Friday, October 29, 2010

Wajasiriamali wakopa bilioni 41/- NMB

BENKI ya NMB imetoa mikopo ya Sh bilioni 41 kwa wajasiriamali wadogo na wa kati wapatao 10,000 nchini katika kipindi cha miezi miwili.

Hayo yalisemwa jana na Meneja Mwandamizi mikopo midogo na ya kati wa benki hiyo, Filbert Mponzi wakati wa uzinduzi wa klabu ya wafanyabiashara wateja wa NMB.

Alisema, mikopo hiyo ilitolewa katika kipindi cha mwezi Agosti na Septemba ambapo katika mwezi Agosti walitoa mikopo ya Sh bilioni 21 iliyowanufaisha wajasiriamali 6,000 na Septemba wajasiriamali 4,000 walinufaika kwa mikopo ya Sh bilioni 20.

Mponzi alisema, uzinduzi wa klabu hiyo ni sehemu ya mikakati wa kuboresha huduma za benki hiyo zinazotolewa kwa wateja wake wa biashara.

Mponzi alisema, thamani ya wateja wa NMB imekuwa ikiongezeka kila siku ambapo wajasiriamali wadogo wamekuwa wakipatiwa mikopo ya kati Sh 100,000 hadi Sh milioni 5.

Alisema wajasiriamali wa kati wamekuwa wakikopeshwa kati ya Sh milioni 5 hadi Sh milioni 500 kulingana na ukubwa wa mtaji na kwamba katika kundi hilo la wajasiriamali limeongezeka kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na siku za nyuma na kuifanya benki hiyo kuvuka malengo yake.

Alisema wanachama wa klabu hiyo watapata nafasi ya kutoa mawazo, maoni, ushauri kwa uongozi wa benki hiyo pamoja na changamoto zinazowakabili.

Aidha amewaomba wafanyabiashara wa klabu hiyo kuwa mabalozi kwa wateja wengine kwa kuondoa dhana kuwa benki hiyo ni kwa ajili ya wateja wadogo tu kwani hata mikopo mikubwa inatolewa.

Naye Meneja Mwandamizi Uhusiano wa benki hiyo, Shyrose Bhanji alisema benki hiyo imeanza kubadilika kwa kasi na sio benki ya makabwela kama ilivyokuwa imezoeleka bali inatoa huduma hadi kwa wateja wakubwa wa biashara.

Alisema NMB kuanzisha klabu ya wafanyabiashara wa benki hiyo ina lengo la kuwaweka karibu wafanyabiashara wateja ili waweze kubadilishana mawazo, uzoefu, kupeana taarifa na vilevile kuwa na jukwaa la kuzungumza kwa ukaribu na wateja wao.

Pia wateja hao wanachama watapata nafasi ya kutengeneza na kuunda uhusiano wa kibiashara baina yao.

Uzinduzi wa klabu hiyo yenye wanachama 150 wa awali ilikwenda sambamba na wafanyabiashara hao kupewa mafunzo mbalimbali yakiwemo ya mchanganuo wa biashara, utunzaji wa kumbukumbu na huduma za kibenki.

No comments: