Monday, June 21, 2010

CCM kumekucha

• JK achukua fomu Dodoma

na Kulwa KarediaWAKATI mbio za kuwania Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ule wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), zikianza leo, mmoja wa vigogo wanaotarajiwa kuchukua fomu, amepigwa kombora kuwa hafai kuwania nafasi hiyo.

Mgombea aliyepigwa kombora ni Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein ambaye leo na wagombea wengine watano wanatarajia kuchukua fomu visiwani Zanzibar kwa nyakati tofauti.

Mbali na Dk. Shein wagombea wengine wanaotarajiwa kuchukua fomu ni Waziri Kiongozi Shamsi Vuai Nahodha, Naibu Waziri Kiongozi Ali Juma Shamhuna, Waziri Kiongozi mstaafu, Dk. Mohamed Gharib Bilal, Ali Abeid Karume na aliyekuwa Mkurugenzi wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, Hamad Bakari Mshindo.

Kwa upande wa Tanzania Bara, Rais Jakaya Kikwete tayari amewasili mkoani Dodoma kwa ajili ya kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya wananchi kwa awamu ya pili.

Rais Kikwete, anakuwa mwanachama wa kwanza wa CCM kwa upande wa bara kujitokeza kuchukua fomu, licha ya kuenea tetesi kuwa kuna baadhi ya vigogo wengine wanajiandaa kufanya hivyo.

Habari za kuaminika zinasema tayari Rais Kikwete na timu yake ya wapambe, wamefanya maandalizi ya kila aina ambayo yanaonekana kuwa ya kihistoria tofauti na ilivyokuwa mwaka 2005 alipochukua fomu.

Kwa upande wa urais wa Zanzibar, Dk. Shein amedaiwa kutokuwa na sifa za kuwania kiti hicho kutokana na jina lake kutokuwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kisiwani Zanzibar.

Habari za kuaminika zilizopatikana kutoka Zanzibar, zinasema Dk. Shein alijiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wakipiga kura eneo la Oysterbay, Dar es Salaam.

Habari hizo zinasema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, kifungu 26(2) C na kifungu 27(4) vinaeleza kuwa mtu anayestahili kuwa Rais anatakiwa kuwa na sifa za kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, wakati kifungu 27(4), kikieleza mtu yeyote mwenye sifa aliyejiandikisha kumchagua mjumbe wa Baraza la Wawakilishi atakuwa na uwezo kupiga kura katika uchaguzi wa Rais.

Kutokana na hali hiyo, vifungu vya Katiba vinamfanya Dk. Shein akose sifa za kugombea nafasi hiyo nyeti kisiwani humo.

Wadadisi wa mambo, wanasema Dk. Shein hana mvuto wowote kwa wananchi wa Zanzibar na kuwa kumteua mgombea ni sawa na kukisafishia njia Chama cha Wananchi (CUF) kuingia Ikulu kirahisi.

Lakini kama Dk. Shein atachaguliwa Rais wa Zanzibar ina maana makamu wake pia atatoka Pemba maana CUF ina nguvu Pemba; kama Rais na Makamu watatoka Pemba utata utajitokeza katika uundwaji wa serikali ya umoja wa kitaifa.

1 comment:

Anonymous said...

russian women awaiting for you!
http://www.myfreeown.com