmir, kusimama kidete na kukabiliana vilivyo na dhuluma ya Marekani na utawala wa Kizayuni, kulinda umoja na mshikamano wa Waislamu na kupambana na mikono michafu na ndimi za vibaraka na mamluki wanaotaka kuvunja umoja wa Waislamu sambamba na kufanyika juhudi maradufu za kueneza mwamko na hisia za kuwajibika kati ya vijana Waislamu katika maeneo yote ya Kiislamu ni majukumu makubwa ambayo inabidi watu wenye ushawishi na muhimu katika ulimwengu wa Kiislamu wayabebe na kuyasimamia vilivyo.

Mandhari tukufu na ya kipekee ya Hija, inatuonyesha njia nyingi na bora za kuweza kutekeleza majukumu hayo na inatutaka tufanye juhudi kubwa zaidi na hima maradufu kwa ajili ya kufanikisha majukumu hayo.

No comments: