Friday, October 29, 2010

Mtikisiko Uchaguzi Mkuu

• CCM yadaiwa kuandaa mipango ya kuvuruga uchaguzi


na Mwandishi wetu
WAKATI zikiwa zimesalia siku mbili kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu Jumapili hii, hali ya kisiasa nchini inazidi kuwa tete na ya kutia shaka.

Hali hiyo kwa kiwango kikubwa imesababishwa na kuanza kuvuja kwa taarifa za kuwapo kwa mipango ya kuvuruga uchaguzi huo kwa wizi wa kura na kwa matendo yanayoweza kuathiri na kuingilia misingi ya uchaguzi ulio huru na wa haki.

Habari ambazo Tanzania Daima imezikusanya kutoka maeneo mbalimbali nchini zinaonyesha kuwa hali hiyo imechangiwa na ukweli kwamba hali ya ushindani wa kisiasa miongoni mwa vyama na wagombea wa urais, ubunge na udiwani ni mkubwa katika maeneo tofauti.

Vyanzo vya kuaminika kutoka ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) vinaeleza kwamba vikundi vya vijana wa chama hicho maarufu kwa jina la Green Guards wamesambazwa katika maeneo mbalimbali nchini wakiwa na maelekezo maalumu ya kuhakikisha wanadhibiti nguvu kubwa inayoonyeshwa na wagombea wa upinzani.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, moja ya mbinu ambazo zinakusudiwa kutumiwa na vijana hao wa Green Guards ni kubeba bendera za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kupita nazo katika maeneo ya vituo vya kupigia kura siku ya uchaguzi.

Habari hizo zinaeleza kwamba, vijana hao wa CCM ambao kwa siku kadhaa sasa wamekuwa wakikusanya bendera hizo za CHADEMA wanakusudiwa kufanya hivyo ili kujenga taswira itakayokiweka chama hicho katika hatia ya kuonekana kikienda kinyume cha sheria za uchaguzi kwa kupiga kampeni hadi siku ya uchaguzi.

Kwa mujibu wa habari hizo, vijana hao inasemekena wamepewa mafunzo maalumu ya kukabiliana na vyombo vya dola ambavyo vitakuwa na wajibu wa kusimamia hali ya ulinzi na usalama kwenye maeneo ya kupigia kura.

Mbali ya hilo, taarifa nyingine zinaeleza kuwa, mkakati mwingine unaoaminika kuwahusisha maofisa wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na wasimamizi wa uchaguzi katika maeneo tofauti ni ule wa kuwapo kwa vituo hewa vya kupigia kura.

Miongoni mwa maeneo ambayo tayari yamebainika kuingizwa katika mkumbo huo ni Jimbo la Segerea, jijini Dar es Salaam ambako kumekuwa na mvutano mkubwa kati ya vyama vya CHADEMA na CCM.

Miongoni mwa maeneo ambayo yameripotiwa kuwa na vituo hewa ni katika Kata ya Kipawa, ambako wananchi wamelieleza gazeti hili kwamba kuna vituo vipatavyo 11 ambavyo kuwapo kwake kunatia shaka.

Suala jingine linaloongeza hofu ya kuvurugwa kwa uchaguzi ni lile la kukosekana katika mbao za matangazo kwa majina ya wapiga kura katika maeneo tofauti nchini, hali ambayo pia inahusishwa na mkakati mahususi wa kuiba kura.

Aidha, huko huko Segerea kumeibuka malalamiko ya watu wasio raia wa Tanzania wanaotoka Malawi, Kenya na Uganda kujiandikisha kupiga kura katika vituo tofauti.

Miongoni mwa watu ambao uraia wao umeibua mashaka ni Yassin Osman, mwenye shahada 27113456, Forotia Mphoma mwenye shahada namba 48584049 na Reverine Samba 30546554, wote wakiaminika kuwa ni raia wa Malawi, Edwin Sijenyi 32194993 na Bakari Atilyo (Kenya) na mwisho ni Ouma Koroneli mwenye shahada 48641113 (Uganda).

Katika nyingine, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imempiga ‘stop’ mgombea ubunge pamoja na madiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika Jimbo la Maswa Magharibi, John Shibuda, kutoshiriki kampeni za Uchaguzi Mkuu kuanzia jana.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni wa CHADEMA, Profesa Mwesiga Baregu, alisema kitendo hicho kimeonyesha unyanyasaji mkubwa kwa vyama vya upinzani.

“Jeshi la Polisi halijathibitisha kama Shibuda ndiye chanzo cha vurugu katika tukio hilo, hivyo tunaamini Nec haina uthibitisho na wala haikutakiwa kutusimamishia kampeni katika siku hizi za mwisho kwa chama chetu pekee bali ilibidi isimamishe za vyama vyote au kumruhusu mgombea wetu kuendelea na kampeni,” alisema Profesa Baregu.

Alisema kwamba wapiga kura wanatakiwa kutokubali kudanganyika kwa kuwa Shibuda bado ni mgombea halali na atashiriki Uchaguzi Mkuu pamoja na madiwani katika jimbo hilo hata kama NEC imesimamisha kampeni za chama hicho kwa muda uliobaki.

Shibuda aliiambia Tanzania Daima kuwa pamoja na hujuma hizo ambazo anaamini zinafanywa na CCM, ataibuka na ushindi wa kishindo.

Dar es Salaam

Katika hali inayooneka kuwepo mazingira ya utatanishi wakati wa Uchaguzi Mkuu, mgombea mwenza wa Chama Cha Wananchi (CUF) Juma Duni, amesema Taasisi ya Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (Redet) na ile ya Synovate ni kati ya maandalizi yaliyotumiwa na CCM kutekeleza mpango wa kuiba kura na kuingiza kura hewa zaidi ya mil. nne kinyemela.

Akizungumza jana wakati wa kuhitimisha mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi, Duni alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inatakiwa kuhakikisha inasimamia uchaguzi ulio huru na wa haki.

Alisema baada ya kufanya uchunguzi na kuangalia idadi ya wapiga kura walioandikishwa mara ya kwanza, CUF iligundua kuwepo wapiga kura mil. 21, lakini baada ya kufuatilia, NEC ikapunguza idadi hiyo na kufikia mil. 19, huku ikiwa haijafahamika idadi ya mil. tatu ilipokwenda.

Alisema hata hivyo hadi sasa wamefuatilia na kugundua kupenyezwa kura zaidi ya mil. nne pamoja na majina hewa 200 ili kuongeza idadi ya kura na kuweza kumpa ushindi uliotabiriwa wa asilimia 71.

Alisema wizi huo umekuwa ukitekelezwa na usalama wa CCM ambao ndio wanaohakikisha kuingizwa kwa kura hizo.

Alisema ili kutekeleza wizi huo, CCM na serikali imekuwa ikiwatumia watendaji wa kata, vijiji na wasimamizi wa kura kama ilivyotokea mwaka 2005, hadi kusababisha CUF ikashindwa kupata wabunge kwa upande wa bara.

“Imebainika na ushahidi tunao, wananchi oneni karatasi zilizosaidia CCM kuibuka na ushindi mwaka 2005, ambapo wasimamizi walipewa vitu mbalimbali ikiwamo tochi, mihuri na kutakiwa kuchota kura katika magari,” alisema.

Kwa upande wake, mgombea urais kwa teketi ya chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema serikali imeuza nchi kwa bei poa, hatua inayosababisha makampuni ya madini kukwepa kodi huku serikali ikiambulia sh 3.

Alisema makampuni makubwa ya uchimbaji madini yanayochimba kwa mrabaha wa asilimia tatu, yamekuwa mstari wa mbele kukwepa kodi, hali inayochangia umaskini kwa wananchi.

“Kila mwaka sh bil. 150 za ushuru wa mafuta wa petroli na dizeli inapotezwa huku misamaha holela ya kodi inaondolewa,” alisema Profesa Lipumba.

Dar es Salaam

Majina ya wapiga kura zaidi ya 107 katika Kata ya Kiwalani, yamedaiwa kurudiwa zaidi ya kituo kimoja cha kupigia kura.

Wakizungumza na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti, wagombea wa kata hiyo, kupitia vyama vya CUF, Said Stawi na CHADEMA, Mathias Malamsha, walisema huo ni usanii uliofanywa na CCM ili kupanga matokeo.

Malamsha alisema ni jambo la kusikitisha watu wakiwa wanadai haki, huku wengine wakiwa wanafanya ujanja kama huo.

Alisema kuna taarifa wamezipata ambazo walithibitisha katika vituo vya kupigia kura kwamba majina yaliyosajiliwa ni ya kutoka katika Jimbo la Temeke na mmoja wa wagombea wa udiwani ndiye aliyehusika.

SHINYANGA

Wakati mchakato wa zoezi la upigaji kura likifika ukingoni, imebainika kuna vituo hewa vya kupigia kura vilivyoandaliwa katika Jimbo la Shinyanga Mjini.

Hali hiyo isiyokuwa ya kawaida imewafadhaisha wakazi wa Manispaa ya Shinyanga, wakiwemo viongozi wa vyama vya upinzani kutokana na kutumika kwa baadhi ya majina ya wapiga kura wa vituo vingine kwenye vituo hivyo hewa.

Kutokana na kubainika kwa upungufu huo, wenye kila sura ya kuvuruga au kuiba kura katika zoezi la uchaguzi wa Oktoba 31, baadaye wiki hii, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), mkoani Shinyanga kimemwandikia barua msimamizi msaidizi wa uchaguzi katika jimbo hilo.

Kituo kimoja kati ya vituo vilivyothibitishwa na waandishi wa habari kubeba upungufu ni kile cha namba 00018940 cha Chekechea Misheni, ambapo wapiga kura walioorodheshwa katika daftari la kupigia kura kwenye kituo namba tatu, majina 264 yamerudiwa kuandikwa, jambo ambalo limewashangaza wengi na kuweka dhana ya kuwepo kwa vituo hewa katika orodha ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Baadhi ya majina yaliyobainika kubeba udanganyifu huu ni pamoja na Veronica Paulo Nyanda mwenye shahada namba 11037634, Veronica Michael Shigulu (11061105), Veronica Philipo Alphonce (46588250) na Veronica Philipo Massawe (11042211), yakiwa yameandikwa kituo namba mbili, pia kuonekana kama yalivyo katika kituo namba tatu.

Wakati huo huo, Katibu wa chama hicho mkoani hapa, Nyangaki Shilungushela, akizungumzia hali hiyo, alisema kitendo hicho kimewapa wasiwasi, kuwa kuna mpango wa kuchakachua kura au kuongeza idadi ya kura hewa mara baada ya zoezi la upigaji kura kukamilika.

No comments: