Friday, October 29, 2010

Vincent Nyerere aionya CCM Musoma

na Sitta Tumma




MGOMBEA ubunge kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Jimbo la Musoma Mjini, mkoani Mara, Vincent Nyerere, ametoa onyo kwa vyombo vya ulinzi na wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mjini hapa kuacha lugha chafu ndani ya jimbo hilo.

Alisema hahitaji kwenda bungeni, huku damu ya Wana Musoma ikiwa imemwagika kwa sababu ya tamaa ya madaraka ya watu wachache, ambao wamekuwa wakichochea vurugu na ghasia hizo.

Nyerere alitoa kauli hiyo juzi katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika eneo la Kibini, Kata ya Kigera, ambapo maelfu ya wakazi wa jimbo hilo la Musoma Mjini walifurika kusikiliza sera za mgombea huyo.

Alisema Tanzania ambayo Mwalimu Julius Nyerere ameiacha ni ya amani na haikuwa na vita, ni lazima Watanzania wadumishe umoja huo na si vinginevyo.

“Ndugu zangu, Tanzania tunayoihitaji ni Tanzania ya amani, kwani sihitaji kuwa kiongozi katika taifa ambalo limemwaga damu,” alisema Nyerere.

Aliwaasa Wana Musoma na Watanzania kwa ujumla, kuwa watulivu na kuhakikisha wanachagua viongozi ambao watawasaidia katika miaka mitano ijayo.

Akiwa katika Kata ya Nayakato jana, mgombea huyo alisema kuwa suala la barabara mbovu katika jimbo hilo si la kuuliza kwani hiyo ni ishara kuwa mbunge aliyemaliza muda wake hakuwathamini wananchi.

No comments: