Friday, October 29, 2010

Mgombea CHADEMA ambeba wa TLP

na Christopher Nyenyembe, Chunya
MGOMBEA Ubunge kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), katika Jimbo la Lupa wilaya ya Chunya,George Mtasha ameamua kupanda jukwaani na kumpigia kampeni mgombea ubunge wa Tanzania Labour (TLP), Sunday Sanga ambaye anapewa nafasi kubwa ya kutwaa jimbo hilo.
Katika hali inayoonyesha kuwa wagombea hao wawili kutoka vyama hivyo viwili wamepania kumuamgusha mgombea wa CCM, Victor Mwambalaswa juzi mgombea wa CHADEMA, Mtasha alipanda jukwani katika mkutano wa kampeni wa Sanga wa TLP na kumnadi kwa wananchi waliofika Chunya mjini kwenye Kata ya Chokaa.

Mtasha alitamka wazi kuwa anamtuma, Sanga aende bungeni na kukalia kiti namba 111 kilichokuwa kikikaliwa na Mwambalaswa kwa kuwa hana nafasi tena ya kurudi bungeni na kama kuna kitu amesahau akachukuliwe apewe.

“Nakufahamu vizuri ndugu yangu Sanga na jinsi wananchi wanavyokukubali nenda Dodoma kakalie kiti namba 111, kachukue koti alilosahau Mwambalaswa umletee najua hawezi kwenda huko tena,kama ukishindwa ujue nafasi ya ubunge ni yangu sio wa CCM tena, watu wamechoka, tumepigika vibaya” alisema Mtasha.

Akishangiliwa na wananchi wakati wa kumnadi mgombea mwenzake wa kambi ya upinzani, katika mkutano huo aliwaomba wananchi wa wilaya ya Chunya kuhakikisha kura zote za urais ifikapo Oktoba 31 wanampa mgombea wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, kuwa ndio chaguo pekee la Watanzania na hana kiongozi kutoka CCM anayeweza kulinganishwa nae.

Mgombea ubunge wa TLP , Sanga alisema kuwa uamuzi wa mgombea ubunge mwenzake wa CHADEMA kuamua kumpigia kampeni kumetokana na uelewano wa dhati wa kuleta mageuzi na kwamba wapo tayari ubunge huo utabaki TLP au CHADEMA kuliko kwenda CCM kwa kuwa mbunge aliyemaliza muda wake (Mwambalaswa) hana kitu alichokifanya kwa ajili ya maendeleo ya jimbo hilo.

No comments: