Saturday, November 21, 2009

Kikwete aumbuka

• Umeme wakatika mara tatu akiwahutubia marais wenzake


na Ramadhani Siwayombe na Violet Tillya, Arusha




TATIZO la umeme ambalo hivi sasa limeanza kuonekana kama mazoea kwa wakazi wa mji wa Arusha, jana lililiaibisha taifa wakati Rais Jakaya Kikwete akihutubia marais watano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kwenye hafla ya utiaji saini mkataba wa soko la pamoja wa jumuiya hiyo mjini hapa.

Marais walioshuhudia adha hiyo ya umeme ni Piere Kurunzinza wa Burundi, Mwai Kibaki, Kenya; Paul Kagame, Rwanda na Yoweri Museveni wa Uganda.

Rais Kikwete akiwa anazungumza katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) baada ya kuthibitishwa kuwa mwenyekiti mpya wa EAC, ghafla umeme ulikatika na taa za ukumbini kuzimika.

Hali hiyo iliwafanya maofisa usalama kuzunguka haraka meza kuu waliyokuwa wameketi viongozi hao wa nchi za EAC kwa ajili ya kulinda usalama wao.

Baada ya sekunde chache kupita, umeme ulirejea tena na Rais Kikwete kuendelea kusoma hotuba yake, lakini ghafla aliikatisha tena baada ya umeme kukatika kwa mara ya pili na taa za ukumbini kuzimika.

Hali hiyo ilionekana dhahiri kumkera Rais Kikwete mbele ya ugeni huo, huku viongozi wa mkoa wakikimbizana huku na kule kuhakikisha umeme unarejea katika hali ya kawaida. Hali ya kukatika na kurejea kwa umeme iliendelea tena mara ya tatu.

Hata hivyo, haikujuliakana mara moja kama jenereta inayotumika kuzalisha umeme wa dharura katika ukumbi huo ilikuwa imeharibika au la.

Wakati umeme ukikatika AICC, katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid ambako hafla ya utiaji saini ya mkataba wa soko la pamoja ilipaswa kufanyika, mvua kubwa ilinyesha na kusababisha marais hao kushindwa kufika kwa wakati uliopangwa na kuwaacha maelfu ya wananchi waliofika uwanjani hapo kushuhudia tukio hilo la kihistoria wakiduwaa.

Ukiachia dosari ya kukatika-katika kwa umeme, Rais Kikwete alichaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa EAC, akirithi nafasi hiyo kutoka kwa aliyekuwa mwenyekiti wa awali, Rais Kagame.

Hata hivyo, nafasi hiyo ilipaswa kuchukuliwa na Rais Kurunzinza kwa mujibu wa utaratibu, lakini alilazimika kumuachia Rais Kikwete kwa kuwa Burundi inatarajia kufanya uchaguzi mkuu mapema mwakani, hivyo angeshindwa kumaliza muda wake wa urais wa EAC.

Baada ya kuchaguliwa, Rais Kikwete aliongoza jopo la marais wenzake kusaini mkataba wa soko la pamoja kwa nchi wanachama wa jumuia hiyo kabla ya kwenda kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Makao Makuu ya jumuiya hiyo, yaliyopo jirani na majengo ya AICC.

Katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid ambako awali mkataba huo ulipaswa kusainiwa, mvua kubwa iliyonyesha, ilisababisha maelfu ya wakazi wa Arusha waliofurika kushuhudia tukio hilo kulowa baada ya kukosa mahala pa kujibanza kutokana na uwanja huo kuwa na jukwaa moja lenye paa.

Baadhi ya wananchi waliwahurumia wanafunzi waliokuwepo uwanjani hapo tangu asubuhi, wakinyeshewa mvua na hata kushindwa kupata chakula cha mchana, wakisubiri ujio wa marais hao.

Kwa upande wa wafanyabiashara, nao walilalamikia kitendo cha uongozi wa Mkoa wa Arusha kuwapa barua za kuwataka kufunga maduka yote yanayozunguka uwanja huo na maeneo ya jirani, hali ambayo imeathiri biashara zao.

Wananchi walianza kukusanyika ndani ya uwanja huo kuanzia majira ya saa mbili asubuhi kama walivyotangaziwa na viongozi wa mkoa na hafla hiyo ilitarajiwa kufanyika saa nne asubuhi.

Marais hao walichelewa kufika uwanjani hapo kwa kile kilichodaiwa kuwapo kwa mvutano wa baadhi ya vipengele vya mkataba ambapo baadhi yao walitofautiana.

Ukiachia adha ya mvua na kuchelewa kwa viongozi kuwasili uwanjani hapo, maelfu ya wananchi walifurika kwa lengo la kutaka kuwasikiliza.

Baadhi ya shughuli zilizokuwa zikifanyika uwanjani hapo, ni pamoja na utoaji zawadi kwa washindi wa mashindano ya wabunge kutoka mabunge ya EAC ambapo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, liliibuka mshindi katika mchezo wa soka dhidi ya Bunge la Uganda.

Naye Waziri wa Ushirikiano wa EAC, Dk. Diodorus Kamala, alisema mkataba huo utaanza rasmi Julai mwakani baada ya nchi wanachama kuridhia.

Akizungumzia masuala ya ajira mara baada ya nchi hizo kuwa na soko la pamoja, Dk. Kamala alisema kila nchi itaeleza kwanza mfumo wa ajira zake na kutoa nafasi kulingana na nchi husika kwa wananchi wa EAC.

Alisema wananchi wa jumuiya hiyo, wataendelea kutumia paspoti zao kama kawaida hadi hapo maridhiano yatakapokamilika.

No comments: