Saturday, November 21, 2009

RC adaiwa kuikosesha halmashauri mapato

na Sammy Lothy, Maswa




BARAZA la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, mkoani Shinyanga, limemtupia lawama Mkuu wa Mkoa, Dk. Yohana Balele, kuwa ndiye chanzo kikubwa cha halmashauri hiyo kutofikia malengo yake ya makusanyo ya mapato ya ndani yanayotokana na ushuru wa zao la pamba msimu wa 2009/2010.

Wakizungumza katika kikao hicho kilichofanyika juzi, madiwani hao walisema kitendo cha wanunuzi wa zao la pamba katika msimu huu kutolipa fedha za ushuru wa kununulia zao hilo katika halmashauri zote za Mkoa wa Shinyanga kabla ya kuanza manunuzi, kumeikosesha halmashauri hiyo mapato zaidi ya sh 600,955,289.

Walisema tangu awali walimtahadharisha mkuu huyo wa mkoa kuwa agizo lake hilo huenda likasababisha halmashauri kutoweza kufikia malengo ya kukusanya ushuru wa sh bilioni moja, lakini alipinga ushauri huo.

“Mheshimiwa mwenyekiti, sisi madiwani tulijaribu kumshauri mkuu wetu wa mkoa kuwa wanunuzi wa zao la pamba si waaminifu, hivyo agizo lake la kuwaruhusu kununua zao hilo kabla ya kulipia ushuru zitaikosesha mapato halmashauri yetu, lakini alipinga ushauri wetu, sasa miradi yetu tuliyopanga hatuwezi kuitekeleza,” alisema Diwani wa Kata ya Ipililo, Silvestre Kasulumbayi (CHAUSTA).

Alieleza kuwa, kitendo cha mkuu wa mkoa kuingilia na kuizuia halmashauri kutotekeleza moja ya majukumu yake ya lazima na ya kisheria, kwa kuamua kuwatetea wanunuzi wa pamba, ni kuimarisha matabaka ya walionacho wavune hata wasichostahili, jambo ambalo ni kinyume na utawala bora.

Walisema kuwa, kitendo hicho kinadhihirisha wazi jinsi serikali kuu zinavyopokonya madaraka ya halmashauri za wilaya, na hivyo kushindwa kuwahudumia wananchi wake katika kutekeleza mipango waliyojiwekea katika kipindi cha mwaka 2009/2010.

Naye Ofisa Ushirika wa Wilaya ya Maswa, Godfrey Mzava, alisema licha ya kujaribu kuyakamata baadhi ya magari ya makampuni yanayonunua zao hilo na kukwepa kulipa ushuru katika wilaya hiyo ili yaweze kulipa, lakini amekuwa akikutana na vikwazo mbalimbali kutoka katika ofisi ya mkuu wa mkoa, jambo ambalo limemfanya akate tamaa kwani linahatarisha ajira yake.

Alisema licha kuyaandikia barua makampuni yanayodaiwa na madeni yao, lakini hakuna utekelezaji wowote hivyo kuwaomba madiwani kutoa ridhaa ya kuyafikisha makampuni hayo mahakamani.

No comments: