Friday, October 29, 2010

Wananchi watakiwa kusikiliza sera za CHADEMA

na Stephano Mango, Songea
WANANCHI wametakiwa kuwa makini katika kuzisikiliza sera na ilani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ili waweze kuchukua hatua stahiki katika Uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge na urais unaotarajiwa kufanyika nchini kote Jumapili, Oktoba 31 mwaka huu.
Wito huo ulitolewa jana na mgombea ubunge wa jimbo la Songea Mjini kupitia chama hicho, Edson Mbogoro, kwenye mikutano yake miwili ya kampeni aliyoifanya kwenye Kata ya Majengo.

Mbogoro alisema Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ndicho chama imara ambacho kimesimamisha wagombea wanaokubalika na wenye uwezo mkubwa wa kuielezea na kuitekeleza kwa kivitendo ilani yake ya uchaguzi.

Alisema muda uliobaki unawatosha wananchi kutafakari kwa umakini na kuchukua hatua madhubuti ya kuwachagua wagombea wa CHADEMA ili wawe viongozi katika nafasi za ubunge, udiwani na urais kwa maslahi ya Watanzania wote.

Alisema Chedema ndicho chama chenye dhamira ya kweli ya kuwakomboa Watanzania wote katika lindi la umasikini, ujinga na maradhi hivyo wananchi kuweni makini sana na uchaguzi huu.

Alisema kuwa wapiga kura wanatakiwa kuwa makini katika kuwatambua wagombea ambao watakuwa na uwezo wa kusema na kutenda mara watakapochaguliwa hivyo ni vyema kufahamu sifa na matendo ya kila mgombea ili siku ya uchaguzi waweze kufanya maamuzi sahihi.

Mgombea huyo wa ubunge ambaye kitaaluma ni mwanasheria ambaye anafanya shughuli zake za uwakili chini ya Kampuni ya Mbogoro Advocates mjini hapa, pia ni mjumbe wa mkutano mkuu wa CHADEMA.

Alisema uchaguzi wa mwaka huu ni wa muhimu sana kwani ni uchaguzi wa kuwakataa kikamilifu wagombea mafisadi, walaghai na watoa rushwa hivyo wananchi mnawajibika kuwachagua viongozi wenye uadilifu mkubwa ambapo wagombea hao wanapatikana katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo.

Alisema kura ya ina thamani kubwa sana katika maisha ya mwananchi na iwapo wataipoteza kwa kuchagua kiongozi kwa ushabiki wajue wamepoteza fursa ya kupata barabara, maji, hospitali na huduma nyinginezo za kijamii.

Aliongeza kuwa CCM imeshindwa kuwakomboa Watanzania katika lindi la umaskini, maradhi na ujinga, hivyo uchaguzi huu ni vema Watanzania wakaacha ushabiki usio na faida ambao mwisho wa siku ni kuongezeka kwa ugumu wa maisha.

No comments: