Friday, October 29, 2010

Waliotoboa siri kura hewa wapewa dhamana

na Moses Ng'wat, Mbozi




HATIMAYE watuhumiwa wawili ambao ni viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kata ya Tunduma, wilayani Mbozi, wanaokabiliwa na kesi ya kutoa taarifa za uongo kuhusu kuingizwa nchini karatasi za kupigia kura zilizowekewa alama ya ‘vema’ kwa mmoja wa wagombea sita wa kiti cha urais, kupitia mpaka wa Tunduma, wameachiwa kwa dhamana na Mahakama ya wilaya Mbozi.

Watuhumiwa hao waliopewa dhamana ni mweka hazina wa chama hicho kata ya Tunduma,Victor Mateni na Joseph Machemba, ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho Mtaa wa Sogea katika mji huo mdogo wa Tunduma.

Hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbozi , Rahimu Mushi, alisema mahakama hiyo imeamua kuwapa dhamana watuhumiwa hao ambao wamekaa rumande kwa siku nane, kwa sababu ni haki yao ya msingi kulingana na sheria.

Hakimu huyo alisema kuwa katika kesi hiyo ambayo kwa mara ya kwanza ilisomwa Oktoba 20, watuhumiwa wote wawili wanakabiliwa na taarifa ya kutoa taarifa za uongo kwa mtumishi wa serikali juu ya kuwepo gari lililokuwa limebeba karatasi za kupigia kura kutoka nje ya nchi na zilikuwa zikiingizwa nchini.

Alisema licha ya kuwa na wadhamini wawili kila mshitakiwa katika kesi hiyo, pia wadhamini hao walitakiwa kuwasilisha dhamana ya maandishi kiasi cha shilingi milioni moja kila mmoja.

Watuhumiwa hao wamepewa masharti ya kutojihusisha na shughuli yoyote ya kisiasa katika wakati huu wa uchaguzi hadi hapo kesi hiyo itakapokuwa imekamilika.

No comments: