Sunday, April 4, 2010

Vigogo watapeliwa mil. 300/-

na Christopher Nyenyembe, Mbeya



HALI si shwari katika mkoa wa Mbeya baada ya kuzuka wimbi zito la mtandao mkubwa wa matapeli wanaotumia fedha za Kimarekani (dola) na fedha za hapa nchini ambapo zaidi ya sh milioni 300 zimetapeliwa kutoka kwa wafanyabiashara sita maarufu mkoani humo katika kipindi cha mwezi mmoja.

Miongoni mwa wafanyabiashara wanaodaiwa kutapeliwa kiasi kikubwa ni kigogo mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani hapa (jina tunalo), ambaye inadaiwa muda mfupi baada ya kufanyiwa utapeli huo, alipatwa na shinikizo la damu.

Taarifa kutoka ndani ya familia ya kigogo huyo na majirani wa karibu zinadai kuwa walimsihi baba yao asijiingize kwenye mtego wa matapeli hao lakini aliwapuuza na kujikuta akitumbukia na kuibiwa kiujanja mamilioni ya fedha.

Habari ambazo Tanzania Daima Jumapili imezipata na kuzifanyia uchunguzi kwa takriban mwezi mmoja umeonyesha kuwa mtandao huo umekuwa ukifanya kazi kubwa ya kuwatapeli fedha wafanyabiashara mbalimbali ambao kwa kutumia mbinu na ushawishi wa hali ya juu kila aliyelizwa hutumwa kumtafuta mfanyabiashara mwenzake.

Baadhi ya wafanyabiashara waliokumbwa na mkasa huo, majina yao tunayo, walieleza jinsi walivyoweza kutapeliwa wakijua kuwa wameingia kwenye mikono salama lakini baadaye hujikita fedha zao walizozitoa kwa lengo la kupata kiasi kikubwa cha fedha nazo zikiishia kwa matapeli hao.

Matukio mengine yaliyoweza kuthibitishwa na gazeti hili na kwa wafanyabiashara tofauti tofauti, zinaonyesha wafanyabiashara kutoka Wilaya ya Chunya ndio waliotapeliwa fedha nyingi kiasi cha sh milioni 130 ndani majina yao tunayo ambapo mmoja anadai kutapeliwa kiasi cha sh milioni 90.

Wafanyabiashara wanaofuatia kwa kutapeliwa ni wa jijini Mbeya ambao zaidi ya sh milioni 120 zimetapeliwa kwa nyakati tofauti, ikifuatia wilaya ya Rungwe ambako mfanyabiashara mmoja alitapeliwa kiasi cha sh milioni 15 na kuwa wengine walioweza kutapeliwa kiwango cha chini ni sh milioni 10.

Mfanyabiashara huyo alisema na kuwataja wenzake kuwa baada ya kuvutiwa na fedha hizo ambazo huelezwa kwamba zinaletwa na Mmarekani mmoja na zingine hupewa maelekezo na Mtanzania mwenye asili ya kiasia kwa njia ya simu baada ya kuunganishwa na matapeli hao ili kuweka mambo sawa.

Miongoni mwa wafanyabiashara hao, wamethibitisha kwenda kutoa taarifa kwenye Ofisi ya Afisa Upelelezi wa Mkoa (RCO) na kupewa askari wa kufuatilia lakini kinyume chake waathiriwa hao hupigiwa simu mbele ya polisi na matapeli hao kuwa wamepata habari za kwenda kutoa taarifa polisi.

“Hii hali inatutisha, tumekwenda polisi kutoa habari kwa siri baada ya muda mfupi hao matapeli wanatupigia simu za vitisho kuwa hata tuende wapi wao wanapata habari, yuko polisi aliyetuambia kuwa hawezi kwenda sehemu walipo kwa kuwa wanamfahamu,” alilalamika mfanyabiashara mmoja.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi, alipohojiwa kuhusiana na tukio hilo, alisema hana habari kuwepo mtandao huo na hajui kama ofisi yake inafahamu jambo hilo kwa vile wakati matukio hayo yanatokea hakuwepo ofisini.

“Taarifa niliyonayo hapa ni ya utapeli ya sh milioni 7 za dhahabu bandia, sina habari kama ofisi yangu inazo taarifa za kuwepo kwa utapeli mkubwa kiasi hicho, nashukuru hii kazi itabidi niifanye mimi mwenyewe,” alisema Kamanda Nyombi.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huo, alipohojiwa kuhusu utapeli huo, alisema hajapewa taarifa na vyombo vinavyohusika.

“Kwanza hawa wanaotapeliwa ni wajinga haiwezekani mtu una pesa zako unampelekea mtu mwingine usiyemjua, wananchi wanapaswa kuwa makini, kama wanataka kukopa benki zipo huo ni upuuzi, ninachotaka kusema kawaida naletewa taarifa kuhusu hali ya usalama na timu yangu ya kazi bado sijapewa taarifa kuhusu utapeli huo,” alisema Mwakipesile.

No comments: