Monday, June 21, 2010

Baraza Kuu CUF kuteua wagombea

na Shehe Semtawa



CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema maamuzi ya mgombea atakayesimama jimboni kwa ajili ya kupambana na wagombea kutoka vyama mbalimbali yatakamilishwa na Baraza Kuu la chama na si kura za maoni za wajumbe.

Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kwenye mkutano mkuu maalum wa kura za maoni za kuwapata wagombea ubunge watakaosimama majimboni na wale wa kuteuliwa katika wilaya ya Temeke.

“Ifahamike kuwa kura za maoni za wajumbe hazimteui mgombea ubunge moja kwa moja na wala katika uchaguzi huo hakuna mshindi bali kinachofanyika kwa wajumbe ni kusaidia kuwapata watu ambao ni waadilifu na wenye uzoefu watakaokisaidia chama,” alisema.

Aidha, alisema wajumbe watambue kuwa hadi wakati huu chama hakina mgombea hadi baraza kuu taifa litakapoyapitia majina hayo kwa ajili ya kutambua uadilifu wa wagombea na kuteua mgombea atayepambana na wagombea wa vyama vingine.

Uchaguzi huo ulikamilika kwa msimamizi wa uchaguzi huo Twaha Rashid kutangaza matokeo ya walioongoza ubunge. Kutoka jimbo la Temeke; Kidau Limbu kura 86 na Abdallah Mtolea kura 71; viti maalum kuwa ni Zainabu Mndolwa na Pili Mfaume.

Kwa upande wa Kigamboni walioongoza ubunge ni Mustafa Ismail na Ahmad Khamisi, viti maalum walikuwa Mwanakombo Tajiri na Rose Silayo.

No comments: