Friday, October 29, 2010

kampeni


Umati wa wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF), wakimsikiliza mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba (hayupo pichani), katika mkutano wa kufunga rasmi kampeni za chama hicho uliofanyika katika Viwanja vya Jangwani Dar es Salaam jana. (Na Fadhili Akida).

WAKATI vyama vingine vya siasa vikifanya kampeni kwa ajili ya kupata ushindi katika uchaguzi utakaofanyika kesho kutwa, CUF imesema kampeni zake ni sehemu ya kupata elimu kutoka kwa wapiga kura.

Aidha, chama hicho kimesema ilani yake ya uchaguzi ilitokana na hisia za mambo ambayo yanawagusa wananchi moja kwa moja.

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ambaye pia ni mgombea urais, alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akifungua semina iliyohusisha wanachama wa chama hicho kuhusu mambo mbalimbali aliyokutana nayo akiwa kwenye kampeni mikoani.

“Kampeni tulizofanya zilikuwa ni sehemu ya semina au mafunzo kwa wananchi … kampeni zilikuwa ni elimu, kubadilishana mawazo na wapiga kura,” alisema Profesa Lipumba.

Aliongeza kuwa akiwa katika kampeni zake mikoani, alikutana na wananchi katika maeneo mbalimbali ambapo miongoni mwa mambo ambayo walikuwa wakililia ni pamoja na wazee kutengewa eneo maalumu ili waweze kupewa huduma muhimu za maisha.

Katika mikoa aliyozunguka, wazee walisema wao ni wengi na kutokana na kutotekelezwa kwa ahadi ya kuwapa vijana ajira, wamejikuta wakikosa uwezo wa kuwahudumia, hivyo ni vyema Serikali ijayo, ikawapa hifadhi maalumu na huduma za kijamii.

Profesa alisema wananchi wamekuwa wakitaka serikali ijayo isiyo na matumizi makubwa ya anasa na badala yake ibane matumizi.

“Suala lingine lililosisitizwa ni pamoja na utekelezwaji wa Kilimo Kwanza kwa vitendo, kuliko kuendelea kubadili sera zake kila mara,” alisema Profesa Lipumba.

Aidha, alisema jambo lingine ambalo wananchi wamekuwa wakisisitiza ni pamoja na elimu bora kwa kila Mtanzania na kwamba mfumo uliojengeka sasa wa matabaka uondolewe.

Alisema tatizo hilo linaonekana wazi katika shule za kata ambako hakuna walimu, vitabu na
hata maktaba na hata watoto wa vigogo hawaonekani kwenye shule hizo na kwamba elimu bora iwe ni haki ya kila Mtanzania.

No comments: