Monday, June 21, 2010

CHADEMA yalaani vurugu Moshi

na Mwandishi wetuBARAZA la Umoja wa Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA), mkoani Kilimanjaro, limelaani fujo na mashambulizi yaliyofanywa na kundi la vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), dhidi ya wakazi wa mji wa Moshi.

Taarifa iliyotolewa na mwenyekiti wa umoja huo, Deogratius Munishi, kwa vyombo vya habari jana, ilisema vurugu hizo, zilisababisha raia kadhaa kujeruhiwa na wengine kupoteza fedha huku uharibifu mkubwa ukitokea kwenye jengo la kituo cha damu cha Hospitali ya Rufaa ya KCMC.

Alisema fujo hizo, zinadhihirisha wazi jinsi CCM walivyojipanga kuleta machafuko mjini Moshi na maeneo mengine ya Kilimanjaro wakati wa uchaguzi mkuu ujao.

“Dhamira hii ilibainishwa na Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Beno Malisa, kwa kauli aliyoitoa Februari, mwaka huu, kuwa Moshi itakuwa uwanja wa mapambano kipindi cha uchaguzi mkuu,” alisema Munishi.

Tukio la juzi ni la tatu katika viashiria vya dhamira hiyo, kwani Februari baada ya CCM kuzomewa wakati walipofanya maandamano ya kuwasimika makamanda wao wa mkoa na lile lililotokea kwenye uchaguzi wa serikali ya mtaa wa Kaloleni ambapo vijana wa UVCCM waliamua kutembeza kichapo kwa raia bila sababu za msingi.

“Fujo hizo zinaashiria kuwa UVCCM ni genge la wahuni kwani kitendo walichokifanya huwa kinafanywa na wahuni na sio chama cha siasa. Hakika hatuwezi kuona tofauti yoyote baina ya wahuni na UVCCM,” alisema Munishi.

“...UVCCM watambue kuwa siasa inaongozwa na uvumilivu. Kama huna hili hakika huwezi kufanya siasa. Je, na sisi BAVICHA tukisema tujibu mashambulizi, mji wa Moshi utakalika kweli? Sisi BAVICHA hatuwezi kufanya hivyo kwa kuwa siasa zetu ni za kisayansi, kistaarabu ambazo zinajali utu wa binadamu,” alisema Munishi.

Aliwataka wananchi wa Moshi, kutotishika na uhuni huo wa kisiasa unaofanywa na CCM na badala yake wachukue hatua madhubuti ya kuiadabisha kwenye uchaguzi mkuu ujao kwa kutowapatia kiti hata kimoja.

Alisema, BAVICHA inalitaka Jeshi la Polisi mkoani hapa, kuhakikisha wahuni wote waliohusika na vurugu hizi wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria bila upendeleo wa aina yoyote.

No comments: