Sunday, April 4, 2010

Mwenyekiti wa CCJ augua ghafla

• CCM yaugua homa ya Mpendazoe

na Francis DandeSIKU chache baada ya Mwenyekiti wa Chama Cha Jamii (CCJ), Richard Kiyabo, kuporwa nyaraka nyeti zinazohusu chama hicho, hali ya afya ya mwenyekiti huyo imezidi kuzorota.

Kiyabo jana alilazimika kukimbizwa katika kituo cha Afya cha Dk. Hameer kilichoko maeneo ya Fire, jijini Dar es Salaam, baada ya kuugua shingo na kubanwa na kifua.

Mwenyekiti huyo katika siku za hivi karibuni amekuwa akiwatuhumu watu mbalimbali wakiwamo watendaji wa serikali kwa jitihada za kutaka kukihujumu chama hicho ili kisipate usajili wa kudumu.

Kiyabo, ambaye amekuwa akitembea kwa miguu katika mitaa mbalimbali ya jiji la Dar es salaam bila kuchukua tahadhari yoyote, amesema kuugua kwake ni matokeo ya kuvamiwa na kujeruhiwa wiki iliyopita.

Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili akiwa kitandani katika hospitali hiyo, Kiyabo, alisema tangu akabwe, kuporwa na kujeruhiwa afya yake haijatengamaa lakini hakuwahi kwenda hospitali mpaka jana alipozidiwa.

Alisema katika tukio hilo la uporaji, alikabwa shingo pamoja na kubanwa kifua; na mkoba wake uliokuwa na shilingi laki tano, Laptop pamoja na reja iliyokuwa na orodha ya majina ya wanachama wa chama hicho kwa upande wa Zanzibar vilichukuliwa na waporaji.

Kiyabo ambaye mara kadhaa amekuwa akilihusisha tukio hilo na njama zinazofanywa na baadhi ya watendaji wa vyombo vya dola, amesema ni vema Jeshi la Polisi likampa ulinzi hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.

“CCJ hivi sasa tunahujumiwa, kila mtu leo hii anataka kujua tunakwendaje na shughuli zetu zinafadhiliwa au kuwahusisha watu wa aina gani,” alisema.

Mwenyekiti huyo amesema analihusisha tukio la kukabwa kwake na watendaji wa vyombo vya dola kwa kuwa kabla ya tukio la uboraji halijafanyika watu waliomkaba walimtisha na kisha kumtolea vitambulisho vilivyokuwa vikionyesha kuwa ni wafanyakazi wa serikalini.

“Niliwaambia kuwa kama nina makosa wanipeleke kwenye vyombo vya sheria lakini walizidi kunikaba na kunipora; hii ilionyesha walikuwa na mkakati maalumu wa kuidhoofisha CCJ,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema matukio hayo ni ya kisiasa kutokana na mazingira yake na kuliomba Jeshi la Polisi kulinda raia wake na kufanya uchunguzi wa kina kuwajua waliohusika na tukio hilo ili sheria ifuate mkondo wake.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida mwenyekiti huyo alisema, “Hata kama nikifa leo Watanzania wasinitafute katika makaburi yaliyopakwa rangi nzuri ila wanitafute kwenye mioyo ya watu wanyonge milioni 40 walio mijini na vijijini, hali si nzuri; sina hela hata mchana sijala,” alisema mwenyekiti huyo na kuongeza kuwa Watanzania wamchangie katika gharama za matibabu ambazo ni kubwa.

Daktari wa zamu, Dk. Sombi Charles, aliyekuwa akisaidiana na Dk. Nassor alisema kuwa katika kumfanyia uchunguzi wao walibaini kuwepo kwa matatizo katika shingo na kifua kutokana na kupata mgandamizo wa kitu chenye ncha butu kwenye shingo na kumsababishia matatizo katika mishipa ya fahamu.

“Hivi sasa tumempatia matibabu ya awali ili kupunguza maumivu aliyokuwa nayo wakati tukimsubiri mtaalamu wa mishipa ya fahamu, Dk. Othman afike ili kumfanyia uchunguzi wa kina kwa ajili ya kutoa tiba sahihi kwa mgonjwa.”

CCJ imekuwa ikipata nguvu na kuvuta hisia za watu mbalimbali na hali hiyo iliongezeka wiki hii baada ya Mbunge wa Kishapu kwa tiketi ya CCM, Fred Mpendazoe, kutangaza kuihama CCM na kujiunga na CCJ.

Tangu Mpendazoe atangaze hatua hiyo, viongozi wa juu wa CCM na makada wa ngazi mbalimbali wa chama hicho tawala wamekaririwa wakitoa matamshi tofauti yenye mwelekeo wa kumponda mwanasiasa huyo ambaye alikuwa miongoni mwa wabunge waliokuwa wakijipambanua kuwa wapambanaji wa ufisadi.

Hata hivyo, tangu atangaze uamuzi wake huo wa kuihama CCM, makamanda wengine wa ufisadi akiwamo Mbunge wa Nzega, Lucas Sellelii, na mwenzake wa Same Mashariki, Anne Kilango, kwa nyakati tofauti, wamejitokeza kumpinga mwenzao na kukana kuwa na mpango wa kwenda katika chama hicho chenye usajili wa muda.

No comments: