Wednesday, April 7, 2010

Bilioni 50/- za kampeni za JK zazua balaa

• Wadau wa siasa waja juu, wapinga kiwango hicho


na Mwandishi Wetu
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimepenyeza mapendekezo yake kwenye ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ikitaka kuhalalisha matumizi ya sh bilioni 50 ilizopanga kuzitumia kwa ajili ya kampeni za mgombea wake, Rais Jakaya Kikwete.
Hali hiyo ilibainika jana kwenye kikao cha wadau wa siasa nchini pamoja na ofisi ya msajili kuhusu kanuni ya sheria ya fedha za uchaguzi kilichofanyika jijini Dar es Salaam jana.

Katika kikao cha Machi 22 na 23, wadau hao walipendekeza kuwa gharama za jumla za mgombea urais na chama chake, zisizidi sh bilioni 5 kuanzia uteuzi hadi kwenye kampeni za ndani na nje ya chama.

Kwa mujibu wa mjadala wa jana ambao ulikuwa mkali, ofisi ya msajili inayoongozwa na John Tendwa ilikuja na pendekezo jipya la CCM lililotaka serikali ipitishe kanuni ya matumizi ya sh bilioni 27 kwa ajili ya kampeni za mgombea urais.

Kwa mujibu wa mapendekezo hayo ambayo yaliwashangaza wadau wengi na kuibua mjadala mzito ndani ya kongamano hilo, CCM imetaka itumie sh bilioni 2 kwa ajili ya mkutano wa uteuzi wa mgombea wake wa urais, sh bilioni 3 kwa ajili ya uteuzi wa wagombea ubunge.

Pia ilitaka itumie sh milioni 500 kwa ajili ya uteuzi wa wabunge wa viti maalum kwa nchi zima, sh bilioni 2 kwa ajili ya uteuzi wa wagombea udiwani na sh milioni 200 kwa ajili ya uteuzi wa wagombea udiwani wa viti maalum.

Kwa mujibu wa habari hizo kutoka ndani ya kikao hicho, CCM ilitaka itumie sh bilioni 5 kwa ajili ya kampeni za mgombea wake kusaka kura za maoni na sh bilioni 5 zingine kwa ajili ya kampeni za nje ya chama.

“Mapendekezo hayo ni mapya kabisa na msajili mwisho wa siku alikiri kwamba ameletewa na CCM tofauti na makubaliano yetu ya kikao cha kwanza kilichopitisha sh bilioni 5 kwa ajili ya kampeni zote za mgombea urais kuanzia kura za maoni, mkutano mkuu hadi kampeni nje ya chama, wabunge sh milioni 40 na madiwani sh milioni 10. Vyama vyote tumeyakataa mapendekezo hayo na tumeshindwa kuyapitisha,” alisema mmoja wa wajumbe kutoka ndani ya kikao hicho.

Kutokana na mvurugano huo, Msajili alivitaka vyama vyote kuendelea kuwasilisha maoni yao katika ofisi yake ili ayafanyie kazi na kuyakabidhi kwa waziri husika.

Iwapo mapendekezo hayo yatapitishwa, CCM itakuwa imefanikiwa kuhalalisha mpango wake wa kutaka kutumia sh bilioni 50 kwa ajili ya kampeni za mgombea wake, jambo ambalo ni kinyume na sheria iliyoasisiwa na kusainiwa kwa mbwembwe na Rais Jakaya Kikwete.

Kuhusu timu ya kampeni, wadau hao walikubali kupitisha pendekezo linalotaka timu ya mgombea wa kiti cha urais iwe na watu 50, wabunge watu 20 na madiwani watu kumi. Hata hivyo kanuni hiyo ilipita kwa shida kutokana na wadau wengi kutoikubali.

Eneo lingine lililoleta mzozo ni kuhusu hoja ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbrod Slaa aliyepinga timu ya wagombea urais kuhakikiwa na ofisi ya Msajili wa vyama, wabunge kuhakikiwa na Makatibu Tawala wa Wilaya na Madiwani kuthibitishwa na Watendaji wa Kata.

Kwa mujibu wa Dk. Slaa, kipengele kinachoonyesha viongozi hao wanapaswa kuthibitisha timu za wagombea husika, kilichomekwa kwani hakikuwepo kwenye muswada wa sheria na kuitaka serikali kurejesha mswaada huo bungeni.

Hata hivyo akifafanua suala hilo, Tendwa alisema
mapendekezo ya suala hilo yatawekwa katika lugha nzuri na kuyapeleka kwa waziri husika.

Tangu CCM itangaze mkakati wake wa kutaka kukusanya sh bilioni 40 kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu za mkononi kwa ajili ya kampeni zake tofauti na mapendekezo ya wadau waliopitisha sh bilioni tano, Tendwa amekuwa na kigugumizi kujadili mkanganyiko unaoendelea kuhusu sheria mpya ya gharama za uchaguzi ambayo inaweka viwango vya pesa zinazopaswa kutumika.

Wakati tayari CCM imeonyesha dalili za kuvunja sheria hiyo kwa kukusanya bilioni 50/- badala ya bilioni 5/- zilizopendekezwa, huku baadhi ya wadau wakilalamikia ubabe huo wa CCM, Tendwa amedai kwamba ni mapema mno kwa vyama vya siasa, na vyombo vya habari kuanza kuzinyoshea kidole kanuni za utekelezaji wa sheria ya kudhibiti gharama za uchaguzi.

Kauli ya Tendwa imekuja baada ya gazeti hili kumtaka aeleze makusudi yake juu ya kudhibiti kiasi sh bilioni 50 zilizopangwa kuchangishwa na CCM kwa ajili ya mchakato wa Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu.

Katika maelezo yake, Tendwa alisema kanuni za sheria hiyo bado hazijakamilika kwa kuwa wadau wanaendelea kupeleka maoni yao.

“Hatujaweka kanuni bado… sasa ninyi mnataka kuweka conclusion kabla sisi hatujaweka conclusion… usinunue mbeleko kabla mtoto hajazaliwa; sasa kanuni bado nashangaa nimeona kwenye vyombo vya habari wanalalamika, huku ni kupotosha.

“Subiri tukamilishe mchakato na tarehe 6 Aprili tunakutana, hizo kanuni kama rais bilioni 5/- zitakuwa zimepita ndipo tutazungumza,” alisema Tendwa.

Baada ya gazeti hili toleo la Jumatano kuripoti kuwa CCM imetenga sh bilioni 50 kwa ajili ya mchakato wa Uchaguzi Mkuu ujao, habari hizo zilionekana kukishtua Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, aliielezea hatua hiyo ya CCM kuwa ni kielelezo cha namna chama hicho tawala kilivyo mstari wa mbele kuvunja Sheria ya Gharama za Uchaguzi iliyosainiwa na Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni.

Mbowe alisema ni jambo lisiloingia akilini kwa chama ambacho mwenyekiti wake ambaye ni rais aliyesaini sheria ya kudhibiti gharama za uchaguzi hivi karibuni, kuwa cha kwanza kuvunja sheria.

Kutokana na hilo, Mbowe alisema kitendo cha CCM kuazimia kukusanya shilingi bilioni 50 kinaonyesha kuwa chama hicho kinakusudia kuwa na fedha nyingi ambazo zinaweza kuzidi kiwango cha makadirio yaliyopendekezwa na wadau.

Alisema iwapo watampa mgombea wao wa urais sh bilioni 5 na kutoa kiasi cha shilingi milioni 50 kwa kila mgombea wao wa ubunge katika majimbo yote 232 yaliyopo sasa basi watakuwa wametumia jumla ya shilingi bilioni 16.5.

Aidha, wakifanya hivyo pia kwa kuwasaidia wagombea wao wote wa udiwani katika kata zote nchini zinazokadiriwa kufikia 3,000 kiasi cha shilingi milioni moja kwa kila mgombea, kama kanuni zinavyopendekeza, basi watatumia jumla ya shilingi bilioni tatu.

Alisema ukijumlisha mgawo wote huo utakaotengwa kwa mgombea urais, wabunge na madiwani wa chama hicho tawala pekee, basi CCM itakuwa imetumia jumla ya shilingi bilioni 19.5 kiasi ambacho ni kidogo kulinganishwa na malengo ya shilingi bilioni 50 walizopanga kuzikusanya.

Katika hatua nyingine, wafanyabiashara mbalimbali nchini, wakiwemo waliopata kutuhumiwa kwa ufisadi na hata wengine kufikishwa mahakamani, wamealikwa kwenye harambee ya kuchangia kampeni za mgombea urais CCM, Rais Kikwete.

Habari ambazo Tanzania Daima Jumatano imezipata, zinasema kuwa wafanyabiashara wote maarufu jijini na nje ya mkoa wa Dar es Salaam, wamealikwa kwenye harambee hiyo ambayo itakwenda sambamba na uzinduzi wa programu ya uchagishaji fedha kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu za mkononi.

Mbali ya wafanyabiashara hao, CCM pia imewaalika wawekezaji, makampuni makubwa wabunge na makada wake ambao pia ni wafanyabiashara wakubwa, kuchangia harambee hiyo.

Baadhi ya wafanyabiashara waliotajwa kualikwa kwenye harambee hiyo ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Kikwete ni pamoja na Yusuf Manji, Tanil Sumaiya, Shubash Patel na wengine.

Somaiya anatajwa katika kashfa ya ununuzi wa rada ya kijeshi kutoka Kampuni ya BAE System ya Uingereza ambapo wahusika wanadaiwa “kulainisha” mikono ya watendaji serikalini ili inunuliwe kwa bei ya juu kuliko gharama yake ya kawaida.

No comments: