Friday, October 29, 2010

Papic kiti moto Yanga

• Wachezaji nao kuhojiwa kulikoni


na Juma Kasesa




MWENDO wa kusuasua wa timu ya Yanga katika Ligi Kuu Bara, umemweka kwenye wakati mgumu Kocha Mkuu wa timu hiyo, Kostadin Papic.

Sare tatu ambazo Yanga imevuna baada ya kumfunga mtani wake Simba Oktoba 16, zimewatia shaka viongozi, wanachama na wapenzi wa klabu hiyo.

Tangu Yanga iifunge Simba, imeambulia pointi tatu katika mechi dhidi ya JKT Ruvu, Azam FC na Lyon, hivyo kufikisha pointi 22.

Kwa pointi hizo, Yanga inakamata nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu iliyoanza Agosti 21 ikiwa na pointi 22 huku Simba ikiongoza kwa pointi 24.

Katika hali ya kusaka kiini cha hali hiyo, viongozi wa Yanga leo wamepanga kukutana na Papic ambapo pamoja na mambo mengine, kujadili kiini cha timu kufanya vibaya.

Kikao hicho kinafanyika siku moja baada ya Yanga kutoka sare ya bao 1-1 na African Lyon kwenye Uwanja wa Jamuhuri, mjini Morogoro.

Mwenyekiti wa klabu hiyo, Llyod Nchunga, alisema jana kuwa, lengo la kikao hicho ni kupata maelezo kutoka kwa Papic na benchi lake la ufundi pamoja na wachezaji.

Alisema kikubwa ambacho wanataka kujua kwanini timu hiyo imekuwa ikifanya vibaya katika mechi tatu mfululizo huku wachezaji wakiwa hawana matatizo yoyote yakiwamo ya kifedha.

Alipoulizwa kama kuna dalili za hujuma, Nchunga alisema ni vigumu kubaini hilo, isipokuwa hakuna mchezaji hata mmoja anayeidai Yanga.

“Hatuna deni na mchezaji yeyote, ndiyo maana tunataka tukutane nao tuwaulize sababu ya timu kufanya vibaya,” alisema Nchunga.

Hata hivyo, timu hiyo imekumbwa na hali hiyo huku Papic akiwa amemaliza mkataba wake wa awali ambao alisaini Oktoba mwaka jana.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kocha huyo kwa sasa anafundisha bila mkataba, akisubiri uamuzi wa mwisho wa uongozi kuhusu kusainishwa mpya au la, huku baadhi wakitaka aondoke.

No comments: