Wednesday, November 17, 2010

Lissu, Mnyika wamtikisa Spika

na Mwandishi wetu, Dodoma




WABUNGE machachari wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu (Singida Mashariki) na John Mnyika (Ubungo), jana walianza kumpa wakati mgumu Spika wa Bunge, Anne Makinda, kwa kumbana kwenye kanuni kwa kutaka awape ufafanuzi.

Akizungumza kwa kujiamini, Mnyika alikuwa wa kwanza kutaka mwongozo wa Spika, kwa kutaja kanuni ya 68 (7) ya Bunge inayozungumzia usiri wa kura lakini katika karatasi walizotoa kwa ajili ya kupiga kura za kuidhinisha jina la waziri mkuu zilikuwa na namba.

Mnyika alisema uwepo wa namba hizo kunaweza kumfanya mtu kujua nani alipewa karatasi namba ngapi na kura aliyopiga ili kumkubali au kumkataa mtu Fulani, hivyo hakutakuwa na usiri tena.

“Mimi nimepata karatasi yenye namba 278, hivyo ni rahisi mtu kujua kura yangu nilimkataa au kumkubali mgombea, hapa siri haitakuwapo, naomba mwongozo wako,” alisema.

Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisema ni kweli kuwapo kwa namba hizo kunaweza kuathiri zoezi hilo lakini kwa sababu awali hakuna mtu aliyekuwa anajua jina la waziri mkuu mteule, uwepo wa namba hizo si tatizo, kwani umefanywa na mashine.

Alisema jina la yeyote lingeweza kuteuliwa na Rais Kikwete, hivyo Bunge lingefahamu jina hilo baada ya bahasha iliyoletwa na Rais kufunguliwa bungeni.

Lissu, naye alimbana Makinda kwa kutumia kanuni 53 (6)a, (6)c ambapo alisema endapo hoja itatolewa na serikali bila kupitia katika Kamati ya Kudumu ya Bunge, kiongozi wa upinzani bungeni atapata fursa ya kujadili hoja lakini Bunge halikufanya hivyo baada ya hoja ya kumuidhinisha Waziri Mkuu kutolewa.

Kabla ya kutoa mwongozo huo, Makinda, alitaka uchaguzi uendelee na kura zihesabibiwe, jambo lililozusha mzozo wa pande mbili (wabunge wa CCM na wale wa CHADEMA).

Hata hivyo swali hilo lilionekana kuwaumiza vichwa wanasiasa wengi, ambapo Spika wa Bunge la tisa Samuel Sitta, alilazimika kunyanyuka kwenye kiti chake na kwenda kwenye kiti cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuteta naye, huku akiwa na kitabu cha kanuni za Bunge.

Wakati Sitta akifanya hivyo, Ukumbi wa Bunge ulilipuka kwa shangwe za kumshangilia, jambo lililomfanya Makinda kusema kuwa angalau amelichangamsha Bunge kwa kuwa lilikuwa kimya kwa muda kidogo.

Wakati hayo yakitendeka, Makinda naye alikuwa akipokea ujumbe wa baadhi ya wabunge ulioonekana kumsaidia namna ya kutoa mwongozo kwa wabunge hao wa CHADEMA.

Baada ya matokeo ya uchaguzi kurejeshwa kutoka kwenye chumba yalikokuwa yakihesabiwa, Makinda alitolea ufafanuzi jambo hilo, ambapo alisema kuwa aliruhusu hoja hiyo kujadiliwa ambapo wa kwanza kuijadili alikuwa ni Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela.

Alisema baada ya Kilango kutoa mchango wake, alitoa hoja ya kutaka hoja hiyo isijadiliwe na kuungwa mkono na wabunge zaidi ya 10, hivyo hakukuwa na haja ya kumpa nafasi Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni.

Alisema kwa mujibu wa kanuni, hoja ikiungwa mkono na wabunge zaidi ya 10 haina haja ya kuendelea kujadiliwa, ndiyo maana hoja hiyo ilifungwa.

Aidha, alisema hoja yoyote iliyoamuliwa na wabunge na Spika akiifunga, hakuna mbunge atakayeruhusiwa kuizungumzia tena.

Baada ya maelezo hayo ambayo yalionekana kupingwa na wabunge wengi, hasa wa CHADEMA, Naibu Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Zitto Kabwe, alisimama kutaka kuuliza swali, lakini Makinda alimnyima nafasi na kuendelea na utaratibu wa kuhesabu kura.

Katika hatua nyingine Lissu, aliteuliwa kuwa msimamizi wa zoezi la kuhesabu kura za kumuidhinisha waziri mkuu, jambo ambalo lilizusha shangwe na makofi mengi kutoka kwa wabunge wa CCM.

Shangwe hizo zilitokana na msimamo uliotolewa juzi na CHADEMA wa kutomtambua Rais Kikwete kwa madai kuwa matokeo yaliyompa ushindi yalikuwa ya wizi.

Wabunge wa CCM na watu wengi walitaka kuona kama Lissu atakataa kwenda kuhesabu kura kwa sababu jina la waziri mkuu, lilipendekezwa na Rais Kikwete ambaye CHADEMA haimtambui.

Hata hivyo Lissu alionekana akijadiliana jambo na viongozi wenzake na baadaye aliinuka kwenda kwenye zoezi hilo huku akishangiliwa na wabunge.

Pinda anatarajiwa kuapishwa kesho katika Ikulu ndogo ya Chamwino mjini hapa.

No comments: