Monday, June 21, 2010

CUF wachapana makonde Dar

na Mwandishi wetuMCHAKATO wa ubunge wa Viti Maalum jimbo la Segerea kupitia Chama cha Wananchi (CUF), juzi uliingia dosari baada msimamizi wa uchaguzi huo kutoweka na masanduku ya kupigia kura huku baadhi ya wanachama wakichapana makonde.

Tukio hilo, lilitokea usiku wa kuamkia jana katika ukumbi wa Ukonga Hill Tec uliopo Banana Dar es Salaam, mara baada ya zoezi la kupiga kura, ambapo inadaiwa wagombea wawili katika kinyang’anyiro hicho, Asha Bani na Ashura Mustafa walikuwa wakisubiri matokeo na mara ghafla uliibuka mzozo wa kutaka matokeo yasitangazwe kutokana na kile kilichodaiwa Bani ameibuka na ushindi.

Mashuhuda wa tukio hilo waliliambia Tanzania Daima kuwa msimazi wa uchaguzi huo aliyefahamika kwa jina moja la Zumba, alishindwa kufanya hivyo kutokana na idadi ya kura kuzidi.

“Kulikuwa na vurugu kubwa, msimamizi alidai kura tano zimezidi kutoka kwa wajumbe na kudai hawezi kutangaza matokeo ya uchaguzi huo, na kukimbilia makao makuu kwa ajili ya ufafanuzi zaidi,” walisema.

Kwa mujibu wa mashuhuda hao, msimamizi huyo alifika makao makuu, alishauriwa kuhesabu kura hizo, ambapo alishindwa kutii amri hiyo na kushikilia msimamo wake.

Hata hivyo, Tanzania Daima ilipowasiliana na Zumba alikiri kutokea kwa matukio hayo, na kudai alishindwa kutangaza matokeo kutokana na sababu za msingi zikiwemo za kuongezeka kwa kura tano za wajumbe huku idadi kamili ikiwa 110.

No comments: