Friday, October 29, 2010

CCM yamwaga damu

• Wamkatakata mapanga mgombea udiwani UDP


na Stella Ibengwe, Bariadi
JESHI la Polisi wilayani Bariadi, mkoani Shinyanga, linawashikilia wafuasi saba wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kosa la kumkatakata mapanga mgombea udiwani wa Chama cha United Democratic (UDP), Benjamin Matondo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Daud Siasi, alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 12 jioni katika Kijiji cha Old Maswa wilayani humo.

“Ni kweli tunawashikilia wafuasi saba wa CCM, kwa kosa la kumkatakata kwa mapanga mgombea wa UDP, baada ya kumfuata nyumbani kwake bila sababu za msingi, tunatarajia kuwafikisha mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili,” alisema Kamanda Siasi.

Kamanda Siasi, aliwataja wana CCM hao kuwa ni Ali Issa (35), Alex Malini (28), Masunga Amos (25), Mussa Joseph (18), Emanuel Lyanga (40), Masumbuko Juma (30) na Evod Philemon (27).

Alisema Wilaya ya Bariadi tangu kuanza kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu zianze haikuwa na vurugu, hatua ambayo amewataka wananchi kuacha kujihusisha na hali hiyo, kwani wakibainika watachukuliwa hatua za kisheria.

Kamanda Siasi alisema katika tukio hilo, watu wawili walijeruhiwa vibaya akiwemo mgombea udiwani huyo ambaye alijeruhiwa kwa kukatwa na mapanga kichwani na kukimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Somanda, ambapo alipatiwa matibabu na kuruhusiwa.

Alimtaja mwingine aliyejeruhiwa ambaye ni ndugu yake na mgombea kuwa ni Edward Nestory (43), ambaye amelazwa katika hospital hiyo kutokana na kupata majeraha makubwa.

Kutokana na vurugu hizo, gari la mgombea ubunge kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika Jimbo la Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, lilishambuliwa kwa mawe na kuvunjwa vioo na wafuasi wa UDP.

Alisema hadi jana gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser linashikiliwa na polisi.

Fujo hizi zinatokea ikiwa ni siku chache, baada ya vurugu nyingine kutokea katika Wilaya ya Maswa, ambako mgombea ubunge kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), katika Jimbo la Maswa Magharibi, John Shibuda, alikamatwa na kuwekwa ndani baada ya kuhusishwa na vurugu zilizosababisha kifo cha mtu mmoja.

Katika vurugu hizo, dereva wa mgombea ubunge wa CCM, Steven Kwilasa Masanja, alifariki dunia kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kutokana na kipigo.

Kutokana na vurugu hizo, Jeshi la Polisi nchini liliunda tume ya watu wanne, iliyoongozwa na Mkrugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, baada ya uchunguzi wa siku kadhaa ilimwachia huru Shibuda, kwa kile ilichodai hakuwapo katika eneo la tukio siku hiyo.

No comments: