Wednesday, November 10, 2010

Tahadhari kwa CHADEMA

Barnabas Lugwisha




BAADA uchaguzi ambao kwa kiwango fulani ninaweza kuuita wenye mafanikio kwa vyama vya upinzani, sasa imebaki taratibu za kibunge ambazo zimeshatangazwa kwa vyombo vya habari na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilia ambazo zitawawezesha wabunge wa upinzani kuanza kazi za kuwawakilisha wapiga kura wao.

Tangu kurudi tena kwa mfumo wa vyama vingi huu ni uchaguzi wa pili wenye mafanikio kwa vyama vya upinzani, baada ya kujizolea takriban viti 30 ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nauita wa pili kwasababu wa kwanza ni ule mwa mwaka 1995 ambao vyamba vya upinzani vilipata wabunge karibu 30, huku NCCR Mageuzi ikiwa na wabunge 16.

Nadhani kwa wakati huo, hayo yalikuwa mafanikio makubwa sana kwa kipindi chote hadi sasa wakati vyama vya upinzani vinaandika historia nyingine ya mafanikio. Mafanikio haya pamoja na mustakabali wake ndiyo mada yangu ya leo.

Mada yangu ya leo ambayo kwayo ni nasaha kwa vyama vya upinzani ambavyo zamu hii kama vitajidhalilisha kama ilivyokuwa mwaka 1995 na kuendelea vitapotea ndani ya mioyo ya Watanzania kwa kipindi kirefu sana na kukipa Chama Cha Mapinduzi nafasi ya ukiritimba na kujisahau tena.

Wakati ule, Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema, alikuwa juu sana, nadhani hii haina haja ya kuizungumza sana wengi wetu tunakumbuka, lakini tunakumbuka namna ambavyo wakubwa wa Chama cha NCCR Mageuzi walivyorushiana viti pale Tanga, wakawa watu wa ajabu kabisa, wakagombania ruzuku badala ya hoja bungeni, kumbukeni baada ya miaka 15 kupita Watanzania wamewaamini tena.

Leo naizungumzia CHADEMA, ndiyo chama kikuu cha upinzani kwa Tanzania Bara, kimezoa wabunge 24, hii ni rekodi mpya kwa siasa za Tanzania Bara kwa chama cha upinzani kupata viti vingi kiasi hicho, hii ni imani ambayo Watanzania wameionyesha kwenu, wajibu wenu ni kuilinda na kuiheshimu imani hiyo.

Kwa maoni yangu, msidhani kwamba CCM wamefurahi, kama ilivyo historia ya CCM ya kuhodhi madaraka ya nchi hii, iwe ndani ya Bunge ama nje, watatafuta njia ya kuwavuta shati.

Ili mdhoofike na muonekane kuwa ni chama legelege ambacho kama kingepewa dola basi nchi ingekuwa mahala pabaya, si kwa Tanzania tu, ni karibu kote Afrika, serikali za vyama tawala hupandikiza mamluki ndani ya vyama vya upinzani ili kuleta migogoro (conflicts).

Neno migogoro lina maana pana sana, inaweza ikawa migogoro ya kisiasa, dini, ardhi na mingine. Kwa Kiingereza neno conflicts linasomeka ‘conflict is actual or perceived opposition of needs, values and interests.

‘A conflict can be internal (within oneself) to individuals. ...au conflict - an open clash between two opposing groups (or individuals)’, kwa tafsiri isiyo rasmi ni tofauti za ki - mawazo, mtazamo baina ya pande mbili.

Sasa kwa vyama vya siasa, conflicts kama ilivyokuwa kwa NNCR Mageuzi wakati ule ilikuwa ni tofauti kati ya mwenyekiti wa taifa na katibu mkuu wa chama hicho. Tofauti ambayo ilileta mgawanyiko na makundi makubwa mawili ndani ya chama ambayo yalisababisha chama kugawanyika na hatimaye kudhoofika na kuwa chama dhaifu kabisa.

Chama kilikuwa na makao makuu sehemu mbili tofauti, japo walikuwa wakikutana pale kwa Msajili wa Vyama Vya Siasa kila mmoja kudai ruzuku.

Kwa kweli hata mimi nilishindwa kumtambua nani mwenye haki, ukikaa na Mrema atakwambia Mabere Marando (Katibu Mkuu) hafai, kadhalika ukiwa na Marando atakwambia Mrema ana matatizo, ilimradi tu, kwetu sisi wananchi ilikuwa kero.

Kilichotokea ni CCM kupata nguvu, na kuwabeza wapinzani kwamba kama wangepewa dola kipindi hicho nchi ingesambaratika.

Ukiangalia kwa ujinga ule ni kweli nchi ingesambaratika, hapo ndipo CCM ilipoonekana mbele ya wapiga kura kuwa ni chama imara na chenye kujiheshimu, ingawa sasa hali taratibu imeanza kubadilika.

Kutokana na mfano huo, nachukua fursa hii kuitahadharisha CHADEMA kwamba Watanzania wengi wanaiangalia kwa makini, wameipa kura nyingi za udiwani, ubunge na urais, ujinga ule wa NCCR Mageuzi usikaribishwe hata kidogo, uogopwe kama ukoma.

Kwa uelewa wangu kuna aina mbili za wanachama ambao wanaweza kuleta vurugu ndani ya CHADEMA, aina ya kwanza ni wale wanachama wa muda mrefu ambao wakipenyezewa rupia kutoka upande mwingine wanaweza kuwa chanzo cha migogoro, wengine ni wale watakaopandikizwa.

Watu hao wanajulikanaje? Kwanza kwa kiherehere, utawakuta kila kitu wanataka wao ndio wawe wa kwanza katika kila jambo, bila hata kuwashirikisha viongozi wao, uchu wa madaraka, kutoa siri za vikao vya chama, kujipendekeza kwa chama tawala na mengine yenye tabia za kizandiki za aina hiyo.

Ushauri wangu kwa chama dhidi ya watu hao ni rahisi, akithibitika mwanachama au kiongozi kuwa ni mamluki wa watu wa nje, basi chama kimchukulie hatua kali za kinidhamu ikiwemo kumtimua.

Ni matumaini yangu kwamba CHADEMA itaendelea kuwa ni chama aminifu cha upinzani kwa Watanzania ambacho kitatetea masilahi yao ndani ya Bunge.

Kitakuwa ni chama ambacho kitaendelea kukua kila kukicha na kuwakilisha mawazo ya wapiga kura wake ndani ya vikao vya Bunge.

Kitakuwa ni chama chenye wabunge wenye nidhamu na wanaoheshimu katiba yao, viongozi wao na kitakuwa ni chama chenye wabunge wanaoweka mbele masilahi ya chama na si vinginevyo.

No comments: