Wednesday, November 17, 2010

Pinda: CHADEMA wamenuna

• Aahidi kuwatendea haki wabunge waliomkataa


na Salehe Mohamed, Dodoma
HATIMAYE kitendawili cha nani atakuwa Waziri Mkuu, kimeteguliwa kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuidhinishwa tena na Bunge kushikilia wadhifa huo.

Muda mfupi baada ya wabunge kumuidhinisha kuwa spika kwa njia ya kura, Pinda alieleza kuguswa na kile alichokieleza kuwa ni hatua ya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ya kumnunia hata kufikia hatua ya kutompigia makofi ya kumuunga mkono.

Hata hivyo, pamoja na hatua hiyo ya baadhi ya wabunge kuonyesha kutomuunga mkono, aliahidi kufanya kazi na wabunge wote katika hali ya kutowabagua.

“Nawashukuru kwa kuniidhinisha ingawa wengine walinikataa, sitamchukia Mbowe, Khalifa, nitafanya kazi na wote,” alisema Pinda wakati akitoa hotuba ya shukrani kwa wabunge.

Uchaguzi wa kumuidhinisha Pinda ulifanyika jana bungeni baada ya Rais Jakaya Kikwete kumpelekea Spika wa Bunge, Anne Makinda, jina hilo ili lisomwe na baadaye liidhinishwe na Bunge.

Katika uchaguzi huo, Bunge lilimuidhinisha Pinda kuwa Waziri Mkuu mteule baada ya kiongozi huyo kupata kura 277 zilizopigwa na wabunge 328, sawa na asilimia 84.5, ambapo kura 49 (asilimia 14.9) zilimkataa na mbili ziliharibika.

Kuchaguliwa kwa Pinda kuwa Waziri Mkuu kunamaliza tetesi za vigogo wa CCM waliokuwa wakitajwa kuteuliwa kushika wadhifa huo.

Miongoni mwa majina yaliyokuwa yakitajwa kuteuliwa kwenye nafasi hiyo ni aliyekuwa Spika wa Bunge lililopita, Samuel Sitta, aliyekuwa Waziri na Uvuvi na Mifugo, John Magufuli na Mizengo Pinda.

Awali kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo, Spika Makinda alisema kanuni ya 25 (1 na 2), inasema baada ya kuapishwa kwa spika na wabunge, rais atapeleka bungeni jina la mbunge aliyemteua kuwa waziri mkuu na baadaye Bunge litamuidhinisha.

Kabla ya kuanza kwa uchaguzi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema, alisema kwa mujibu wa ibara ya 51 (a) ya mwaka 1977, Rais wa Jamhuri ya Muungano atateua jina moja la mbunge na kulipeleka kwa Spika wa Bunge ili liidhinishwe na wabunge.

Werema alimmwagia sifa Pinda kuwa ni mchapakazi, muadilifu, msikivu, asiye na makuu, mwenye busara na mchambuaji wa kina wa hoja, hivyo anafaa kupata nafasi hiyo.

Baada ya mchakato wa uchaguzi kufanyika na Pinda alipata nafasi ya kuwashukuru wabunge kwa kumchagua, alisema atafanya kazi na wabunge wote bila kujali itikadi za vyama vyao.

Alisema kuwa anamshukuru Rais Kikwete kwa kumteua kuwa waziri mkuu, na hiyo inaonyesha kuwa kazi aliyoifanya kwa miaka miwili na nusu ilikuwa ya kuridhisha na kumjengea imani kwa rais na Watanzania wote.

Pinda alisema kuwa ana matumaini katika miaka mitano ijayo wabunge watajikita katika kufanya mabadiliko ya sheria pamoja na kuandaa mipango itakayomsaidia mwananchi wa kawaida wa vijijini ambaye anakabiliwa na umaskini mkubwa.

Alibainisha kuwa vijijini ndiko kwenye umaskini mkubwa, hivyo ni vema wabunge wakajikita kutatua matatizo ya wananchi kuliko kutumia muda mwingi kufanya malumbano yasiyo na tija kwa wananchi.

Aliongeza kuwa matatizo ya wananchi hayataweza kupata ufumbuzi kama wabunge hawatakuwa na hasira za matatizo yanayowakabili wananchi na kuyatafutia ufumbuzi.

Alibainisha kuwa wakulima, wafugaji na wavuvi wanapaswa wasaidiwe kuyafikia maisha bora ambayo yanahitaji maandalizi na ushirikiano mkubwa wa viongozi na wananchi.

Pinda pia hakusita kummwagia sifa Spika wa Bunge, Anne Makinda, kwa uchapakazi aliouonyesha kwenye Bunge lililopita na kusema kuwa ana imani nafasi ya spika anaiweza na ataifanya kwa ufanisi mkubwa.

Aliongeza kuwa Spika wa Bunge la tisa, Samuel Sitta, amefanya kazi kubwa kwa kuruhusu hoja huru za wabunge ambazo zimesaidia kuimarisha demokrasia.

“Kaka yangu Sitta, alinisaidia sana hasa kwa nyakati ambazo mambo yalikuwa magumu, nashukuru tulimaliza salama, nina imani busara zake tutaendelea kuzitumia kwa sababu bado tunaye humu ndani,” alisema.

Sitta pia alipata sifa kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema, ambaye alisema kuwa uongozi wa Sitta ulichangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko kadhaa.

Wakati huo huo, Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai (CCM) amefanikiwa kuwa Naibu Spika baada ya kumshinda Mbunge wa Mbulu, Mustafa Akunaay (CHADEMA), aliyekuwa akiwania kiti hicho. Ndugai alipata kura 276 dhidi ya 46 za Akunaay, huku kura sita zikiharibika.

Nafasi hiyo pia ilikuwa ikiwaniwa na Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mnyaa (CUF), aliyeamua kujitoa kwa madai kuwa nguvu zake anazielekeza kwenye uchaguzi wa uwakilishi wa Bunge la nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Nafasi ya Naibu Spika katika Bunge la tisa ilikuwa ikishikiliwa na Spika Anne Makinda, ambaye mwaka huu aliamua kuwania uspika na alifanikiwa kuchaguliwa kwa kura 265, akimshinda mgombea wa CHADEMA, Mabere Marando, aliyepata kura 53.

No comments: