Saturday, November 27, 2010

JK ateua mawaziri 50

• Wamo mzee wa kasi na viwango, Mwakyembe, Magufuli


na Kulwa Karedia




HATIMAYE Rais Jakaya Kikwete ametangaza Baraza la Mawaziri lenye jumla ya mawaziri 50, huku akifanya mabadiliko ya muundo wa wizara mbalimbali kwa kile alichokiita ‘kurahisisha ufanisi wa utendaji kazi’ wa serikali yake.

Katika idadi hiyo, mawaziri kamili ni 29 na manaibu waziri 21.

Baraza hilo limezidi ukubwa wa baraza lililopita kwa tofauti ya mawaziri watatu, kwani Rais Kikwete alimaliza awamu yake ya kwanza akiwa na baraza lenye jumla ya mawaziri 47.

Hatua hiyo imekwenda kinyume kabisa na kilio cha aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, aliyelalamikia ukubwa wa baraza la mawaziri kuwa unasababisha serikali kuendeshwa kwa gharama kubwa badala ya kubana matumizi kwa maendeleo ya wananchi.

Dk. Slaa kama angetangazwa kuwa rais alikusudia kubana matumizi na kuunda serikali yenye baraza dogo la mawaziri wasiozidi 15 ili kuwa na fedha nyingi za kusukuma maendeleo ya wananchi.

Akizungumzia mabadiliko ya baraza hilo mbele ya waandishi wa habari Ikulu jijini Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisema amefanya mabadiliko katika Ofisi ya Rais ambayo sasa itakuwa na mawaziri wawili.

Aliwataja mawaziri hao kuwa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utawala Bora, Mathias Chikawe na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, ambayo itaongozwa na Steven Wassira.

Katika mabadiliko hayo, Rais Kikwete alitangaza kuigawa iliyokuwa wizara ya miundombinu na kupata wizara mbili; Wizara ya Ujenzi itakayoshughulikia masuala ya barabara na viwanja vya ndege na Wizara ya Uchukuzi.

Wizara ya Ujenzi itaongozwa na Waziri John Magufuli na Naibu Waziri, Dk. Harrison Mwakyembe, huku Wizara ya Uchukuzi ikiongozwa na Waziri Omar Nundu, atakayesaidiwa na manaibu waziri wawili, ambao ni Athuman Mfutakamba na Lazaro Nyalandu.

Katika baraza hilo, Rais Kikwete amewaacha baadhi ya mawaziri waandamizi ambao ni aliyekuwa Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya, aliyekuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kapteni John Chiligati na aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Margaret Sitta.

Pia Rais Kikwete amewaacha aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Jeremia Sumary na aliyekuwa Naibu Waziri wa Miundombinu, Ezekiah Chibulunje.

Katika mabadiliko hayo, Rais Kikwete ameongeza mawaziri wawili katika Ofisi ya Makamu wa Rais, ambapo Samia Suluhu atashughulikia Muungano, wakati Dk. Terezya Hovisa, atashughulikia Mazingira.

Katika uundaji huo, Rais Kikwete amemteua Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), huku Dk. Mary Nagu akiteuliwa kuwa Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji.

Katika sura hizo mpya yumo aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watu na makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ambaye ametangazwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, akisaidiwa na Naibu Waziri, Goodluck ole Madeye.

Aliyekuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Samuel Sitta, ameteuliwa kuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, akisaidiwa na Naibu Waziri Dk. Abdallah Juma Abdallah.

Rais ameongeza wizara mpya katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ambayo itaongozwa na Waziri George Mkuchika, atakayesaidiwa na manaibu waziri wawili, ambao ni Aggrey Mwanri na Kassim Majaliwa.

Wizara ya Fedha itaendelea kuongozwa na Mustapha Mkulo akisaidiwa na manaibu waziri, Gregori Teu na Pereira Ame Silima.

Alisema Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi itaongozwa na Shamusi Vuai Nahodha, akisaidiwa na Balozi Khamis Kaghasheki, wakati Wizara ya Katiba na Sheria itaongozwa na Celina Kombani.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa itaendelea kuongozwa na Waziri Bernard Membe, Naibu wake ni Mahadhi Juma Mahadhi, wakati Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa itaendelea kuongozwa na Dk. Hussein Mwinyi, huku akifuta nafasi ya naibu waziri.

Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi itaongozwa na Waziri Dk. Mathayo David Mathayo na Naibu wake ni Benedict ole Nangoro, wakati Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia itaongozwa na Waziri Profesa Makame Mnyaa Mbawala na Naibu wake ni Charles Kitwanga.

Rais amewapandisha vyeo aliyekuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige kuwa waziri kamili wa wizara hiyo, huku aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami, akipewa uwaziri kamili wa wizara hiyo. Dk. Shukuru Kawambwa anakuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Naibu wake ni Philip Mulugo.

Katika uteuzi huo, Rais Kikwete amemteua Dk. Hajji Hussein Mpanda kuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, wakati Naibu wake ni Dk. Lucy Nkya.

Wizara ya Kazi na Ajira itaongozwa na Waziri Gaudensia Kabaka na Naibu wake ni Dk. Makongoro Mahanga, huku Wizara ya Habari, Vijana na Michezo, ikiongozwa na Emmanuel Nchimbi, akisaidiwa na Fenella Mukangara.

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto itaongozwa na Waziri Sophia Simba, akisaidiwa na Naibu Waziri, Umi Ali Mwalimu.

Profesa Jumanne Maghembe aliyekuwa Waziri wa Elimu, safari hii ameteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, akisaidiwa na Naibu Waziri Injinia Christopher Chiza, huku akimteua, Profesa Mark Mwandosya kuwa Waziri wa Maji na Naibu Waziri wake ni Injinia Gerson Lwinge.

Wizara ya Nishati na Madini itaendelea kuongozwa na William Ngeleja na Naibu wake ni Adam Malima.

Baada ya uteuzi huo, Ofisi ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, imesema shughuli ya kuapishwa mawaziri hao itafanyika siku ya Jumamosi saa 5 asubuhi, huku mawaziri hao wateule wakisisitizwa kufika Ikulu majira ya saa 3 asubuhi kwa ajili ya kukamilisha taratibu mbalimbali zinazohitajika.

No comments: