Saturday, November 27, 2010

Lowassa: Nimechoka kuzushiwa

• Mwanaye ajipanga kuchukua hatua za kisheria kujisafisha


na Mwandishi wetu




WAZIRI Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, ameeleza kushangazwa na mwenendo wa kisiasa wa siku za hivi karibuni ambao unaliingiza jina lake katika matukio makubwa ya kisiasa yanayotokea.
Mbali ya kueleza mshangao wake huo, Lowassa alikwenda mbele zaidi na kusema alikuwa amefikia hatua ya kuchoshwa na aina ya siasa zinazomhusisha na mambo yasiyo na ukweli wowote.

“Nimechoka kukaa kimya kila mara zinapotengenezwa habari za uongo juu yangu. Imefika mahali sasa nimeamua kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wale ambao kwa makusudi na kwa nia mbaya wanafinyanga uzushi dhidi yangu na wakati mwingine dhidi ya familia yangu,” alisema Lowassa aliyezungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana.

Akitoa mfano, Lowassa ambaye alitafutwa ili kutoa maoni yake kuhusu muundo wa baraza jipya la mawaziri lililotangazwa hivi karibuni, alieleza kushangazwa na uamuzi wa baadhi ya watu kufikia hatua ya kumtuhumu kwamba alikuwa akishinikiza ateuliwe katika nafasi kadhaa za uwaziri jambo ambalo halina ukweli wowote.

“Rais anaunda baraza la mawaziri kwa utashi wake na si kwa kushinikizwa na mtu yeyote. Jambo la kushangaza imefikia watu wanasema uongo wa wazi kwamba eti Lowassa alikuwa akishinikiza na wengine wakafikia hatua ya kudai kulikuwa na msukumo mkubwa wa kutaka niteuliwe. Huu wote ni uzushi,” alisema Lowassa.

Alisema ni jambo la ajabu kwamba jina lake ndilo linaloonekana kuwa katikati ya mjadala wa uteuzi huo wakati kila mmoja akijua kuwa wako mawaziri wakuu wastaafu wengine ambao wangeweza kuteuliwa katika nafasi za ubunge na uwaziri ambao hawakuteuliwa ingawa majina yao hayatajwi.

Ingawa Lowassa hakutaja jina la mtu yeyote, mawaziri wakuu wastaafu ambao wapo ni Frederick Sumaye, John Malecela, Joseph Warioba, Cleopa Msuya na Salim Ahmed Salim.

Ukimuacha Malecela ambaye alionyesha dhamira ya kuendelea kuwa bungeni kabla ya kushindwa katika mchakato wa kura za maoni ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), mawaziri wakuu wastaafu wengine wote wako nje ya wigo wa siasa za mikikimikiki.

Kwa sababu hiyo, mwanasiasa huyo alieleza kusikitishwa na hatua ya watu aliowaita wachimvi waliofikia hatua ya kukielezea kitendo cha rais kutomteua katika nafasi yoyote ya uwaziri kuwa ni cha kumtosa kisiasa.

“Mimi ni mbunge wa Monduli kwa tiketi ya CCM, ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, bado ninazo fursa nyingi za kuendelea kutoa mchango wangu wa kisiasa kwa chama changu na kwa taifa langu kwa njia nyingi.

Nafasi za uongozi nilizonazo zimetokana na ridhaa ya chama changu. Haiingii akilini kusema nimetoswa au nimefikia ukomo wa kisiasa,” alisema Lowassa kwa masikitiko.

Alisema iwapo Kikwete au CCM wangekuwa wamemtosa kisiasa, basi jina lake lisingeweza kupitishwa kugombea ubunge, kwani rais ndiye mwenyekiti wa taifa wa chama hicho.

Mbali ya hilo, Lowassa alisema, watu wasiomtakia mema, ambao hata hivyo hakuwataja, wamefikia hatua ya kuanza kuipaka matope hata familia yake katika mambo ambayo si ya kweli.

Lowassa alikuwa akizungumzia habari zilizomhusisha mtoto wake Frederick Lowassa katika tuhuma za kuchunguzwa na taasisi za ndani ya nchi na zile za nchini Uingereza kwa madai ya kusafirisha fedha nje ya nchi katika mazingira yenye utata.

Habari hizo zilizoandikwa katika gazeti moja linalochapishwa mara moja kwa wiki, zilimhusisha Frederick na ununuzi wa nyumba yenye thamani ya pauni za Uingereza 475,000 (takriban shilingi bilioni moja) ambayo inatajwa katika maelezo ya awali iko mtaa wa Leinster Gardens, jijini London.

“Habari hizo zinazomhusu Frederick na ambazo zililitaja pia jina langu hazina ukweli wowote. Nimechoka kuzushiwa na kushambuliwa kwa mambo ambayo si ya kweli. Nimekuwa kimya na sasa wameanza kuichafua hata familia yangu.

“Nimewasiliana na Frederick mwenyewe ambaye amenihakikishia kuwa tayari ameshaanza kuchukua hatua za kulifikisha suala hilo mbele ya vyombo vya kimaadili na kisheria kama Baraza la Habari Tanzania (MCT) na mahakamani ili kulisafisha jina lake,” alisema Lowassa.

No comments: