Friday, October 29, 2010

Ndesamburo aishika pabaya CCM

• NEC yazuia mahafali ya wanafunzi


na Mwandishi wetu, Moshi
UPEPO wa kisiasa umebadilika katika Jimbo la Moshi Mjini ambako zikiwa zimesalia siku mbili tu Watanzania wapige kura, mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Philemon Ndesamburo, anaonekana kukivuruga Chama Cha Mapinduzi(CCM).

CCM sasa imeanza kuhaha na kubuni mbinu za kupunguza kasi ya Ndesamburo maarufu kwa jina la “Ndesa Pesa” baada ya kuonekana kukubalika kwa wapiga kura bila kujali itikadi zao, huku mgombea wa CCM, Justine Salakana, akidaiwa kutegemea kudra za Mwenyezi Mungu kumshinda.

Licha ya CCM kutumia kila aina ya mbinu za kumvuruga Ndesamburo, ikiwemo kusambaza vipeperushi vya kumchafua pamoja na matumizi makubwa ya fedha zilizochangwa maeneo mbalimbali ya nchi ikiwamo harambee iliyoendeshwa na Rais Jakaya Kikwete, mambo bado ni magumu.

Katika tukio la kushangaza kama si kuchekesha, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imepiga marufuku mahafali ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Majengo, inayomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi yaliyokuwa yafanyike kesho kwa kile kinachoelezwa ni misingi ya kisiasa.

Habari za uhakika kutoka ndani ya shule hiyo, zilizodhibitishwa na Mkuu wa shule hiyo, Peter Lyimo, zimedai kuwa tume hiyo imepiga marufuku mahafali hayo ikiegemea katika misingi ya hali ya usalama.

Hata hivyo, kupigwa marufuku kwa mahafali hayo kumezua sintofahamu miongoni mwa wakazi wa mji wa Moshi wengi wakihoji hatua ya NEC, lakini wengine wakienda mbali wakidai mafuriko kamwe hayawezi kuzuiwa kwa mikono.

Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Moshi Mjini, Bernadette Kinabo alikiri jana kuzuiwa kwa mahafali hayo, lakini alikataa kuingia kwa undani na kulitaka gazeti hili kwenda kusoma barua iliyotumwa kwa uongozi wa shule hiyo ambayo hata hivyo imedaiwa kupigwa mhuri wa siri.

Wakati msimamizi huyo akigoma kuelezea kwa undani sababu za kuzuiliwa mahafali hayo, habari za uhakika kutoka ndani ya shule ya majengo zimedai kuwa, kabla ya kuzuiliwa mkuu wa shule hiyo juzi, aliwekwa kiti moto na Kamati ya Ulinzi na Usalama kwa zaidi ya saa mbili.

Kamati hiyo inamjumuisha Mkuu wa Usalama wa Taifa wa Wilaya (DSO), Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) na maofisa wengine na taarifa zinadai kuwa, zuio hilo ni agizo kutoka ngazi za juu serikalini.

Taarifa zinadai kuwa, CCM ililazimika kukimbilia NEC kutaka mahafali hayo yazuiliwe kutokana na kile kilichoelezwa yanaweza yakatumika kumjenga kisiasa Ndesamburo ambaye kila kukicha nyota yake inazidi kug’ara.

Aidha, imebainika kuwa mmoja wa walimu wa shule hiyo, Pantaleo Minja ni mmoja wa wanaowania kiti cha udiwani katika kata hiyo ya Majengo kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), na anaonekana kuungwa mkono na makundi mbali mbali hasa vijana.

Mkuu wa shule hiyo, Peter Lyimo, licha ya kuthibitisha kutokuwepo kwa mahafali hayo, alikataa kuingia kwa undani zaidi na kueleza kwa ufupi kuwa wamefuta mahafali ili kupisha uchaguzi mkuu na sasa yatafanyika Novemba, mwaka huu.

No comments: